Ripoti ya CAG inaeleza nini kuhusu utawala wa Rais Samia?

    • Author, Ezekiel Kamwaga
    • Nafasi, Mwandishi

Mmoja wa wanasiasa mashuhuri nchini Tanzania alipata kuniambia wakati mmoja kwamba kwa kawaida mijadala ya masuala makubwa nchini humo huwa ina tabia ya kudumu kwa saa zisizozidi 72 (siku tatu). Kama ukiwa na subira kwa muda huo, mjadala utaisha na Watanzania wataingia kwenye suala lingine.

Hata hivyo mojawapo ya masuala ambayo yameingia katika utamaduni wa siasa za Tanzania na kudumu kwenye mijadala ya kisiasa ni suala la ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, CAG anatakiwa kukabidhi ripoti za hesabu zilizokaguliwa za Serikali bungeni kila mwaka kwa ajili ya kujadiliwa na kuchukuliwa kwa hatua. Katika kipindi cha walau miaka 15 iliyopita, ripoti hii imekuwa chanzo cha mijadala mikali ya kisiasa nchini humo.

Mjadala wa mwaka huu ya 2021/2022 ni muhimu katika utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa vile hii inachukuliwa kama ripoti ya kwanza ya utawala wake – ya mwaka 2020/2021 iliandaliwa zaidi kwenye siku za mwisho za utawala wa mtangulizi wake, hayati John Magufuli.

CAG ameona nini?

Mjadala wa mwaka huu ulifunguliwa na Rais Samia mwenyewe mwishoni mwa mwezi uliopita. Akipokea ripoti hiyo kutoka kwa CAG Charles Kichere, Rais huyo wa kwanza mwanamke nchini Tanzania alionesha kukerwa na kiasi kwamba alizungumza neno “pumbavu” ambalo hajawahi kusikika akilizungumza tangu awe Rais mwezi Machi mwaka juzi.

Kilichomkera Rais Samia kilikuwa ni kitendo cha kuongezeka kusiko na maelezo kwa gharama ya ndege mpya ya mizigo ambayo serikali imeagiza kwa ajili ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL). Rais alieleza kwamba wakati gharama ya awali iliyokubalika ilikuwa ni dola milioni 37 serikali ililetewa bili ya dola milioni 86.

“Invoice imekuja tunatakiwa kulipa dola milioni 86. Unauliza mkataba ulisemaje? Hii imetokea wapi? Unaambiwa vifaa vimepanda bei, nauliza mkataba wetu ulisemaje? Mtu anapokea bila kuuliza anailetea serikali ilipe. Stupid,” alisema Rais Samia akiwa Ikulu.

Kwa sababu ya ukali ulioonyeshwa hadharani na Rais, watu wengi walikuwa wakisubiri kwa hamu siku ambayo ripoti hiyo itafikishwa bungeni ambako ndiko kisheria itawekwa hadharani na kuruhusiwa kujadiliwa ndani na nje ya Bunge.

Mwaka huu, mijadala ya ripoti hiyo ilijikita zaidi katika masuala tofauti kama vile upotevu wa fedha kupitia mikopo kwa wanawake, vijana na walemavu, mikataba mibovu kwenye ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kwa kipande cha 3 na 4, hali mbaya ya Mfuko wa Bima ya Afya, gharama kubwa zisizo na sababu za utekelezaji wa Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere na upotevu wa fedha katika wizara, idara, taasisi za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.

Mengi ya yaliyotajwa kwenye ripoti ya sasa yamekuwa mambo ya kawaida katika ripoti za CAG. Katika kitabu cha maisha ya CAG mstaafu, Ludovick Utouh, kiitwacho Uwajibikaji katika Kalamu Isiyo na Wino alilalamika kwamba tatizo kubwa liko kwenye ukweli kwamba mara nyingi mijadala na uchungu huonekana wakati ripoti inatoka lakini baada ya muda mfupi, Watanzania huhamia kwenye mijadala mingine na maisha kuendelea kama kawaida.

Katika uchambuzi wake wa ripoti ya mwaka huu, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema kinachoonekana ni kwamba “mambo ni yaleyale, watu ni walewale na kinachofanyika ni kilekile”.

Uchambuzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, ulimtaka Rais Samia kuchukua hatua dhidi ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kwa vile mambo ya hovyo yaliyoibuliwa na CAG yamefanyika wakati yeye akiwa msimamizi mkuu wa shughuli za serikali.

Muktadha wa ripoti ya mwaka huu

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Zitto alisema pamoja na kasoro zilizojionyesha, jambo zuri lililojitokeza ni kwamba angalau kumekuwa na uwazi mkubwa kwenye kuijadili ripoti hiyo kulinganisha na hali ilivyokuwa wakati wa Magufuli.

“Miaka mitatu tu iliyopita, tulikuwa tunalipia hoteli kwa ajili ya kuja kuzungumzia mambo haya ya CAG lakini baadaye mwenye hoteli anakurudishia fedha zako na kukuambia kwamba akiruhusu atashughulikiwa kibiashara. Hii kwamba leo tumekaa wote na tunajadiliana kwa uwazi, ni hatua muhimu,” alisema.

Wakati wa utawala wa Magufuli, aliwahi kuingia kwenye mgogoro mkubwa na mtangulizi wa Kichere, Profesa Mussa Assad, ambaye alionekana kama mkosoaji mkubwa wa mwenendo wa matumizi ya serikali yake. Mgogoro huo ulisababisha hatimaye Bunge likatae kufanya kazi naye – jambo lililofanya aondolewe kwenye wadhifa wake kinyume cha taratibu.

Kuimarika kwa uhuru wa CAG kukagua na kutoa mapendekezo yake, uhuru wa wabunge na vyombo vya habari kujadili kilicho ndani ya ripoti na utayari wa Rais kuchukua hatua dhidi ya mapendekezo yaliyotolewa kwenye ripoti hiyo kunaelezwa kama hatua muhimu kwenye eneo la uwajibikaji nchini Tanzania.

Tayari Rais Samia amechukua hatua ya kuvunja Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) kutokana na kashfa ya ununuzi wa mabehewa na vichwa vya treni lakini amemsimamisha kazi aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), Mhandisi John Nzulule, kupisha uchunguzi wa suala hilo la ununuzi wa ndege.

Jambo kubwa kihasibu ambalo serikali ya Rais Samia imeweza kulifanya ni kuweka uwiano wa mapato na matumizi ya kwenye fedha zilizoingia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Suala la matumizi ya fedha zilizo kwenye mfuko huo ndizo zilizosababisha mgogoro wa kwanza baina ya Magufuli, Zitto na Profesa Assad mwaka 2018 kutokana na ukaguzi wa hesabu za mwaka 2016/2017.

Mwaka huo, Zitto alibaini tofauti ya kiasi cha shilingi trilioni 1.5 baina ya makusanyo ya serikali na kiasi kilichotumika. Serikali ilikuwa imekusanya shilingi trilioni 25.3 lakini taarifa ikaonyesha ilikuwa imetumia shilingi trilioni 23.79. Swali kubwa na lililoonekana kuikera serikali ya Magufuli wakati ule ilikuwa kwamba wapi zilikopelekwa shilingi trilioni 1.5?

Katika ripoti ya mwaka huu – ambayo CAG pia aliruhusiwa kukagua mfuko huo, serikali ilikusanya shilingi trilioni 35.486 lakini matumizi yakawa shilingi trilioni 36.063.

Nakisi ya shilingi bilioni 577 inayoonekana kwenye matumizi – kwa mujibu wa CAG, ni kutokana na fedha zilizoingizwa moja kwa moja kwenye miradi ya wafadhili pasipo kupitia serikalini na mapato mengine ambayo hayakuwa yameingizwa kwenye hesabu za mfuko hadi wakati hesabu zinafungwa.

Tayari CAG mstaafu, Utouh na wanaharakati wa mazingira kama Profesa Felician Kilahama, wamepongeza hatua za awali zilizochukuliwa na Rais Samia baada ya kukabidhiwa ripoti ya mwaka huu.

Hata hivyo, nikinukuu maneno ya kiongozi aliyenieleza kuhusu tabia ya Watanzania mwanzoni mwa makala haya, jambo linalosubiriwa kwa hamu ni kuona kama Rais atatimiza mapendekezo ya CAG kama yalivyo kwenye ripoti kwa utimilifu wake, au historia itaendelea kubaki ya “yaleyale”.

Lakini jambo la kwanza lililo dhahiri kwenye mjadala wa safari hii wa ripoti ya CAG ni kwamba angalau watu wanaijadili kwa uwazi; ndani na nje ya Bunge la Tanzania.