'Sisi ni upinzani': Hamas yatangaza mapambano - Gazeti la The Observer

Hamas

Chanzo cha picha, Getty Images

The Observer ilichapisha ripoti ya mwandishi wake huko Ramallah, Sufyan Taha, na mwandishi wake huko Jenin, Jason Burke, yenye kichwa cha habari "Sisi ni upinzani: Hamas yatangaza mapambano katika mazishi ya waathiriwa huko Jenin."

Ripoti hiyo inaelezea hali ilivyokuwa baada ya mazishi huko Jenin, ambapo washiriki walianza kutawanyika katika mitaa ya katikati mwa jiji.

Wengine walikwenda msikitini, wengine majumbani mwao, na wengine walikwenda kununua sharobati au chai kwa wafanyabiashara wa mitaani, lakini wengi walikuwa wamebeba silaha, na wote walikuwa vijana.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa tukio hili lilitokea siku moja baada ya Israel kuuvamia mji huo ulioko kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, ambao ulimalizika kwa mapigano makubwa yaliyoshuhudia vifo vya Wapalestina 14.

Ripoti hiyo inaendelea kuwa jeshi la Israel, kwa upande wake, lilieleza kwamba lilimkamata “mmoja wa viongozi wa magaidi, likaharibu kundi la kigaidi,” likabomoa miundombinu yake, na kunyakua silaha na mabomu.

Ripoti hiyo inaelezea hali ilivyokuwa wakati wa mazishi ya waathiriwa, kwani mmoja wa vijana hao anasema huku macho yake yakiangaza akiwa amevaa kinyago usoni, "Tunapinga uvamizi kila mahali, huko Gaza, katika Ukingo wa Magharibi, sisi sote ni wamoja.”

Ripoti hiyo inabainisha kuwa wanajeshi wa Israel na walowezi wameua Wapalestina 176 katika Ukingo wa Magharibi tangu kuanza kwa vita huko Gaza mwezi uliopita, huku mashambulizi ya Wapalestina yakiua Waisraeli 3, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, huku Israel ikiwakamata zaidi ya Wapalestina 2,500 katika ukingo wa Magharibi ikiwatuhumu kwa kupanga mashambulizi dhidi yake.

Ripoti hiyo inahusu suala la mrithi wa Mahmoud Abbas, ambaye ana umri wa miaka 87, na imani ya wachunguzi wengi kwamba mgombea wa karibu zaidi ni Hussein Al-Sheikh, mmoja wa wasaidizi wake wa karibu, ingawa Marwan Barghouti anahesabiwa kuwa maarufu zaidi, ingawa amekuwa kizuizini katika jela ya Israel kwa muda mrefu na Wapalestina wanamtaja kuwa ni "Mandela wa Palestina."

Ripoti hiyo inaongeza kuwa wafuasi wa Mamlaka ya Kitaifa ya Palestina wanasema kwamba hapo awali ilianzishwa kama mamlaka ya mpito ya kujenga taasisi za utawala na mamlaka muhimu kwa ajili ya kuanzishwa kwa taifa la Palestina, lakini hilo halikufanyika, huku wakikiri kwamba Hamas ilipata umaarufu kwa kiasi kikubwa.

Ripoti hiyo inaendelea kusema kuwa Jenin imekuwa ikilengwa jeshi la Israel, ambako kuna mamia ya wanamgambo wenye mafungamano na Hamas, jambo ambalo linaleta changamoto kubwa kwa serikali ya Israel, na lengo lake lililotajwa la kuliondoa vuguvugu la Hamas na kuharibu miundombinu yake.

Sehemu ya uharibifu huko Gaza

Chanzo cha picha, Getty Images

"Suluhu ya serikali mbili"

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika The Guardian, tunasoma makala ya Ahmed Samih Khalid yenye kichwa cha habari, "Kama msuluhishi wa zamani wa Palestina, najua kuwa suluhisho la serikali mbili lililopendekezwa na Biden ni udanganyifu mtupu."

Mwandishi huyo anasema kuwa hauoni mwisho wa mchezo wa kisiasa unaofanywa na serikali ya Israel, kuua watu huko Gaza, kwa uungaji mkono wa washirika wake wa Magharibi, kwa kisingizio kwamba inajilinda, na bila kujali.

Mwandishi huyo anasema kuwa, lengo la kwanza la Israel ni kwamba harakati ya Hamas lazima ifutwe kabisa na kusambaratisha uwepo wake wa kijeshi na kisiasa katika Ukanda wa Gaza.

Lengo la pili ni kutoruhusu kurejea kwa hali hii siku za usoni, ambayo ina maana kwamba utawala utakaorithi Hamas lazima uwe na utulivu.

Mwandishi huyo anaeleza kuwa licha ya kuwepo tofauti za wazi katika ngazi ya kijeshi kati ya Israel na Hamas, harakati hiyo imeenea kijeshi na kijamii katika Ukanda wa Gaza, na imeenea katika eneo hilo na ina wafuasi wengi, miongoni mwa harakati zinazojitanua na kubwa zaidi kama vile Muslim Brotherhood, ambayo ina maana kwamba vuguvugu hilo lina uwezo wa kujiunda upya katika jamii ya Wapalestina.

Mwandishi anahitimisha kwa kutoa wito kwa Rais wa Marekani Joe Biden, na viongozi wengine, kwa wazo la suluhu ya mataifa mawili, ambayo ina maana kwamba vikosi vya kulinda amani vya Waarabu vitawekwa katika Ukanda wa Gaza, baada ya kumalizika kwa vita, na Mamlaka ya Kitaifa itachukua utawala wa Ukanda wa Gaza pamoja na Ukingo wa Magharibi, na kisha kufufua mchakato wa amani.

Mwandishi analichukulia suala hili kuwa ni udanganyifu mtupu, kwani mamlaka yoyote ya kudumu au ya kudumisha usalama huko Gaza kutokana na hatua za uhasama dhidi ya Hamas au harakati zozote zitachukuliwa na watu wa Palestina kama uvamizi na ukatili.

Mwandishi anabainisha kuwa kikwazo kikubwa zaidi kinachokabili suluhisho la serikali mbili ni Israeli yenyewe, kwa sababu hatua yoyote ya kweli katika mwelekeo huu lazima iegemee juu ya mabadiliko ya kweli ya hali iliyopo, ambayo ni dola moja, ambayo ni Israel.

Mwandishi anahitimisha kuwa utawala wa Biden, baada ya kuendelea kuiunga mkono Israel katika kufanya mauaji dhidi ya Wapalestina, ni vigumu kwake kumshawishi mtu yeyote kuzungumzia suala la amani, na pia hauna uzito wa kutosha wa kuweka migawanyiko inayoridhisha pande zote mbili.

Maelfu ya watu wameuawa wakati wa vita vinavyoendelea

Chanzo cha picha, Getty Images

'Waathirika ni wengi'

Gazeti la Financial Times lilichapisha ripoti ya baadhi ya waandishi wake yenye kichwa "Blinken asema majeruhi ni wengi katika vita vya Hamas na Israel."

Ripoti hiyo inasema kuwa matamshi ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken, yanatoa mwanga juu ya shinikizo la kimataifa linalotolewa na jumuiya ya kimataifa dhidi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na serikali yake, ambalo linaelezwa kuwa kali zaidi katika historia ya Israel, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya waathirika.

Ripoti hiyo inaongeza kuwa taarifa hizo zilikuja siku ya Ijumaa baada ya maafisa wa Palestina kusema kuwa wanajeshi wa Israel walishambulia kwa mabomu hospitali kaskazini mwa Gaza, ambako maelfu ya watu waliokimbia makazi yao wanakaa, wakikimbia uvamizi wa Israel.

Ripoti hiyo inamnukuu Blinken akisema wakati wa ziara yake nchini India, "Juhudi zaidi lazima zifanywe kulinda raia na kuhakikisha kuwa misaada inawasilishwa kwao. Wapalestina wengi wameuawa, na wengi wameteseka sana katika wiki zilizopita.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa taarifa za Blinken sio pekee katika suala hili.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema katika mahojiano na BBC kwamba Israel lazima "ikomeshe mauaji ya raia na watoto wachanga huko Palestina," ambayo ina maana kwamba kauli za Blinken ziliweka shinikizo zaidi la kimataifa kwa Israel, na mfumo wake wa mahakama, kuchunguza hatua zilizochukuliwa wakati wa vita.

Ripoti hiyo inaashiria kuwa pamoja na kwamba Marekani bado haijatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano huko Gaza, lakini mara kwa mara imekuwa ikitoa wito wa kuwepo kwa mapatano ya kibinadamu ili kuruhusu misaada zaidi ya kibinadamu na matibabu kupita katika Ukanda huo uliozingirwa.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa Marekani inataka Mamlaka ya Kitaifa kuchukua udhibiti wa hali ya Ukanda wa Gaza baada ya kumalizika kwa vita, kufuatia miaka 16 ya kuzingirwa kwa nguvu kwa Ukanda huo, ambayo ilisababisha umaskini wa watu bila kudhoofisha harakati za Hamas au kubomoa miundombinu yake.

Kwa upande mwingine, ripoti hiyo inahitimisha kwamba Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema katika taarifa kwa vyombo vya habari vya Israel kwamba baada ya kumalizika kwa vita huko Gaza, "kutakuwa na udhibiti kamili wa usalama wa Israel katika Ukanda wa Gaza, na hii ni pamoja na kupokonya silaha .”