Jinsi mzozo wa Israel na Gaza unavyoathiri vita vya Ukraine na Urusi

Chanzo cha picha, Getty Images
Mapema mwezi Novemba, Ukraine iliripoti kuwa karibu maeneo 120 yalishambuliwa kwa mabomu katika muda wa saa 24 zilizopita, likiwa ni shambulio kubwa zaidi tangu kuanza kwa mwaka huu.
Hata hivyo, nadhari ya dunia inaendelea kulenga Gaza na Israel.
Uwezekano wa kupungua kwa uungwaji mkono wa kimataifa imekuwa hofu kuu ya Ukraine tangu uvamizi wa Urusi uanze.
Bila msaada wa kijeshi na kifedha wa washirika wake, Kyiv ingekuwa na nafasi ndogo ya kukabili Urusi kwenye uwanja wa vita na kudumisha ulinzi wake wa anga, ambao ni muhimu kwa ulinzi wa miji ya Ukraine.
Tuangazie baadhi ya mabadiliko makubwa ambayo yametokea katika vita vya Urusi na Ukraine katika mwezi uliopita.
Vita vya uasi
Wachambuzi wengi wanaamini kwamba upande ambao unaweza kuendeleza hasara kwa muda mrefu zaidi hatimaye utashinda vita.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kamanda Mkuu wa Ukraine Valery Zaluzhny pia amezungumza juu ya "vita vya uasi."
“Kama vile katika Vita vya Kwanza vya Ulimwengu, tumefikia kiwango cha kiteknolojia ambacho hutuweka katika hali ngumu,” amesema katika makala ya jarida la The Economist.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Anaonyesha wasiwasi wake juu ya mashambulizi ya miezi mitano ya kutwaa tena eneo lililokaliwa na Urusi, akisema jeshi la Ukraine limeweza kusonga mbele kilomita 17 pekee.
Kwa sasa Urusi inadhibiti karibu 17.5% ya eneo linalotambulika kimataifa la Ukraine.
Katika wiki za hivi karibuni, mapigano yameongezeka karibu na mji wa Avdiivka mashariki mwa Ukraine, ambapo pande zote mbili zinakabiliwa na hasara kubwa lakini zinapiga hatua ndogo. Wizara ya Ulinzi ya Uingereza inakadiria kuwa hasara ya Urusi huko Avdiivka inaweza kuwa mbaya zaidi mnamo 2023.
Jenerali Zaluzhny kisha alieleza jinsi pande zote mbili sasa zilivyo na teknolojia ya hali ya juu inayowawezesha kuona kile ambacho upande mwingine unafanya. Matokeo yake, alisema, hakuna hata mmoja anayeweza kusonga mbele na kufikia malengo yao.
Alitoa wito kwa washirika kuipatia Ukraine silaha zenye usahihi zaidi, teknolojia ya kujikinga dhidi ya silaha na vifaa vya kuondoa mabomu yaliyotegwa chini ya ardhi ikiwa ni pamoja na roboti.

Chanzo cha picha, Getty Images
Marekani na Ukraine
Kasi na urahisi wa washirika wa Magharibi wa Ukraine kuipatia silaha mpya na msaada wa kifedha inachunguzwa, kwa kuzingatia uchaguzi wa rais mpya wa Bunge la Marekani.
Mwakilishi Mike Johnson wa Republican kutoka Louisiana, alichaguliwa kwa wadhifa huo wa juu mnamo Oktoba 25.
Hapo awali, Rais wa Marekani Joe Biden aliliomba Bunge kuidhinisha mfuko wa ufadhili wa usalama wa dola bilioni 106, ambao ulijumuisha msaada wa dola bilioni 61 kwa Ukraine.
Msemaji huyo mpya alitanguliza uungaji mkono wa Marekani kwa Israel, akisema kwamba wakati Marekani "haiwezi kuruhusu Vladimir Putin kutawala Ukraine, ni lazima tumuunge mkono mshirika wetu muhimu katika Mashariki ya Kati, ambaye ni Israel.
Mike Johnson alisema ingawa anaunga mkono msaada zaidi kwa Ukraine, Ikulu ya White House pia inahitaji kuweka wazi majukumu na malengo.
Afisa mkuu wa usalama wa Kiev, Oleksiy Danylov, alipuuzilia mbali suala hilo: "Tuna furaha kutoa taarifa zote kuhusu msaada huo, hakuna siri."
Hata hivyo, hata kama msaada zaidi utaidhinishwa, kunaweza kuwa na ucheleweshaji unaogharimu maisha kwenye uwanja wa vita.
Baadhi ya wajumbe wa Bunge la Marekani tayari wanataka kukata misaada kwa Ukraine na kuielekeza Taiwan.

Chanzo cha picha, Getty Images
Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky amekanusha ripoti za vyombo vya habari kwamba maafisa wa Marekani na Ulaya walikuwa wakishinikiza Kyiv kufanya mazungumzo na Moscow.
"Kila mtu anajua mtazamo wangu, unaofanana na ule wa jamii ya Ukraine ... Hakuna mtu anayenipa shinikizo (kwa mimi kufanya mazungumzo), sio viongozi wa EU au wale wa Marekani," alisema wakati wa mkutano na vyombo vya habari pamoja na mkuu wa Tume ya Ulaya, Ursula von der Leyen, mjini Kyiv, Jumamosi (4/11).
Alikataa uwezekano wa kufanya mazungumzo yoyote na Urusi, lakini alikiri kwamba vita vya Mashariki ya Kati vilivuruga nadhari upande wa Ukraine.
Akitoa wito wa jenerali wake mkuu, alitoa kwa washirika wake wa kimataifa - "Marekani, Ulaya, Asia" - kuendelea kuisaidia Ukraine kwa sababu Kiev "inatetea maadili ya kawaida" kama vile demokrasia.
Akizungumza katika mahojiano na shirika la utangazaji la Amerika Kaskazini NBC, alisema mbadala ni hatari sana: "Ikiwa Urusi itatuua sote, itashambulia nchi za NATO."
Ukraine imeahidi kutwaa tena maeneo yote yanayokaliwa na Urusi, ikiwemo Crimea, iliyotwaliwa mwaka 2014.
Moscow imeelezea uvamizi kamili wa Ukraine kama "operesheni maalum ya kijeshi" iliyoanzishwa kujibu kile inachokiona kama Magharibi yenye uhasama na uchokozi.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alisisitiza kwamba vita "haviko kwenye mkwamo" na kwamba wanajeshi wa Urusi wanaendelea kusonga mbele kwenye uwanja wa vita.
Taarifa za kila siku kutoka kwa Wizara ya Ulinzi ya Urusi hazina marejeleo ya majeruhi au shida vitani. Badala yake, wanaorodhesha hasara za wanajeshi na vifaa kwa Ukraine.
Lakini wanablogu wa kijeshi wa Urusi wanawakosoa vikali makamanda wakuu kwa kushindwa kutoa mafunzo ya kutosha na msaada kwa vitengo vinavyopigana karibu na Avdiivka.
Kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya raia
Mojawapo ya wasiwasi mkuu wa Ukraine majira ya baridi yanapokaribia ni kuongezeka kwa mashambulizi ya Urusi dhidi ya miundombinu muhimu ya kiraia kama vile vyanzo vya nishati na njia za usafiri.
Kuongezeka kwa mashambulizi hufanya iwe vigumu kulinda ulinzi wa anga wa Ukraine.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ukraine inakabiliwa na mashambulizi ya kila siku ya mabomu yanayofanywa na mizinga, roketi, makombora na ndege zisizo na rubani. Maeneo yaliyo karibu na eneo la vita na ndani ya safu ya mizinga ya Urusi yanakabiliwa na viwango vya juu vya majeruhi na uharibifu.
Mnamo Oktoba 31, afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba "mashambulizi ya Urusi yanasababisha mateso yasiyofikirika kwa watu wa Ukraine na kwamba zaidi ya 40% yao wanahitaji msaada wa kibinadamu ".
Ramesh Rajasingham, mkurugenzi wa uratibu katika ofisi ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, alisema maelfu ya raia wameuawa katika mashambulizi tangu uvamizi wa Urusi Februari 2022.
Umoja wa Mataifa ulithibitisha rasmi vifo vya raia 9,900, lakini ukasema "idadi halisi hakika ni kubwa."
Ukrainians pia wanakabiliwa na kushuka kwa huduma za afya. Tangu uvamizi huo, Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa limerekodi zaidi ya mashambulizi 1,300 kwenye miundombinu ya afya, kama vile hospitali. Idadi hii inawakilisha zaidi ya 55% ya mashambulizi yote duniani kote katika kipindi hicho.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, tangu mwanzoni mwa Septemba mwaka huu, vituo vya afya 13 vimeshambuliwa na wahudumu wa afya na wagonjwa 111 wameuawa.
Mkataba wa mauzo ya nafaka
Mwezi uliopita, mamlaka ya Ukraine ilifanikiwa kusafirisha nafaka kupitia ukanda mwembamba wa pwani ya magharibi ya Bahari Nyeusi, kupitia maji ya eneo la Romania na Bulgaria, hadi Uturuki, katika juhudi za kujikinga na mashambulizi ya Urusi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mkataba huu unaruhusu tu usafirishaji wa kiasi kidogo cha nafaka. Inakadiriwa kuwa karibu tani milioni 1 za nafaka zimeondoka kwenye bandari za Ukraine kupitia njia hiyo mpya tangu mwezi Agosti.
Kabla ya uvamizi huo mkubwa, Ukraine ilisafirisha hadi tani milioni 6. Ingawa kiwango cha sasa cha mauzo ya nje ni nusu ya kile ilivyokuwa mnamo Oktoba 2022, bado ni cha juu kuliko ilivyotarajiwa.















