Palestina – Israel: Mambo matatu muhimu kuielewa awamu ya pili ya operesheni ya ardhini Gaza

Chanzo cha picha, EPA
"Wanajeshi wetu wako katika Ukanda wa Gaza, wamesambazwa kila mahali," maneno ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu akithibitisha siku ya Jumamosi - nchi yake inaanza awamu ya pili ya operesheni ya ardhini dhidi ya kundi la wanamgambo wa Palestina Hamas.
Tangu jeshi la Israel lianzishe mashambulizi hayo mapya kati ya Ijumaa jioni na Jumamosi asubuhi, machafuko yametawala katika Ukanda wa Gaza, ambapo maelfu ya watu wamelazimika kuyahama makazi yao, huku idadi ya waliouawa ikizidi 8,000. Mamia ya majengo ya ghorofa na maelfu ya nyumba yameharibiwa.
Eneo la Kusini ambako watu wengi walikimbilia baada ya Israel kuwataka kuondoka Kaskazini, mashambulizi pia yaliripotiwa, ingawa kwa kiwango kidogo.

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
"Hivi vitakuwa vita vya muda mrefu na vigumu," Netanyahu alisema katika hotuba ya televisheni siku ya Jumamosi.
Jumamosi iliyopita mawasiliano ya simu na intaneti yalikatika Gaza, na hivyo kufanya kuwa vigumu kujua nini kinaendelea huko. Mapema Jumapili asubuhi, iliripotiwa kuwa baadhi ya huduma za mtandao na simu za rununu zilirejea.
Katika taarifa iliyotolewa Jumapili hii, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limeripoti - maelfu ya wakaazi wa Gaza walivunja maghala na vituo vya usambazaji wa misaada vilivyoko kusini na katikati mwa Ukanda wa Gaza na kuchukua unga na mahitaji mengine.
"Hii ni ishara mbaya kwamba utaratibu wa kiraia unaanza kuporomoka baada ya wiki tatu za vita na kuzingirwa," Thomas White, mkurugenzi wa UNRWA katika Ukanda wa Gaza.
"Watu wana hofu, wamechanganyikiwa na wamekata tamaa. Mivutano na hofu inazidi. Wanajihisi kuwa peke yao na wametengwa."
Israel inasema nini kuhusu uvamizi wake?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Katika hotuba yake baada ya kukutana na jamaa za baadhi ya mateka wanaoshikiliwa na Hamas huko Gaza, Benjamin Netanyahu alieleza - lengo lake kuu ni kuwashinda Hamas na kuwaachia huru mateka.
Netanyahu alisema, "wanajeshi na makamanda wa Israel sasa wako katika Ukanda wa Gaza, wamesambaa kila mahali na operesheni inayoendelea ya ardhini ni hatua ya pili ya vita na Hamas."
Aliongeza, "Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) linachukua tahadhari kuwalinda raia na kuwashutumu Hamas kwa kufanya uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa kuwatumia watu wake kama ngao."
Netanyahu aliviweka vita hivyo katika muktadha mpana zaidi na kusema uingiliaji kati wa Gaza ni kama "vita vya pili vya uhuru wa Israeli."
"Tutapigana na hatutasalimu amri. Hatutarudi nyuma. Tutapigana juu na chini ya ardhi," alisema.

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC Paul Adams, mkakati wa jeshi la Israel umejikita katika awamu tatu. Awamu hii ya pili inalenga "kuondoa upinzani kutoka kwa Hamas.
Awamu ya kwanza ilikuwa ni kuharibu miundombinu ya kundi hilo na ya tatu itakuwa kuiondoa Israel katika Ukanda wa Gaza na kuanzisha hatua mpya za usalama kwa raia wa Israel.''
Jumamosi hii, pia iliripotiwa kuwa Hamas iko tayari kubadilishana mateka zaidi 220 inayowashikilia huko Gaza kwa wafungwa wa Kipalestina katika magereza ya Israel.
Katika maelezo yake, Netanyahu alisema suala hilo lilijadiliwa na baraza la mawaziri la vita la Israel, lakini alikataa kutoa maelezo zaidi.
Hali ikoje Gaza?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Milipuko mikubwa inaendelea kusikika Gaza. Kwa mujibu wa mamlaka ya Palestina, mamia ya majengo yameharibiwa kwa mashambulizi ya anga na makombora.
Jeshi la Israel linasema ndege zake za kivita zimeshambulia maeneo 150 ardhini, zikiwemo njia za chini ya ardhi na miundombinu mingine. Vifaru na wanajeshi pia waliingia Ukanda wa Gaza na kukabiliana na wapiganaji wa Hamas.
Tawi la kijeshi la kundi hilo limesema linapambana na wanajeshi wa Israel katika mji wa kaskazini mashariki wa Beit Hanoun na eneo la kati la Bureij, pia limeanzisha mashambulizi ya roketi dhidi ya Israel.

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Jumamosi asubuhi, Rushdi Abu Alouf, mwandishi wa habari wa BBC aliyeko Khan Younis kusini mwa Gaza, alielezea, milipuko ya mabomu katika eneo la kaskazini ni ya kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.
Aliongeza kulikuwa na mashambulizi machache katika mikoa ya kusini, lakini hofu inawakumba maelfu ya watu waliokimbilia huko.
Mpiga picha Shehab Younis aliweka video kwenye mtandao wa Instagram ikimuonyesha mtu aliyejeruhiwa vibaya akitolewa katika jengo na kusafirishwa kwa lori bila gari la kubebea wagonjwa.
William Schomburg, mkuu wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu huko Gaza, alisema hospitali zinafanya kazi usiku kucha kuwatibu waathiriwa.
"Niliweza kutembelea hospitali tofauti, ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Al-Quds, na matukio yanayotokea huko ni magumu kuelezea," alielezea.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), ambalo linasaidia zaidi ya watu 600,000 kati ya milioni 1.4 waliokimbia makazi yao, limesema limepoteza mawasiliano mengi na timu zake.
Mwitikio kuhusu mzozo huo ukoje?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) António Guterres alisema ameshangazwa na kuongezeka kwa mashambulizi, haswa baada ya makubaliano ya kimataifa ambayo yanataka kusitishwa kwa mapigano kutokana na hitaji la msaada wa kibinadamu kwa Gaza.
"Nimetiwa moyo na kile kinachoonekana kuwa maelewano yanayokua ndani ya jumuiya ya kimataifa - juu ya haja ya angalau kusitishwa mapigano kwa ajili ya misaada ya kibinadamu," Guterres alisema katika taarifa yake ya Jumamosi.
"Kwa bahati mbaya, badala ya kusitisha, nilishangazwa na ongezeko kubwa la milipuko ya mabomu na athari zake, na kudhoofisha malengo ya kibinadamu yaliyotajwa," aliongeza.
Siku ya Ijumaa, Umoja wa Mataifa uliidhinisha azimio la kutaka kusitishwa kwa mapigano - lililowasilishwa na Jordan kwa niaba ya nchi za Kiarabu na ambalo lilipata kura 120 za ndio, 14 zilipinga na 45 hazikupiga kura.
Israel ilikataa vikali pendekezo hilo.

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu pia ilitoa wito kwa Israel kusitisha mashambulizi, pamoja na kuachiliwa huru kwa mateka huko Gaza.
"Raia milioni mbili wamekwama Gaza bila pa kwenda," shirika hilo lilisema. Ni janga ambalo ulimwengu haupaswi kulivumilia," taarifa yake iliendelea.
"Kipaumbele cha juu ni kuokoa maisha, hiyo ina maana kuwezesha utoaji endelevu wa misaada," inasema taarifa isiyo ya kawaida ya kamati ya Mkataba wa Geneva. Ni mara chache kamati hiyo huzungumza hadharani kuhusu migogoro. Mara nyingi huchagua mawasiliano ya siri na wale wanaohusika.
Jumamosi hii maelfu ya watu walikusanyika katika miji tofauti ulimwenguni kutaka kusitishwa mapigano. Maandamano yalifanyika katika miji ya London, Paris, Rome, Copenhagen na Baghdad.

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Huko Istanbul, Uturuki, Rais Recep Tayyip Erdoğan alihutubia maelfu ya waandamanaji na kutangaza Israeli inatenda "uhalifu wa kivita."
Pia alikosoa viongozi wa mataifa yenye nguvu ya Magharibi kwa kutoingilia kati ili kusimamisha vita.
Bila kutaja jina la rais wa Uturuki, Netanyahu alielezea wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kwamba "wanafiki ni wale wanaolishutumu jeshi lake kwa kufanya uhalifu wa kivita. Sisi ndio jeshi lenye maadili zaidi ulimwenguni," alisema.
Israel iliamua kuwaondoa wanadiplomasia wake kutoka Uturuki Jumamosi mchana.














