Benjamin Netanyahu: Waziri mkuu wa Israel akataa kung'atuka licha ya tuhuma za ufisadi zinazomkabili

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akizungumza na vyombo vya habari

Waziri mkuu wa Israel Benjamini Netanyahu amekataa katakata kuondoka madarakani baada ya kushtakiwa na tuhuma za kutoa hongo, kufanya udanganyifu na kuwavunja imani raia waliomchagua kuhusiana na kesi tatu tofauti.

Alishtumu mashtaka hayo kama jaribio la mapinduzi dhidi yake. 'Sitakubali uongo kushamiri', alisema katika hotuba ya kupinga kesi hiyo.

Bwana Netanyahu alidaiwa kukubali kuchukua zawadi kutoka kwa wafanyabiashara matajiri na kutoa hongo ili kuweza kuwa katika vyombo vya habari mara kwa mara.

'Nitaendelea kuongoza taifa hili , kulingana na sheria ya nchi', aliongeza.

Katika hotuba ya dakika 15 , bwana Netanyahu alishutumu idara ya mahakama, maafisa wa polisi na wengine kwa kupanga njama dhidi yake wakiwa na nia yenye madai ya msukumo wa kisiasa.

''Katika mchakato huu mzima uliotiwa doa wachunguzi hawakuwa wakitafuta ukweli bali walikuwa wakinitafuta'' , alisema akiwashutumu wachunguzi hao kwa kuwahonga mashahidi ili kusema uongo.

Awali mwanasheria mkuu Avichai Mandelblit alisema kwamba alitoa uamuzi huo kwa 'moyo mzito' lakini akasema imeonyesha kwamba hakuna asiyeweza kushtakiwa nchini Israel.

'Hatuna budi kufuata sheria - sio swala la kisiasa' , alisema.

Tangazo hilo linajiri huku kukiwa na mkwamo wa kisiasa nchini Israel kufuatia chaguzi mbili kuu ambazo hazikutamatishwa mwezi Aprili na Septemba.

Siku ya Jumatano, mpinzani wa Bwana Netanyahu Benny Gantz alisema kwamba ameshindwa kubuni serikali ya muungano na walio wengi bungeni.

Alipewa fursa kujaribu baada ya Netanyahu kushindwa kufanya hivyo.

Wafuasi wa bwana Netanyahu walikongamana nje ya afisi ya waziri mkuu ili kupinga mashtaka hayo.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Wafuasi wa bwana Netanyahu walikongamana nje ya afisi ya waziri mkuu ili kupinga mashtaka hayo.
Maandamano pia yalifanyika dhidi ya waziri mkuu Netanyahu

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha, Maandamano pia yalifanyika dhidi ya waziri mkuu Netanyahu

Rais Reuven Rivlin aliwaomba wabunge siku ya Alhamisi kukubaliana kuhusu mtu atakayechukua wadhfa wa uwaziri mkuu katika kipindi cha siku 21 ili kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mwengine wa tatu.

Baada ya mashtaka hayo kutangazwa, bwana Gantz alichapisha ujumbe wa Twitter akimuunga mkono mwanasheria mkuu na maafisa wa polisi na kuandika 'ni siku ya kuhuzunisha'.

Je anakabiliwa na mashtaka gani?

Mwanasheria mkuu Mandelblit alisema mwezi Februari kwamba alilenga kumshtaki bwana Netanyahu kutokana na kesi tatu tofauti zinazojulikana kama kesi 1000, kesi 2000 na kesi 4000 kabla ya kesi hiyo kusikilizwa mwezi uliopita.

  • Kesi ya 1000: Netanyahu ameshtakiwa na ulaghai na kuwavunja imani raia. Anadaiwa kupokea zawadi ya thamani ya juu ikiwemo mvinyo na sigara, kwa lengo la kumsaidia tajiri mmoja rafikiye. Bwana Netanyahu anasema kwamba alipokea vitu hivyo kama zawadi ya kirafiki na kwamba hakumfanyia hisani yoyote rafiki huyo. Rafiki huyo pia amekana kufanya makosa yoyote.
  • Kesi 2,000: Bwana Netanyahu anakabiliwa na mashtaka ya ulaghai na uvunjaji wa imani. Anadaiwa kukubaliana na mchapishaji wa gazeti moja kuweka sheria za kudhoofisha gazeti pinzani kwa lengo la kuangaziwa mara kwa mara na gazeti hilo. Mchapishaji huyo ameshtakiwa na mashtaka ya kutoa hongo . Sawa na waziri huyo mchapishaji wa gazeti hilo amekana kufanya makosa yoyote. Wote wawili wamesema kuwa hawakuwa na lengo la kukuza maswala waliozungumzia katika mkutano wao na kwamba hakuna sheria kama hiyo iliopitishwa.
  • Kesi 4,000: Haya ndio madai makali kwa sababu Bwana Netanyahu ameshtakiwa na tuhuma za kutoa hongo pamoja na ulaghai na uvunjaji wa imani za wengi. Imedaiwa kwamba alipitisha maamuzi ambayo yalikuwa yakipendelea kampuni moja ya mawasiliano kwa lengo la kuangaziwa mara kwa mara na vyombo vya habari , ikiwa ni miongoni mwa makubaliano na mwanahisa mkuu wa kampuni hiyo. Waziri mkuu amesisitiza kwamba wataalam waliunga mkono uamuzi huo na kwamba hakulipwa chochote. Mwanahisa huyo ambaye pia naye amefunguliwa mashtaka ya hongo amekana madai hayo.

Ni nini kinachotarajiwa kufanyika

Haijulikani hatua hii ina maanisha nini kwa hatma ya bwana Netanyahu.

Hajapatikana na hatia yoyote kufikia sasa na kwamba hakuna sheria yoyote inayomzuia kusalia katika afisi kama waziri mkuu.

Inaweza kuchukua miezi mingi kabla ya kesi hiyo kuwasilishwa katika mahakama ya wilaya.

Na hata iwapo atapatikana na hatia , bwana Netanyahu hataruhusiwa kujiuzulu hadi pale kesi ya kukata rufaa uamuzi huo itakaposikilizwa na kukamilshwa swala ambalo linaweza kuchukua miaka kadhaa.

Hatahivyo , waandishi wanasema kwamba wengi wataulizia uwezo wa waziri huyo mkuu kusimamia maswala ya serikali iwapo anaendelea na kesi mahakamani.

Mashirika yasio ya serikali yanaweza kuwasilisha kesi katika mahakama ya kilele kushinikiza Bwana Netanyahu kujiuzulu.

Mahakama awali ilikuwa imeamuru kwamba waziri aliyeshtakiwa na tuhuma za uhalifu ni sharti kujiuzulu la sivyo aondolewa katika afisi na itaamua iwapo hatua kama hiyo pia inaweza kumuathiri waziri mkuu.

Washirika wa waziri mkuu bungeni wanaweza kupitisha sheria ambayo inaweza kumpatia kinga ya kushtakiwa akiwa afisini na kuruhusu wabunge kufutilia mbali uamuzi wa mahakama ya kilele iliomuondolea kinga hiyo.