Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
William Ruto: Rais 'mtoza ushuru' anayezua hasira za Wakenya
Na Basilioh Rukanga
BBC News, Nairobi
Rais wa Kenya William Ruto anaitwa kimzaha kama Zakayo - tafsiri ya Kiswahili ya mtu kwenye Biblia Zacchaeus, ambaye anainyeshwa katika kitabu kitakatifu cha Kikristo kama mtoza ushuru mwenye tamaa aliyepanda juu ya mti ili kumwona Yesu.
Hii ni kwa sababu Bw Ruto ameanzisha msururu wa tozo mpya na kuongeza za zamani, tangu achaguliwe kuwa rais mnamo Agosti 2022, na kumfanya kutopendwa na Wakenya wengi wanaoamini kuwa amesaliti ahadi yake ya kampeni ili kutetea masilahi ya "mahasl ama walalahoi " - wale wanaohangaika na umaskini kwa kukosa pesa.
Bw Ruto amekiri kwamba ushuru huo ni "mchungu" lakini, katika hotuba ya Siku ya kuadhimisha uhuru wa taifa hilo mnamo 12 Desemba, alisema mzigo unaobebwa na taifa "zitawafanya wapigania uhuru wetu wajivunie".
Kwake, ushuru wa juu ni muhimu ili kupunguza ukopaji wa serikali, na kupunguza deni la taifa, ambalo limepanda hadi shilingi trilioni 10 ($65bn; £51bn).
"Tumefanya maamuzi sahihi, wakati mwingine tunalazimika kufanya maamuzi magumu na machungu sana, ili kuirejesha Kenya kutoka kwenye makali ya janga kubwa la dhiki ya madeni," alisema.
Wala rais hana tatizo la kulinganishwa na Zakayo wa biblia .
“Kwa kuwa tayari nimeitwa Zakayo katika baadhi ya maeneo, labda tuwe na siku ya watoza ushuru,” alisema Mei.
Lakini Wakenya wengi hawakubaliani naye. Maumivu ya kodi yanatawala mazungumzo ya kila siku, hasa jinsi gharama ya maisha inavyopanda.
Pia wanasema ushuru unasaidia tu kufadhili ubadhirifu serikalini badala ya kuboresha huduma za umma.
Mtazamo huu umekua, hasa baada ya Mdhibiti wa Bajeti wa Kenya - afisi huru inayosimamia matumizi ya fedha za umma - hivi majuzi kuibua wasiwasi juu ya ushuru mkubwa huku kukiwa na matumizi "ya ubadhirifu", ikiwa ni pamoja na safari za ndani na kimataifa za maafisa wa serikali.
Rais Ruto, ambaye amefanya zaidi ya safari 40 nje ya nchi kwa takriban mwaka mmoja, ametetea safari zake akisema alikuwa akiwatafutia Wakenya uwekezaji wa kigeni na nafasi za kazi.
Katika kipindi hicho, kazi 70,000 za sekta ya kibinafsi zimepotea huku kukiwa na ongezeko kubwa la gharama za uendeshaji shughuli za kiviwanda au kibiashara na kufungwa kwa baadhi ya biashara, kulingana na ripoti ya hivi punde zaidi ya Shirikisho la Waajiri Kenya (FKE).
Inaonya juu ya hatari ya upotezaji zaidi wa kazi, ikisema kwamba 40% ya waajiri bado wanafikiria kupunguza shughuli zao.
FKE imetoa wito kwa serikali kuangalia upya ushuru, lakini wafanyabiashara wanalalamika kuwa serikali haisikilizi.
Mchumi Ken Gichinga anasema Kenya imekuwa ikikatisha tamaa biashara kwa kuweka mzigo mzito wa ushuru kwa makampuni ambayo yanastahili kubuni nafasi za kazi, kupata faida na kuimarisha fedha za serikali.
Mwishowe, baadhi ya makampuni yanahamia nchi nyingine, watu ambao walikuwa wanafikiria kufungua biashara ndogo kama migahawa wanaacha wazo hilo, huku biashara zilizopo zikilazimika kuingia katika sekta isiyo rasmi ili kuepuka kulipa kodi - jambo ambalo tayari limeanza kutokea.
Mike Muriuki, mkurugenzi wa kampuni ya a miaka 10 inayosambaza na kuuza mitungi ya gesi ya LPG, anaambia BBC kwamba nyongeza ya ushuru inazorotesha biashara yake.
Anasema watu wa kawaida hawana pesa za kununua gesi ya kupikia - hiyo imefanya biashara yake kudorora katika mwaka uliopita kutoka kwa oda za mitungi 700 kwa siku hadi takriban 200.
Bw Muriuki anasema hili limemlazimu kuachisha kazi zaidi ya asilimia 70 ya wafanyikazi wake, na kumuacha na takriban 20 pekee.
Kwa biashara nyingi ndogo na za kati kama yake, Bw Muriuki anasema, athari za ushuru zimekuwa nzito sana - na mienendo ya watoza ushuru imepakana na "kunyanyaswa" katika visa vingine.
Mwezi uliopita, kitengo cha Mamlaka ya Kukusanya Mapato Kenya (KRA) chenye mafunzo ya kijeshi kilitembelea moja ya majengo yake katika kaunti ya Kiambu, ambayo inapakana na mji mkuu, Nairobi.
Kitengo cha wakala wa ushuru kilitumwa mnamo Septemba kutekeleza uzingatiaji wa ushuru.
Akiwa katika majengo yake, Bw Muriuki anasema, maafisa hao wa ushuru waliuliza rekodi zake za mauzo na mapato, zikiwemo za miamala ya pesa kwa njia ya simu, pamoja na malipo yake ya ushuru. Pia walipiga picha za duka.
Ilikuwa hali "ya kutisha", anaiambia BBC.
"Jinsi walivyofanya [inaweza] kuweka hofu kubwa kwa wafanyabiashara… Watu wanafikiri watu hawa wanakuja kutukamata," Bw Muriuki anaongeza.
Anasema watu "sasa wanajaribu kutafuta njia za kuficha kile wanachokusanya", ikiwa ni pamoja na kutumia pesa taslimu na kuelekeza malipo ya pesa kwa simu kwa nambari za kibinafsi badala ya biashara zao kwenye akaunti za benki .
Mmiliki wa duka la vipuri vya magari katikati mwa jiji la Nairobi anasema alikuwa ameacha kutumia nambari ya malipo ya biashara yake hadi kiasi cha tozo ya malipo na gharama nyingine zipungue .
Mabadiliko ya taratibu katika mfumo wa malipo yamekuwa mada ya mjadala wa hivi majuzi kwenye mitandao ya kijamii nchini Kenya, ingawa data kutoka kwa kampuni kubwa zaidi ya mawasiliano ya Safaricom bado inaonyesha kuongezeka kwa miamala ya pesa kwa simu hadi Septemba.
Tangu Julai, kumekuwa na ongezeko la ushuru kwa mishahara ya kila mwezi kutoka kiwango cha juu cha 30% hadi 35%, ushuru mpya wa nyumba wa 1.5%, ushuru wa 2.75% wa mfuko wa bima ya hospitali, ushuru wa mauzo wa 3% (mauzo ya jumla) kwa biashara ndogo na kuongezeka maradufu kwa ushuru wa mafuta hadi 16% - miongoni mwa aina nyingine nyingine za ushuru .
Baadhi ya kodi, huku kukiwa na kupanda kwa gharama ya maisha, ilisababisha maandamano mabaya mitaani mapema mwaka huu.
Pia kumekuwa na ongezeko kubwa la gharama za kupata vitambulisho, hati za kusafiria, hati za kuzaliwa, ndoa na kifo.
Mmiliki wa kampuni ya watalii iliyoanzishwa mwaka wa 2017 ambayo inajishughulisha zaidi na safari za nje anaiambia BBC kwamba amekerwa na mazingira yasiyo rafiki ya biashara ambayo sasa anajikuta.
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwa vile anahofia kuadhibiwa, anasema ushuru mkubwa umepunguza uwezo wa watu kutumia katika mambo kama vile usafiri, akiongeza kuwa kila mtu katika sekta ya utalii anahisi joto, lakini kwa njia tofauti.
Kwake yeye, kushuka kwa kasi kwa thamani ya shilingi ya Kenya, hata dhidi ya sarafu katika soko la Afrika Mashariki, kumemfanya kushindwa kupanga mapema shughuli zake .
Analalamika kwamba Huduma ya Wanyamapori ya Kenya imeongeza zaidi ya mara nne ada za kuingia kwenye mbuga, lakini "hakuna thamani [ya ziada] inayotolewa".
"Watalii wananiuliza: 'Ni nini kinatokea katika nchi yako?'," anaiambia BBC, akiongeza kuwa Kenya inaharibu soko lake la utalii kwani watu wanaweza kupata dili bora katika nchi jirani za Tanzania na Rwanda.
Katika miezi michache iliyopita, hajapanga ziara zozote za ndani - na amehamia katika sekta nyingine, ikiwa ni pamoja na kilimo, ili kuishi.
KRA, katika ripoti ya Disemba 11, inasema imedumisha ukuaji wa mapato ya juu tangu Julai, lakini ilikuwa chini ya lengo lake la kila mwaka, kwani kuongezeka kwa bei ya mafuta kumepunguza mahitaji ya bidhaa kutoka nje.
Ilikubali kuwa mahitaji ya bidhaa na huduma za ndani yamepungua, huku pia ikitaja ongezeko la viwango vya mikopo na kupungua kwa faida ya benki.
Wiki moja iliyopita, waziri wa Fedha aliwaambia wabunge nchi inapata shida kupata pesa za kulipa mishahara ya watumishi wa umma na pia kutoa pesa za wabunge kwa miradi yao ya maeneo bunge, ambayo inamaanisha kutakuwa na maendeleo kidogo.
Kwa taswira hiyo ya kuhuzunisha, Wakenya wengi wanatumai kuwa Bw Ruto atawapa nafuu na kulegeza msimamo wake, kama vile hatimaye Zakayo alivyofanya aliposhuka chini ya mti baada ya Yesu kumwita.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah na kuhaririwa na Ambia Hirsi