Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Christian Atsu wa Ghana alikuwa na 'moyo wa kipekee'
Mwana wa mvuvi, Christian Atsu hakuwahi kunaswa na mitego ya umaarufu.
Mwanzo wake duni ulimaanisha kuwa kiungo huyo wa Ghana, ambaye alikufa katika tetemeko la ardhi la hivi karibuni lililoharibu Uturuki na Syria, hakupoteza kamwe tamaa ya kutumia mafanikio yake kusaidia wengine katika maisha yao.
Ukarimu wake na asili yake ya hisani inamaanisha mchezaji-mwenza wa zamani wa kimataifa amemtaja Atsu kama "mmoja kati ya milioni".
"Alisaidia watu wengi kutatua matatizo yao, alitoa pesa taslimu kwa waliohitaji," John Paintsil aliiambia BBC Sport Africa.
"Alikuwa mwerevu sana hali ya kwamba alikua na mawazo tofauti chungu nzima.
"Alikuwa mcheshi na mbunifu, kama nyota wa filamu," mlinzi huyo wa zamani wa Fulham na West Ham aliongeza.
"Tumepoteza mtu mwenye roho nzuri. Alikuwa mmoja kati ya milioni kwa sababu wakati mwingine aliwatanguliza wengine mbele yake."
'Messi wa Ghana'
Pengine kivutio cha maisha ya kimataifa cha Atsu kilifika kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2015 huko Equatorial Guinea ambapo alifunga mabao mawili kuelekea fainali ambapo walishindwa na Ivory Coast kwa mikwaju ya penalti.
Hata hivyo, kiungo huyo anayetumia mguu wa kushoto alinyakua tuzo mbili pekee za bao bora na mchezaji bora wa michuano hiyo.
"Ilikuwa furaha kuwa pamoja naye - mtu ambaye alikuwa na ustadi mwingi na ubora," alisema Kwesi Appiah, ambaye alicheza pamoja na Atsu kwenye Afcon hiyo ya 2015.
"Alipewa jina la utani Messi wa Ghana kwa mtindo wake na pia jinsi tulivyomtegemea kama timu," alifichua mshambuliaji huyo wa zamani wa Crystal Palace.
"Alikuwa mchezaji wa kipekee na nina heshima kubwa kushiriki naye nyakati maalum uwanjani."
Kwa jumla, Atsu aliiwakilisha nchi yake mara 62, akifunga mabao 10.
"Mbali na soka, alikuwa mwenye kujali sana na kusaidia na angefanya kila njia kusaidia mtu yeyote," Appiah aliendelea.
"Angefurahisha mahala popote."
Kutoka kwa uvuvi nchini Ghana hadi kupata nyavu huko Uropa
Kutoka kwa uvuvi nchini Ghana hadi kupata nyavu huko Uropa
Atsu alizaliwa Januari 1992 huko Ada Foah, mji ulioko kusini-mashariki mwa pwani ya Ghana ambapo Mto Volta unaungana na Bahari ya Atlantiki kuunda delta ambayo ilimruhusu marehemu baba yake kupata maisha ya uvuvi na kilimo.
Alipokuwa akikua, alilala chumba kidogo na mama yake, dada yake mapacha Christiana na ndugu wengine wanne.
Kama watoto wengine wa Kiafrika, mpira wa miguu ulikuwa tikiti ya ndoto kutoka umaskini.
Atsu alianza mchezo wa kulipwa Katika klabu za Cheetah FC na Feyenoord Fetteh - akademi ya Uholanzi - kabla ya kuhamia kwa wababe wa Ureno FC Porto mnamo 2009.
Atsu alikuwa na umri wa miaka 17 tu alipowasili Ureno, mwanzoni akihangaika kuingia kwenye kikosi cha kwanza.
Lakini kipindi cha mkopo huko Rio Ave kilimfanya afanikiwe katika klabu yake kuu wakati wa kampeni za 2012/13.
Akicheza mechi 25 katika mashindano yote ya klabu ya Porto, pamoja na kucheza kila mechi huku Ghana ikimaliza nafasi ya nne kwenye Afcon nchini Afrika Kusini, aliwashawishi Chelsea kumnasa Septemba 2013.
Lakini baada ya kuhamia London, kwa ada iliyoripotiwa kuwa ya pauni milioni 3.5, hakufanikiwa kama ilivyopangwa kwa sababu Atsu hakuwahi kuchezea kikosi cha kwanza cha Chelsea .
Badala yake, alikua sehemu ya jeshi la mkopo la Chelsea, na kusababisha kukaa kwa muda huko Uholanzi, England na Uhispania akizichezea oVitesse Arnhem, Everton, Bournemouth na Malaga.
Lakini hilo halikuathir uchezaji wa Atsu kwenye jukwaa la kimataifa; ni wakati huu ambapo aling’ara vilivyo kwa Black Stars kwenye Afcon 2015.
Wakati wa mkopo mwingine, Atsu aliisaidia Newcastle United kushinda kupanda tena Ligi ya Premia, akifunga katika mchezo huo ambapo timu hiyo ilifanikiwa kurejea mara moja kwenye ligi kuu ya Uingereza.
Hatua hiyo ilifanywa kuwa ya kudumu hivi karibuni.
"Alikuwa mtu ambaye alikuwa mpole sana, aliyezungumza kwa upole," alisema mtangazaji wa BBC Radio Newcastle Matthew Raisbeck, ambaye anamkumbuka Atsu kutokana na kampeni hiyo iliyofanikiwa ya Newcastle kupandishwa kurudi katika ligi ya Premia.
"(Yeye) mara nyingi alichaguliwa na Rafa Benitez na Steve Bruce [wote wa zamani wa Newcastle] kwa bidii yake katika mazoezi na kiwango cha juu cha utimamu wa mwili."
Baada ya miaka mitano huko St James' Park, Atsu alipata majeraha huko Saudi Arabia akiwa na Al-Raed kabla ya kujiunga na Hatayspor ya Uturuki ya Super Lig mnamo Septemba.
Katika hali ya kushangaza, alifunga bao la ushindi katika dakika ya 97 ya mechi ya Hatayspor dhidi ya Kasimpasa saa chache kabla ya tetemeko la ardhi la kwanza kutokea na kupoteza maisha yake.
Alikuwa na umri wa miaka 31.
'Mtu wa kipekee na wa ajabu'
Lakini pengine mafanikio makubwa zaidi ya Atsu yalikuja nje ya uwanja, ambapo aliishi maisha ambayo yalikuwa kinyume kabisa na dhana ya umaarufu inayohusishwa na wanasoka wa kisasa.
Alirejea Cheetah FC, ambako alijifunza kazi yake kwa mara ya kwanza, akichangia buti na vitu vingine kwa akademi ya timu ya daraja la pili ya Ghana.
Alilenga pia kuwarekebisha wahalifu, watu ambao walikuwa na hamu ya chakula na kuishia kuhukumiwa kwa uhalifu mdogo.
Atsu aliamini kuwa jela haipaswi kuharibu watu na alikuwa na jukumu la kuunganisha familia kadhaa maskini nchini Ghana baada ya kulipa maelfu ya dola za faini na pesa za dhamana.
Katika mfano mmoja, anasaidia kuwachiliwa kwa bibi mwenye umri wa miaka 62 na binti yake, waliofungwa jela kwa kuiba mahindi yenye thamani ya dola mbili ili kulisha familia yao.
Pia aliwapa baadhi ya wafungwa pesa ili waanze biashara na pia akaboresha uwanja wa soka katika Gereza la Awutu.
Lakini uhisani wa Atsu haukuwa tu kuwasaidia wale walio katika matatizo na sheria.
"Alikuwa mtoaji sana, binadamu wa hali ya juu sana," Ellie Milner, mwenyekiti wa Arms Around the Child, aliambia BBC alipoulizwa kuhusu kazi ya kiungo huyo na watoto walio katika mazingira magumu.
"Alipowatembelea watoto, alikuwa akifika na kuvua viatu vyake na kucheza bila viatu.
"Wangemkaribisha kama shujaa, lakini pia kama baba, mjomba au kaka.
Atsu alikuwa balozi wa shirika hilo la hisani tangu 2016 na alikuwa "mfadhili mkuu" wa shule ya Ghana inayosaidia watoto waliotelekezwa, mayatima, wagonjwa sugu na wale waliookolewa kutokana na biashara haramu ya binadamu.
"Alikuwa mtu wa kipekee na wa ajabu," aliongeza Milner.
"Mmoja wa watu wema, wenye talanta zaidi, wanyenyekevu kuingia katika ulimwengu huu."
"Urithi wake utaendelea kupitia mamia, ikiwa sio maelfu ya maisha ambayo amesaidia."