Kwanini Chadema inaingia barabarani?

Bh

Chanzo cha picha, EAGAN SALLA/BBC

Maelezo ya picha, Viongozi wakuu wa Chadema Freeman Mbowe (kushoto) na Tundu Lissu

Chama Kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema kinaingia barabarani asubuhi ya leo katika maandamano yatakayoanzia Mbezi Mwisho na Buguruni Sheli, jijini Dar es Salaam na kuishia katika ofisi za Umoja wa Mataifa.

Katika kuonyesha kuridhia maandamano hayo, taarifa ya Jeshi la Polisi, siku ya jana, limeitaka Chadema kuhakikisha inazuia lugha za uchochezi na kejeli zinazoweza kusababisha uvunjifu wa sheria. Pia, limeagiza kufuatwa kwa taratibu katika maeneo yote ambayo chama hicho kimetoa taarifa za kufanya maandamano.

Sababu za Kuandamana

Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Januari 13, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema maandamano yanalenga kuishinikiza Serikali kuzingatia maoni na mapendekezo ya wadau mbalimbali kuhusu masuala ya uchaguzi.

Vilevile chama hicho kinaitaka serikali iondoe Bungeni miswaada inayohusu vyama vya siasa na uchaguzi, ambayo ni muswada wa Marekebisho ya Sheria za Vyama vya siasa na Sheria ya gharama za Uchaguzi.

Badala yake Serikali iwasilishe muswada wa kukwamua mchakato wa Katiba mpya kwa kuzingatia mwafaka wa kitaifa. Kwani Chadema inaamini, "serikali imepuuza maoni yaliyotolewa na Kikosi Kazi pamoja na wadau mbalimbali."

Kadhalika, Chadema imeitaka Serikali iwasilishe bungeni muswada wa kufanya marekebisho ya mpito ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ili uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2024 na ule mkuu wa 2025 uwe huru na haki.

Suala la gharama za maisha pia limekuwa ajenda ya maandamano: "Tunataka serikali ipeleke mpango wa kuwakwamua wananchi na hali ngumu ya maisha Bungeni, ikiwa ni pamoja na kushusha bei ya bidhaa muhimu au kuweka ruzuku katika baadhi ya bidhaa," amesema Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Itakumbukwa kuwa katazo la kufanya maandamano lililotolewa na hayati Rais John Pombe Magufuli, lilidumu kwa miaka saba na kulikuwa na msururu wa matangazo na majaribio ya maandamano yaliyoshindwa au kuvunjwa na Jeshi la Polisi.

Mwanzoni mwa mwezi Januari 2023, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alitoa tangazo rasmi la kuruhusu mikutano ya hadhara ya kisiasa na maandamano, baada ya mwaka mmoja na miezi kumi tangu alipoingia madarakani Machi 2021.