Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wanaume wa Somalia wanaovalia vikoi wanavyopambana na wanamgambo wa al-Shabab
Baadhi ya wapiganaji wasiotarajiwa wanaimarisha silaha za serikali ya Somalia katika vita vyake vya muda mrefu dhidi ya al-Shabab, mojawapo ya washirika waliofanikiwa zaidi wa al-Qaeda - na kundi ambalo lilikuwa nyuma ya mlipuko wa bomu lililotegwa kwenye gari katika mji mkuu, Mogadishu, mwishoni mwa wiki iliyopita na kuua takriban watu 120.
Picha za wanaume waliovaa vikoi na makubazi wakikimbia huku na kule wakiwa na bunduki ni mojawapo ya dhana potofu za kudumu katika migogoro nchini Somalia.
Picha za wapiganaji hawa waliotapakaa kila mahali katika mji wenye ghasia wakifyatua risasi wakiwa wanaenda, inaonyeshwa tena na tena, kiasi cha kuwaudhi Wasomali ambao wanasema huu si uwakilishi wa kweli au sahihi wa jamii yao.
Wasomali huuita vikoi "ma'awiis".
Kwa kawaida huja katika rangi mbalimbali, zilizopambwa kwa miundo ambayo asili yake ni Indonesia.
Wanaume wengi huvitumia kama vazi la kila siku, huku wakizivaa wakati wa kupumzika jioni au kuwa huru zaidi na kufurahia huku wakitafuna mirungi.
Sasa wanaume waliovaa vikoi wamekuwa silaha mpya yenye nguvu katika vita vya kukomesha uasi wa miaka 15 kwenye nchini hiyo ya Kiislam.
Makundi haya ya wapiganaji wa koo yamechipuka kwa kiasi kubwa kutoka kwa jamii za kuhamahama na wakulima wanaoishi chini ya al-Shabab, ambazi zinadhibiti maeneo makubwa ya kusini na katikati mwa Somalia na kuweka sheria kali kwa wale wanaoishi huko.
Ingawa wanamgambo hao wa Kiislamu wana mtandao wenye nguvu wa majasusi ambao hufuatilia kila nyanja ya maisha ya watu na kuwaadhibu vikali wale wanaokaidi, vuguvugu la chinichini limeinuka dhidi yao.
Wakati ukame mbaya zaidi katika miaka 40 unavyoendelea na njaa inazidi kuongezeka, watu hawawezi tena kumudu kulipa kodi kwa al-Shabab.
Huku zaidi ya mifugo milioni tatu wakiangamia kwa kukosa chakula na maji, hawawezi tena kuwakabidhi wanyama wanaodaiwa na wanamgambo hao.
Hawawezi tena kuvumilia kuwakabidhi wana wao wa kiume na wa kike kutumika kama wanamgambo na watumwa wa ngono.
Tulichopitia imetosha.
Vikundi vidogo vya wahamaji na wakulima mara kwa mara wamekuwa wakipinga al-Shabab katika miaka ya hivi karibuni, na kukandamizwa bila huruma.
Wakati huu wanaume waliovaa vikoi ni wengi na sasa wana utaratibu zaidi, na wanapewa risasi, chakula na mafuta na serikali.
Wachambuzi wa masuala ya usalama wanasema baadhi yao ni kutoka vikosi vya Jeshi la Kitaifa la Somalia.
‘’Waasi sasa wanakabiliwa na uasi wao wenyewe,’’ anasema Mohamed Mubarak, mwenyekiti wa taasisi ya usalama ya Hiraal yenye makao yake mjini Mogadishu.
Ikiwa haya yataenea nchi nzima, sidhani kama al-Shabab wataendelea kuwepo.
'Hatuna hofu'
Mwitikio wa wapiganaji wa jihadi unaonyesha jinsi wanavyowachukulia kwa uzito.
Wameanzisha msururu wa kuchoma nyumba, kuharibu visima na kuua wafanyabiashara na wazee wa koo moja na wapiganaji wanaovaa vikoi.
Katika hotuba ya hivi majuzi kwa wahitimu wa kambi za mafunzo za al-Shabab, msemaji wake Sheikh Ali Dheere aliwataja wanaume wanaovaa vikoi kama "majambazi na wabakaji waliokuwa wakizurura nchini kabla ya al-Shabab kuingia madarakani".
Lakini Musa Idris Hassan, mwanachama wa wanamgambo wa wanaovaa vikoi katika eneo la kati la Somalia la Hiran, anapinga hili.
"Sisi ni wahamaji. Siku zote tumekuwa wapiganaji. Tumeishi chini ya wanamgambo kwa miaka mingi hivyo tunajua kila kitu kuhusu wao ikiwa ni pamoja na mahali wanapojificha.
"Tutaingia katika kila kichaka kuwatafuta na kuwachinja wote. Hatuna hofu ya al-Shabab au mtu mwingine yeyote."
Wanaoaa vikoi pia nao hawafanyi haya wakiwa peke yao.
Wanaunda sehemu muhimu ya mkakati mpya wa serikali wa kupambana na al-Shabab, ambayo ni pamoja na jeshi la anga la Marekani, wanajeshi wa Umoja wa Afrika (AU), wanajeshi wasomi wa Somalia waliopewa mafunzo ya kigeni, jeshi la taifa na wanajeshi kutoka majimbo matano ya shirikisho la nchi hiyo.
"Sijawahi kuona jumuiya ya kimataifa ikifurahia vita dhidi ya al-Shabab," anasema mbunifu wa mbinu hii mpya, Mshauri wa Usalama wa Taifa Hussein Sheikh-Ali.
Wanaume wanaovaa vikoi ni nyongeza muhimu katika uwanja wa vita. Wanatoa uhalali wa vita vyetu dhidi ya wanamgambo kwa sababu wanatoka katika jamii wanazozitawala.
"Wanachukua jukumu muhimu la msaada kwa kutoa ujasusi ambao unawezesha vikosi vyetu maalum kuwapata na kuwapiga waasi. Sasa tunaelekea kuwashinda al-Shabab kabisa."
Amina Musa aliishi kwa miaka 13 chini ya udhibiti wa al-Shabab katika mji wa kati wa Booco, ambao ulichukuliwa tena na serikali mnamo mwezi Septemba.
"Wanaume wanaovaa vikoi ni bora kuliko jeshi," anasema. "Wanapigana kutoka mioyoni mwao sio matumbo yao."
Wamehamasishwa zaidi kwa sababu maisha yao yameathiriwa moja kwa moja na wanamgambo hao wa Kiislam, ambao wameiba watoto wao, wanyama wao na kila kitu kizuri kuhusu maisha yao ya kuhamahama. Hasira zao ni za kweli."
Kuongezwa kwa wanamgambo wa koo kwa kile Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud amekielezea kama "vita kamili" dhidi ya al-Shabab kumefanya mabadiliko makubwa.
Wataalamu wa usalama wanasema Somalia imepata maeneo mengi kati ya Juni na Septemba kuliko ilivyopata katika miaka mitano iliyopita.
Hatari za vita vya ukoo
Lakini kuwapiga al-Shabab haitoshi.
Changamoto ni kushikilia eneo.
Wanamgambo hao wana historia ndefu ya kujiondoa kimbinu kisha kurejea moja kwa moja mara tu jeshi na wanajeshi wa AU wanaposonga mbele.
Iwapo serikali inataka kufanikiwa katika "vita vyake vyote", itahitaji kubadilisha miundo ya utawala na huduma za kijamii zinazofikia mbali za al-Shabab, ikiwa ni pamoja na vikosi vya polisi, mahakama, mifumo ya ushuru, shule na vituo vya afya.
Kulingana na Bw Mubarak, mamlaka pia itahitaji kufikiria nini cha kufanya na wanaume wanaovaa vikoi, ambao wameonya kuwa wanaweza kuwa kikombe chenye sumu.
"Mkakati huu utafanya kazi tu ikiwa wanaume hao wapiganaji watanyanganywa silaha au kuwekwa katika vikosi vya usalama vya kawaida baada ya maeneo kurejeshwa na masuala yao ya ndani kutatuliwa kabla ya kuanzisha shughuli za ukombozi, hasa katika maeneo yenye migogoro iliyopo," mtaalamu wa usalama wa Hiraal anasema.
"Vinginevyo, Somalia ina hatari ya kukabiliwa na hatari mpya ya kuwa na wanamgambo wa koo waliojihami na kushambuliana. Hii inaweza kuturudisha kwenye vita vya koo za miaka ya 1990."
Mafanikio ya hivi majuzi dhidi ya al-Shabab yanapendekeza ushirikiano wa sasa wa vikosi vya kimataifa, kikanda, rasmi na visivyo rasmi vya Somalia ambavyo vinafanya kazi kwenye safu ya kijeshi.
Makumi ya miji na vijiji vimetekwa katika wiki za hivi karibuni.
Ikijumlishwa na juhudi za serikali za kuvuruga mtiririko wa fedha kwa wanamgambo na kupinga itikadi zao, hii inaweza kuwa jibu la kudhoofisha harakati hiyo kwa kiasi kikubwa, ikiwa sio kuishinda kabisa.