'Tuueni, lakini msiturudishe Myanmar'

Katika miaka yake minne dhaifu, Yasmin ameishi maisha ya kutokuwa na uhakika, bila uhakika anakotoka.

Alizaliwa katika kambi ya wakimbizi nchini Bangladesh, hawezi kurejea katika kijiji cha mababu zake huko Myanmar.

Kwa sasa, anaishi katika chumba kibovu katika mji mkuu wa India, Delhi, ambacho anakitumika kama nyumbani.

Sawa na maelfu ya watu wa jamii ya Rohingya- walio wachache nchini Myanmar - wazazi wa Yasmin walitoroka nchi mwaka 2017 kukwepuka oparesheni ya kikatili iliyozinduliwa na majeshi dhidi yao.

Wengi wao walikimbilia nchi jirani kama Bangladesh na India, ambako wanaishi kama wakimbizi.

Miaka mitano baadaye, Waislamu wa Rohingya - idadi kubwa zaidi ya watu wasio na utaifa duniani, kulingana na Umoja wa Mataifa - wanabaki katika utata.

Baba yake Yasmin, Rehman, alikuwa mfanyabiashara nchini Myanmar. Wakati wanajeshi walipowavamia watu vibaya, alikuwa mmmoja wa Warohingya 700,000 waliotoroka kwa wingi.

Baada ya kutembea kwa siku kadhaa, Rehman na mke wake Mahmuda walifanikiwa kufika katika kambi ya wakimbizi ya Cox Bazar, eneo la kusini mashariki mwa Bangladesh karibu na mpaka wake na Myanmar.

Wanandoa hao waliishi katika hali ngumu. uhaba wa chakula ulikuwa jambo la kawaida na walilazimika kutegemea chakula cha mgao kutoka kwa mashirika ya kutoa msaada.

Mwaka mmoja baada ya wao kufika Bangladesh, Yasmin alizaliwa. Serikali ya Bangladesh imekuwa ikishinikiza Waislamu wa Rohingya kurejea Myanmar.

Maelfu wa ya wkimbizi wamehamishiwa katika kisiwa cha vijijini kinachoitwa Bhasan Char, ambacho wakimbizi wanakiita "island prison".

Rahman alihisi kwamba kuondoka Bangladesh kungewasaidia watoto wao kuwa na maisha mazuri ya siku za usoni.

Kwa hivyo mwaka 2020, wakati Yasmin akiwa na miaka michache, familia ilivuka mpaka na kuingia nchi jirani ya India.

Makadirio yanatofautiana, lakini mashirika ya wakimbizi yanaamini kuna kati ya wakimbizi 10,000 na 40,000 wa Rohingya nchini India. Wengi wamekuwa nchini tangu 2012.

Kwa miaka mingi, Warohingya hapa wameishi maisha ya kawaida na kuvutia mabishano kidogo.

Lakini baada ya waziri wa shirikisho kutweet mwezi huu kwamba wakimbizi watapewa makazi, huduma na ulinzi wa polisi, uwepo wao mjini Delhi megongwa upya vichwa vya habari.

Saa kadhaa baadaye serikali ya chama tawala cha Bharatiya Janata Party (BJP) nchini India ilikana kuwa ilikanusha kuwa imetoa makazi kwa Waislamu wa Rohingya, badala yake ikawaelezea kama "waageni haramu" ambao wanapaswa kufukuzwa au kupelekwa katika vituo vya kuzuilia watu.

Mabadiliko haya ya ghafla yameziacha familia kama vile Rehman katika njia panda na hali ya kukata tamaa.

"Mustakabali wa mtoto wangu unaonekana kuwa mbaya," alisema, akiwa ameketi kwenye kitanda cha mbao kisicho na godoro.

"Serikali ya India pia haitutaki... lakini ni afadhali watuue kuliko kutufukuza na kuturudisha Myanmar."

Hakuna taifa lililo tayari kuchukua maelfu ya Warohingya. Wiki iliyopita Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina alimwambia Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Michele Bachelet, kwamba wakimbizi nchini mwake lazima warejee Myanmar.

Lakini Umoja wa Mataifa unasema si salama kwao kufanya hivyo kwa sababu ya mzozo wa Myanmar. Mnamo Februari 2021, jeshi la Myanmar - ambao wanatuhumiwa kwa uhalifu dhidi ya Warohingya - walichukua udhibiti wa nchi katika mapinduzi ya kijeshi.

Mamia ya Warohingya wamefanya safari za hatari kwa njia ya bahari hadi nchi kama vile Malaysia na Ufilipino ili kuepuka ukatili unaofanywa na serikali ya kijeshi.

Idadi ya wakimbizi katika kambi nchini Bangladesh imeongezeka na kufikia karibu milioni moja. Nusu yao ni watoto.

Kama Rehman, Kotiza Begum pia alitoroka Myanmar mnamo Agosti 2017, akitembea kwa siku tatu bila chakula chochote.

Yeye na watoto wake watatu wanaishi katika chumba kimoja katika kambi huko Cox's Bazar.

Wanatumia karatasi ya plastiki kama paa, ambayo hutoa ulinzi duni dhidi ya mvua wakati wa vuli.

Mambo ya kutisha aliyoyaacha nyuma nchi mwake bado yamezonga mawazo yake. "Wanajeshi waliingia katika nyumba yetu na kututesa. Walipofyatua risasi, tulikimbia. Watoto walitupwa mtoni. Waliua mtu yeyote waliyepatana naye njiani."

Kama ilivyo kwa wengine katika kambi, Kotiza anategemea mgao wa chakula kutoka kwa mashirika ya kutoa misaada, ambayo mara nyingi yanazingatia mambo ya msingi kama vile dengu na mchele.

"Siwezi kuwaatia wanagu chakula wanachotaka, siwezi kuwapa nguo nzuri, siwezi kuwapatia matibabu yanayostahili," anasema.

Kotiza anasema wakati mwingine analazimika kuuza mgawo wake wa chakula ili kuwanunulia watoto wake kalamu za kuandikia.

Kulingana na tathmini ya hivi majuzi ya Umoja wa Mataifa, kupunguzwa kwa ufadhili wa kimataifa kumeongeza changamoto kwa idadi ya watu ambayo bado "wanategemea kikamilifu msaada wa kibinadamu kuishi".

Umoja wa Mataifa ulisema wakimbizi wanaendelea kutatizika kupata chakula chenye lishe bora, makazi ya kutosha na usafi wa mazingira, na fursa za kufanya kazi.

Na elimu - mojawapo ya vipaumbele vikubwa vya Kotiza kwa watoto wake - pia ni changamoto kubwa.

Kuna wasiwasi wa kizazi kilichopotea, ambacho hakipati elimu bora. "Watoto huenda shuleni kila siku, lakini hakuna maendeleo kwao. Sidhani wanapata elimu nzuri," Kotiza anasema.