Barabara iliyojengwa na Israel huko Gaza yazusha maswali

Chanzo cha picha, עכשיו 14
- Author, Abdirahim Saeed, Tom Spencer, Paul Brown & Richard Irvine-Brown
- Nafasi, BBC Arabic & BBC Verify
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limemaliza kujenga barabara mpya inayopita kaskazini mwa Gaza kutoka mashariki hadi magharibi, kulingana na picha za satelaiti zilizothibitishwa na BBC.
Israel inasema inajenga barabara ya usambazaji vifaa. Lakini wataalamu wana wasiwasi kuwa inaweza kuwa ni barabara ya kudumu.
Wanahofia itatumika kama kizuizi, kuwazuia Wapalestina kurejea makwao kaskazini mwa nchi hiyo.
Njia hiyo mpya inaanzia kwenye uzio wa mpaka wa Gaza na Israel karibu na Nahal Oz kibbutz. Inapita Gaza na kuishia karibu na pwani ya magharibi.
Brigedia Jenerali Mstaafu Jacob Nagel, mshauri wa zamani wa usalama wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, aliiambia BBC Arabic lengo la njia hiyo mpya ni kwa ajili ya kutoa urahisi kwa vikosi vya usalama wakati wa kukabiliana na mapigano mapya.
Lakini baadhi ya wachambuzi walielezea wasiwasi wao kuwa barabara hiyo inaonekana kuwa sehemu ya mpango wa Israel kubaki Gaza baada ya kumalizika kwa vita.
Hakuna mtandao wa barabara zinazounganisha mashariki na magharibi, njia mpya ya IDF ndiyo pekee yenye uwezo huo.
Pia inaingiliana na barabara ya Salah al-Din na al-Rashid, barabara mbili kuu katika eneo hilo.
Mwezi Februari, Waziri Mkuu Netanyahu alisema Israel itadhibiti usalama wa Gaza baada ya vita kwa muda usiojulikana.
Viongozi wa kimataifa hapo awali wameionya Israel dhidi ya kuwafukuza Wapalestina au kupunguza ukubwa wa Gaza.
Barabara hiyo mpya huenda ikaanzisha upya mjadala kuhusu mkakati wa Israel baada ya vita.
Katika kujibu maswali kuhusu barabara hiyo mpya, IDF iliiambia BBC, ipo ili kuwezesha utendaji wa haraka wa askari na vifaa.
Zaidi kuhusu barabara hii

Uchambuzi wa picha za satelaiti na BBC unaonyesha ni barabara mpya ya zaidi ya kilomita 5 ili kuunganisha barabara ambazo hazikuwa zimeunganishwa hapo awali.
Sehemu ya awali ya barabara mashariki mwa Gaza karibu na mpaka wa Israel ilijengwa mwishoni mwa Oktoba iliyopita na mapema Novemba.
Lakini sehemu nyingine za barabara hiyo zilijengwa wakati wa Februari na mapema Machi.
Barabara hii ni pana kuliko barabara za kawaida za Gaza, bila kuijumuisha Salah al-Din.

Uchambuzi pia unaonyesha majengo kando ya barabara, yalibomolewa kuanzia mwishoni mwa Disemba hadi mwishoni mwa Januari.
Barabara hiyo imepita katika eneo ambalo hapo awali lilikuwa na majengo machache na lilikuwa na watu wachache, ikilinganishwa na maeneo mengine ya Gaza.
Kituo cha televisheni cha Israel kiliripoti kuhusu njia hiyo mwezi Februari, kikisema inaitwa "Barabara kuu ya 749." Mwandishi wa habari kutoka Channel 14 alisafiri na jeshi la Israel katika barabara hiyo.
Katika video hiyo, magari ya ujenzi wa barabara na wachimbaji walionekana wakijiandaa kwa ujenzi.

Chanzo cha picha, עכשיו 14
Inaweza kutumikaje?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wachambuzi wa kampuni ya intelejinsia ya ulinzi ya Janes, walisema aina ya barabara isiyo na lami inayoonekana kwenye picha ya Channel 14, inafaa kwa magari yenye silaha.
Mkuu wa zamani wa Baraza la Usalama la Taifa la Israel, Jenerali Jacob Nagel, alisisitiza barabara ni kwa ajili ya masuala ya usalama.
"Itasaidia Israel kuingia na kutoka, kwa sababu Israel itakuwa na jukumu kamili la ulinzi na usalama wa Gaza," aliiambia BBC Arabic.
"Hatutaki kusubiri hadi tishio litokee," aliongeza.
Meja Jenerali Yaakov Amidror, aliyehudumu katika IDF, ana maoni sawa na hayo.
Madhumuni ya msingi ya barabara hiyo mpya ni "udhibiti wa kijeshi na mipango katika ukanda wa Gaza," alisema.
Justin Crump, afisa wa zamani wa Jeshi la Uingereza ambaye anaendesha kampuni ya kutathmini shughuli za kijasusi, Sibylline anasema, njia hiyo mpya ni muhimu.
"Kwa hakika inaonekana kama ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu kuwa na angalau aina fulani ya uingiliaji kati wa usalama na udhibiti katika Ukanda wa Gaza," alisema Crump.
Khaled Elgindy, mfanyakazi mwandamizi katika Taasisi ya Mashariki ya Kati yenye makao yake Marekani, pia anadhani barabara hiyo ni mradi wa muda mrefu.
"Inaonekana kuwa wanajeshi wa Israel watasalia Gaza kwa muda usiojulikana," Elgindy aliambia BBC.
"Kwa kuigawanya Gaza nusu, Israel itadhibiti sio tu yale yanayoingia na kutoka Gaza, lakini pia harakati ndani ya Gaza," mchambuzi huyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mpango wa Masuala ya Palestina na Palestina-Israel katika taasisi hiyo.
"Hii ni pamoja na uwezekano wa kuwazuia Wapalestina milioni 1.5 waliokimbia makazi yao kusini kurejea makwao kaskazini."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi












