Wajumbe wa Hamas waondoka Cairo kwenye mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza bila makubaliano

Lakini kundi hilo lenye silaha linasema mazungumzo ya moja kwa moja na Israel juu ya usitishaji vita kwa wiki sita hayajaisha.

Moja kwa moja

Dinah Gahamanyi, Lizzy Masinga, Asha Juma and Ambia Hirsi

  1. Na kufikia hapo ndio tunakamilisha matangazo yetu kwa leo. Kwaheri

  2. Fisi amshtua Mkenya baada ya kuingia kisiri katika duka lake eneo la Nakuru

    .

    Chanzo cha picha, CITIZEN DIGITAL

    Mfanyabiashara mmoja katika jiji la Bonde la Ufa la Nakuru nchini Kenya "amepatwa na mshtuko" alipofika kazini mapema Jumatano na kupata "mnyama wa ajabu" katika duka lake dogo.

    Fredrick Omungu hakujua ilikuwa ni nini mwanzoni, lakini alisema alikuwa na hofu.

    "Ni wazi hakuwa mbwa - nilifikiri ni chui au kitu kingine," aliiambia BBC.

    Baadhi ya majirani walifika na kumtambua mnyama huyo kuwa ni fisi ambaye kwa hali fulani anaweza kushambulia binadamu.

    "Nilishtuka na kukaa mbali. Nimesikia fisi ni hatari na wanaweza kuua watu," Bw Omungu alisema.

    Katika chini ya dakika 30, wakazi wengi walikuwa wamekusanyika karibu na kibanda chake ili kuona mnyama huyo aliyekuwa amejificha chini ya eneo moja.

    Haijulikani ni vipi mnyama huyo aliishia kwenye kibanda chake katika eneo lenye watu wengi.

    Bw Omungu, ambaye huuza miraa pamoja na vinywaji baridi, peremende na karanga, alisema alikuwa amefunga biashara yake mwendo wa saa 20:00 kwa saa za hapa nchini usiku uliopita na alifika karibu 07:00 asubuhi iliyofuata.

    Eneo hilo haliko mbali na Mbuga ya Kitaifa ya Ziwa Nakuru, ambapo fisi huyo anashukiwa kupotea kutoka usiku.

    Walinzi kutoka Shirika la Huduma ya Wanyamapori (KWS) baadaye walifika eneo hilo na kumkamata mnyama huyo.

    Mizozo kati ya wanyama na binadamu inazidi kuongezeka nchini Kenya na katika siku za hivi majuzi kumekuwa na ripoti za fisi kushambulia watu katika maeneo tofauti kote nchini.

    Soma zaidi:

  3. Zaidi ya wanafunzi 100 watekwa nyara Nigeria

    Zaidi ya wanafunzi 100 wa shule nchini Nigeria wametekwa nyara katika mji wa kaskazini-magharibi wa Kuriga, walioshuhudia wanasema.

    Wanafunzi walikuwa shuleni mwendo wa 08:30 (07:30GMT) wakati makumi ya watu wenye silaha wakiwa kwenye pikipiki walipowavamia, shahidi mmoja alisema.

    Wanafunzi hao, wenye umri wa kati ya miaka minane na 15, walichukuliwa pamoja na mwalimu, waliongeza.

    Magenge ya utekaji nyara, yanayojulikana kama majambazi, yamewateka mamia ya watu katika miaka ya hivi karibuni, hasa maeneo ya kaskazini-magharibi.

    Hata hivyo, visa vya utekaji nyara mkubwa wa watoto vimepungua katika miaka ya hivi karibuni.

    Shahidi huyo alisema kuwa mwanafunzi mmoja alipigwa risasi na watu wenye silaha na kwa sasa anapokea matibabu katika hospitali ya Birnin Gwari.

    Kuriga iko katika jimbo la Kaduna na afisa kutoka serikali ya jimbo hilo amethibitisha tukio hilo kwa BBC lakini alishindwa kutoa maelezo zaidi.

    Mnamo Januari, majambazi walimuua mkuu wa shule katika eneo hilo na kumteka nyara mkewe.

    Utekaji nyara huo unakuja siku moja tu baada ya makumi ya wanawake na watoto kuhofiwa kutekwa nyara na kundi la Kiislamu la Boko Haram walipokuwa wakikusanya kuni kaskazini-mashariki mwa Nigeria.

    Hata hivyo visa hivyo viwili vya utekaji nyara wa watu wengi havifikiriwi kuhusishwa. Magenge ya wahalifu wa utekaji nyara yanayoleta hofu kaskazini-magharibi mwa Nigeria yamejitenga na Boko Haram kaskazini-mashariki, ingawa kumekuwa na ripoti kwamba huenda walifanya kazi pamoja mara kwa mara.

  4. Wajumbe wa Hamas waondoka Cairo kwenye mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza bila makubaliano

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Ujumbe wa Hamas waondoka kwenye mazungumzo huko mjini Cairo bila makubaliano ya kusitisha mapigano yanayoendelea Gaza, lakini kundi hilo lenye silaha linasema mazungumzo ya moja kwa moja na Israel hayajakamilika.

    Ilitarajiwa kwamba makubaliano ya kusitisha mapigano kwa siku 40 yanaweza kufikiwa kwa ajili ya kuanza kwa mwezi wa Kiislamu wa Ramadhani wiki ijayo.

    Kwa dalili zaidi za kipindi cha njaa wakati ujao, shinikizo la kimataifa limeongezeka.

    Lakini wapatanishi wa Misri na Qatar wamekuwa na kipindi kigumu kusaini makubaliano ambayo yangeifanya Hamas kuwaachia huru mateka wa Israel badala ya Wapalestina wanaoshikiliwa katika jela za Israel.

    Israel haikutuma ujumbe mjini Cairo, ikisema ilitaka kwanza orodha ya mateka walionusurika ambao wanaweza kuachiliwa chini ya makubaliano hayo.

    Kwa upande mwingine, Hamas ilisema kuwa Israel haikubali matakwa yake ya kuwataka Wapalestina waliofurushwa makwao waweze kurejea nyumbani au kuondolewa kabisa kwa wanajeshi wa Israel katika miji ya Gaza.

    Vita huko Gaza vilianza wakati wapiganaji wa Hamas walipovamia kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba, na kuua takriban watu 1,200 na kuwakamata mateka 253, kulingana na hesabu za Israeli.

    Zaidi ya watu 30,800 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo, wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas inasema.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Joslin Smith: Mama na mpenzi wake washtakiwa kwa ulanguzi wa mtoto Afrika Kusini

    .

    Chanzo cha picha, MEYA MTENDAJI ANDRÈ TRUTER/ FACEBOOK

    Maelezo ya picha, Zawadi ya randi 100,000 ($5,200; £4,100) imetolewa kwa yeyote aliye na taarifa kuhusu mahali alipo Joslin.

    Mama wa msichana mwenye umri wa miaka sita aliyetoweka nchini Afrika Kusini tangu tarehe 19 Februari amefunguliwa mashtaka ya ulanguzi wa binadamu na utekaji nyara.

    Kelly Smith alishtakiwa pamoja na mpenzi wake, Jacquen Appollis, na wengine wawili, baada ya kukamatwa.

    Binti ya Bi Smith, Joslin, alitoweka nje ya nyumba yake huko Saldanha Bay, karibu na Cape Town.

    Washtakiwa hao wanne walifika mahakamani, lakini hawakuulizwa kujibu kesi ambayo imezua gumzo Afrika Kusini.

    Umati mkubwa ulikusanyika nje ya mahakama, ukiimba: "Mrudishe Joslin."

    Upande wa mashtaka unadai kuwa Bi Smith alimwagiza Bw Appollis na mshtakiwa mwingine, Stefano van Rhyn, kumuuza Joslin kwa mganga wa kienyeji kwa randi 20,000 ($1,000; £835), gazeti la kibinafsi la Citizen linaripoti.

    Mtoto hupotea kila baada ya saa tano nchini Afrika Kusini, lakini wengi hupatikana.

    Joslin bado hajapatikana, licha ya operesheni kubwa ya utafutaji iliyohusisha jeshi la wanamaji, ndege zisizo na rubani na mbwa wa kunusa.

    Polisi wanasema msako wa kumtafuta unaendelea.

    Siku ya Jumamosi, wachunguzi walipata nguo zilizokuwa na damu katika uwanja wa wazi eneo ambalo Joslin alitoweka zaidi ya wiki mbili zilizopita.

    Bi Smith na mshtakiwa mwenzake, ambaye mmoja wao ametambuliwa na vyombo vya habari kuwa mganga wa kienyeji, wamerudishwa rumande hadi Machi 13, wakati ombi la dhamana litakaposikilizwa. Wote wamesema wataomba msaada wa kisheria.

    Katika mila iliyokemewa na watu wengi, baadhi ya waganga wa kienyeji hutumia viungo vya mwili kutengeneza dawa, wakidai wanaweza kuwaponya watu magonjwa au kuboresha maisha yao.

    Bi Smith hapo awali aliambia jarida la ndani la The Daily Voice kwamba hakuwa amekata tamaa ya kumpata bintiye kufuatia kutoweka nje ya nyumba yao katika makazi yasiyo rasmi.

    Pia unaweza kusoma:

  6. Kenya: Wataalamu wahusisha kemikali ya nywele na saratani ya ubongo

    ,

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Watafiti katika Taasisi ya Utafiti wa Madawa ya Kenya (Kemri) wamegundua formaldehyde, sumu hatari ya neva ambayo inaweza kusababisha saratani ya ubongo na kudumaza kumbukumbu, katika kemikali za nywele zinazotumiwa sana nchini Kenya.

    Ripoti ya sumu ya Kemri inaonyesha kuwa angalau aina nane ya kemikali za nywele zimeathirika. Lakini, watafiti hawakutaja chapa kwenye ripoti hiyo.

    "Sita kati yazo (asilimia 75) zilitengenezwa nchini Kenya na mbili (asilimia 25) nchini Uganda na Afrika Kusini mtawalia. Tano (asilimia 62.5) ziliandikwa 'kwa matumizi ya kitaalamu pekee'," utafiti wa Kemri ulisema.

    Kemikali 11 tofauti zilitambuliwa katika aina nane za mafuta ya nywele.

    Hasa, petrolatum and sodium hydroxide (Kiwango cha 2) zilikuwepo katika asilimia 100 na asilimia 87.5 ya bidhaa za nywele, huku bidhaa kutoka kwa mtengenezaji sawa vilikuwa na formaldehyde na isoeugenol (Kiwango cha 1).

    Lakini, chapa zilizojaribiwa hutumiwa sana katika sehemu zingine za nchi, haswa Nairobi.

    Utafiti huo wa Kemri unahusishwa na mwingine uliofanywa Marekani na Ghana, ambao ulipata ushahidi kwamba matumizi ya baadhi ya bidhaa za utunzaji wa kibinafsi (PCPs) na bidhaa za nywele, kama vile rangi za kudumu za nywele na mafuta ya kemikali, viliongeza hatari ya saratani ya matiti.

  7. Serikali yatafuta wakimbizi wa ndani waliotekwa nyara Nigeria

    .

    Chanzo cha picha, BOKO HARAM

    Mamlaka katika jimbo la kaskazini-mashariki la Borno nchini Nigeria zimesema timu ya pamoja ya wana usalama kutoka Jeshi la Nigeria na Jeshi la Wanahewa limeanza operesheni ya kuwatafuta wakimbizi wa ndani waliotekwa nyara na watu wanaoshukiwa kuwa wapiganaji wa Boko Haram.

    Takriban watu 200 waliokimbia makazi yao, wengi wao wakiwa wanawake, wavulana na wasichana, walitekwa nyara walipotoka kwenye kambi zao kutafuta kuni.

    Baadhi ya wanawake wazee na watoto walio chini ya umri wa miaka 10 waliripotiwa kuachiliwa na watekaji nyara hao.

    Serikali inaiita "operesheni ya utafutaji na uokoaji".

    Wanajeshi wamezunguka misitu karibu na Gamboru Ngala na bonde la ziwa Chad.

    Wanasaidiwa na wafanyakazi wa Jeshi la anga wanaotumia helikopta kutafuta kwa upande wa juu.

    Baada ya mkutano wa usalama Alhamisi asubuhi, Mshauri Maalum wa Gavana, kuhusu masuala ya Usalama, Jenerali Abdullahi Ishaq aliambia BBC kwamba serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa waathiriwa wanarejea salama.

    Lakini bado hawajajua idadi kamili ya waliotekwa nyara.

    Taarifa ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu nchini Nigeria, ilisema tukio hilo lilitokea Alhamisi wiki iliyopita.

    Sasa imechukua serikali takriban wiki moja kukabiliana na hali hiyo.

    Kutekwa nyara kwa karibu wasichana 300 wa shule huko Chibok muongo mmoja uliopita, kulifuata mwelekeo kama huo.

    Zaidi ya wasichana 100 bado hawajapatikana.

    xx

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Soma zaidi:

  8. Magenge ya Haiti yateketeza vituo vya polisi

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Maelezo ya picha, Zaidi ya watu 15,000 wamekimbia makazi yao katika wiki iliyopita kutokana na ghasia hizo

    Magenge yanayoshinikiza kuondolewa madarakani kwa Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry yamechoma moto vituo vya polisi katika mji mkuu wa Port-au-Prince.

    Kituo cha polisi kilicho katika soko la wazi la Salomon ndicho cha hivi punde zaidi kulengwa, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.

    Magenge katika mji huo uliokumbwa na ghasia yalizidisha mashambulizi yao wakati Bw Henry alipoondoka kwa mkutano wa kilele wa kanda wiki jana.

    Machafuko hayo yamelemaza usafiri wa anga, jambo ambalo limezuia kurejea kwake.

    Bwana Henry alijaribu kusafiri hadi Port-au-Prince siku ya Jumanne lakini badala yake akaishia katika eneo la Marekani la Puerto Rico.

    Hakuweza kutua katika mji mkuu wa Haiti kwa sababu uwanja wake wa ndege wa kimataifa ulifungwa huku wanajeshi wakizuia majaribio ya watu wenye silaha kutaka kuuteka.

    Mamlaka ya usafiri wa anga katika nchi jirani ya Jamhuri ya Dominika pia iliirejesha ndege ya waziri mkuu, ikisema kwamba hawakupewa mpango unaohitajika wa safari.

    Bw Henry hajatoa taarifa yoyote kwa umma tangu alipozuru Kenya, ambapo alikuwa akijaribu kuokoa makubaliano ya nchi hiyo ya Kiafrika kuongoza vikosi vya mataifa mbalimbali kusaidia kurejesha utulivu nchini Haiti.

    Magenge katika mji mkuu walichukua fursa ya kutokuwepo kwake kuanzisha mfululizo wa mashambulizi yaliyoratibiwa.

    Soma zaidi:

  9. Watu watatu wauawa katika shambulio la Houthi kwenye meli ya mizigo

    A US Central Command image of the cargo ship

    Chanzo cha picha, Centcom

    Maelezo ya picha, Kamandi Kuu ya Marekani imetoa picha ya meli hiyo ya mizigo

    Wafanyakazi watatu wameuawa katika shambulio la kombora la Houthi kwenye meli ya mizigo kusini mwa Yemen, wamiliki wake na Marekani wanasema - vifo vya kwanza vilivyosababishwa na mashambulizi ya kundi hilo kwenye meli za wafanyabiashara.

    Meli kwa jina True Confidence iliyokuwa na bendera ya Barbados iliachwa baada ya kutokea kwa shambulio hilo Jumatano, ambalo lilileta uharibifu mkubwa.

    Mabaharia waliofariki walikuwa Wafilipino na mwingine alikuwa Mvietnam.

    Waasi wa Houthi wanasema mashambulizi yao yanaunga mkono Wapalestina katika vita kati ya Israel na Hamas huko Gaza.

    Msemaji wa jeshi la kundi linaloungwa mkono na Iran alidai kuwa lililenga meli hiyo kwa sababu ilikuwa ya "Marekani" - jambo ambalo wamiliki wamekanusha.

    Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (Centcom) ililaani "mashambulizi ya kizembe" ya Wahouthi, ambayo ilisema "yametatiza biashara ya kimataifa na kuchukua maisha ya mabaharia wa kimataifa".

    Saa chache baada ya shambulio hilo, majeshi ya Marekani yalifanya mashambulizi dhidi ya magari mawili ya angani yasiyokuwa na rubani (UAVs) nchini Yemen, ambayo Centcom ilisema yalikuwa tishio kwa meli za Jeshi la Wanamaji la Marekani katika eneo hilo.

    Televisheni ya Al Masirah inayoongozwa na Houthi iliripoti kwamba mashambulizi mawili yalilenga uwanja wa ndege katika mji wa Hudaydah wa Bahari ya Shamu.

    Soma zaidi:

  10. Siku zijazo mgombea urais akiwa mwanamume lazima mgombea mwenza awe mwanamke- Rais William Ruto

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Rais wa Kenya William Ruto amekariri kujitolea kwake kukuhakikisha kuwa sheria ya thuluthi mbili ya jinsia inatekelezwa kikamilifu katika chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) na katika serikali ya Kenya Kwanza kwa jumla.

    Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mkakati wa Baraza la Magavana Wanawake G7 jijini Nairobi, Ruto alisema kuwa serikali yake imeweka mikakati ya kufikia hitaji kiwango cha ujumuishaji wa kijinsia katika katiba na atakuwa mstari wa mbele kuonyesha kwa mfano alichosema.

    “Wakati Riggy G (Naibu rais Rigathi Gachagua) na mimi tukikubaliana jinsi mambo yatakavyokuwa siku za usoni lazima pia tukubaliane kwamba kwenda mbele ikiwa mwanamume ni mgombea wa urais mwanamke lazima awe mgombea mwenza na ikiwa mwanamke ni mgombea, mwanamume anafaa kuwa mgombea mwenza," Ruto alisema katikati ya umati wa watu waliokuwa wakishangilia.

    Aliongeza: "Lazima tufanye kwa kukusudia kuhusu hilo vinginevyo halitatokea kamwe."

    Ruto alisema wazo hilo pia linafaa kuzingatiwa katika cheo cha ugavana na nyadhifa zote za uongozi ndani ya chama.

    Alionyesha imani kuwa viongozi wengine wa chama watapokea vyema pendekezo la kufanikisha kikamilifu kanuni ya thuluthi mbili ya jinsia.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Marekani yasema utoaji wa misaada nchini Sudan sasa ndio lengo kuu

    Uwasilishaji wa misaada ya kibinadamu nchini Sudan sasa ndio lengo kuu la serikali ya Marekani kulingana na Robert Scott kutoka wizara ya mambo ya nje.

    Jeshi la Sudan lilikuwa limesema halitaruhusu usambazaji wa misaada kwa maeneo yanayodhibitiwa na vikosi vya Rapid Support Forces (RSF).

    Katika taarifa yake kwenye mtandao wa X, RSF imelishutumu jeshi la Sudan kwa "kutumia vibaya misaada ya kibinadamu" na kuwaacha raia wakiwa na njaa.

    Bw. Scott amesema kwamba majaribio ya upatanishi ya kumaliza vita kati ya Jeshi la Sudan na RSF yanasumbua.

    Vita nchini Sudan vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 12,000 na wengine karibu milioni 8 kuhama makazi yao tangu vilipoanza Aprili mwaka jana kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

  12. Niger, Mali na Burkina Faso kuunda kikosi cha pamoja ili kupambana na wanajihadi

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Niger, Mali na Burkina Faso wanasema wataunda kikosi cha pamoja ili kupambana na vitisho vya wanajihadi katika nchi zao.

    Mkuu wa jeshi la Niger Moussa Salaou Barmou alitangaza kuwa kitaanza kazi haraka iwezekanavyo, bila kutoa maelezo ya ukubwa wake.

    Alizungumza katika hotuba ya televisheni siku ya Jumatano kufuatia mazungumzo katika mji mkuu Niamey.

    Makundi yenye uhusiano na Islamic State na al-Qaeda yameua maelfu ya watu katika eneo hilo katika mwaka uliopita.

    Tawala za kijeshi katika nchi hizo tatu zimezidi kuwa washirika wa karibu katika miezi ya hivi karibuni.

    Septemba iliyopita, waliunda mkataba wa ulinzi wa pande zote unaojulikana kama Muungano wa Mataifa ya Sahel, wakijiondoa kutoka kwa kikosi cha kimataifa, G5, kilichoundwa kupambana na makundi ya jihadi katika eneo hilo.

    Ghasia katika eneo la Sahel la Afrika Magharibi zimezidi kuwa mbaya katika miaka ya hivi karibuni licha ya ahadi za serikali za kijeshi kukabiliana na mzozo wa muongo mmoja na makundi ya kijihadi.

    Nchi hizo tatu zote zimekatiza uhusiano wao na Ufaransa, ukoloni wa zamani, ambao kwa miaka mingi ulikuwa na uwepo mkubwa wa kijeshi katika eneo la Sahel.

    Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Mali, Minusma, ambao ulikuwa umekuwepo kwa zaidi ya muongo mmoja pia uliamriwa na viongozi wa nchi hiyo kujiondoa "bila kuchelewa", na kukamilisha kuondoka mwezi Desemba.

    Tawala za kijeshi zimeimarisha uhusiano na Urusi, ambayo imeingia kuziba pengo.

    Pia wametangaza kuwa wanaondoka katika jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi Ecowas.

    Soma zaidi:

  13. Zimbabwe yalaani vikwazo vipya vya Marekani na kuviita 'haramu na vya kukandamiza'

    .

    Chanzo cha picha, EPA

    Serikali ya Zimbabwe imelaani vikwazo vipya ambavyo Marekani iliweka dhidi ya rais na maafisa wakuu wa nchi hiyo siku ya Jumatatu.

    Marekani ilimshutumu Rais Emmerson Mnangagwa na wengine kwenye orodha yake ya ufisadi na ukiukaji wa haki za binadamu.

    Msemaji wa Rais Mnangagwa siku ya Jumatano alisema shutuma hizo ni za "kuwaharibia jina" na "kashfa zisizo na maana" dhidi ya viongozi na watu wa Zimbabwe.

    Vikwazo hivyo vipya vilibadilisha mpango mpana ulioanzishwa miongo miwili iliyopita.

    Naibu katibu mkuu katika timu ya mawasiliano ya Rais Mnangagwa George Charamba aliitaka Marekani kuondoa mara moja "hatua zisizo halali za kukandamiza".

    "Tunalaani kauli hizi ovu na kusema kuwa hazifai kabisa, ni za kukashifu, za uchochezi, na kuendeleza uhasama mbaya dhidi ya Zimbabwe unaofanywa na serikali ya Marekani," alisema katika taarifa yake.

    "Tunataka utawala wa Biden utoe ushahidi wa kuunga mkono shutuma hizi zisizo na msingi, na iwapo itashindwa, bila kuchelewa zaidi, iviondoe bila masharti."

    Bw Charamba pia alitoa wito kwa Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na jumuiya ya kanda ya kusini mwa Afrika Sadc kuunga mkono wito wa Zimbabwe wa kuondolewa kwa vikwazo hivyo.

    Zimbabwe pia imekuwa ikikosoa jinsi serikali ya Marekani ilivyoondoa mpango wa zamani wa vikwazo siku ya Jumatatu, ikisema kuwa Wazimbabwe hawawezi kutarajiwa kushukuru kwa hatua hiyo.

    Soma zaidi:

  14. Kampuni ya kamari, Bet365 yachunguzwa Australia

    Kituo cha Ripoti za Miamala na Uchambuzi cha Australia (Austrac) kilikuwa kimeamuru ukaguzi

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Shirika linalofuatilia uhalifu wa kifedha nchini Australia limeanzisha uchunguzi kuhusu kampuni ya kamari ya mtandaoni ya Uingereza ya Bet365 kuhusu kukiuka sheria za kupambana na utakatishaji fedha na kufadhili ugaidi.

    Kituo cha Ripoti za Miamala na Uchambuzi cha Australia (Austrac) kilikuwa kimeamuru ukaguzi wa nje kwa kampuni hiyo mnamo 2022.

    Bet365 haikujibu mara moja ombi la BBC la kutoa maoni yao.

    Sekta hii imekuwa chini ya uangalizi mkubwa baada ya kamari mtandaoni kuongezeka wakati wa janga la corona.

    "Biashara zisizo na taratibu za kutosha za kudhibiti hatari hizo zinajiweka katika hatari ya kunyonywa na wahalifu," alisema Brendan Thomas, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ripoti za Miamala na Uchambuzi cha Australia (Austrac).

    Austrac huchunguza benki, kasino na kampuni za kamari ili kuhakikisha kuwa zina mifumo thabiti ya kufuata ili kuzizuia kufaidika kutokana na mapato ya uhalifu.

    Mmiliki wa Ladbrokes Entain pia amekuwa akifanyiwa uchunguzi nchini Australia tangu 2022, huku mpinzani mwingine wa Sportsbet anakabiliwa na ukaguzi wa nje.

    Chini ya sheria za Australia, makampuni yanatakiwa kutathmini wateja na kufuatilia miamala yao ya kifedha ili kubaini, kupunguza na kudhibiti hatari ambayo wanaweza kuwa wanajihusisha na utakatishaji fedha au kufadhili ugaidi.

    Kampuni zozote zinazopatikana na Austrac kuwa na mifumo dhaifu ya kufuata zinaweza kutozwa faini.

    Katika miaka ya hivi karibuni shirika hilo limewapiga faini wakopeshaji wakuu wa Westpac na Benki ya Jumuiya ya Madola kwa kutozwa faini kubwa kwa kukiuka sheria za kupambana na utakatishaji fedha na ufadhili wa kukabiliana na ugaidi.

    Sekta ya kamari mtandaoni pia inakabiliwa na changamoto nyingine nchini Australia kama vile sheria mpya zinazopiga marufuku matumizi ya kadi za mkopo kwa kucheza kamari mtandaoni na sheria kali za serikali ya shirikisho kuhusu matangazo.

    Mwaka jana, Bet365 iliripoti hasara kubwa lakini mtendaji wake mkuu Denise Coates alilipwa karibu £221m.

    Hiyo ilikuwa £7m juu kuliko mwaka uliopita na Bi Coates pia alipata takribani £50m ya gawio.

    Nyongeza ya malipo ina maana kwamba jumla ya mshahara wake katika kipindi cha miaka minne ilipita £1bn. Bi Coates alianzisha tovuti ya Bet365 katika jengo linalobebeka katika maegesho ya magari ya Stoke-on-Trent zaidi ya miaka 20 iliyopita.

    Sasa ni mwajiri mkubwa zaidi wa sekta binafsi nchini Uingereza.

    Anafikiriwa kuwa mmoja wa wanawake tajiri zaidi wa Uingereza na kati ya watendaji wanaolipwa vizuri zaidi ulimwenguni.

  15. London: Maafisa wa polisi wakiwaokoa watu kutoka kwenye jengo lililokuwa likiungua

    Maelezo ya video, London: Maafisa wa polisi wakiwaokoa watu kutoka kwenye jengo lililokuwa likiungua

    Polisi wa jiji la London (Metropolitan) wametoa kanda ya video iliyoonyesha wakati maafisa wa polisi walipokuwa wakiingia ndani ya jengo jengo lililokuwa likiungua ili kuwaokoa watu waliokuwemo ndani.

    Takriban watu 160 walihamishwa kutoka katika jengo la makazi la Empero's Gate, lililoko eneo la kensington Kusini magharibi mwa London, baada ya moto kuenea kutoka gorofa ya chini baada ya saa sita usiku Ijumaa, tarehe 1 Machi.

    Baada ya kuingia kwenye mlango wa mbele, maafisa walipata fursa ya kuingia kwenye gorofa sita ili kuwaokoa waliokuwa ndani.

    Vyombo vya zima moto kumi na tano na wazima moto wapatao 100 pia walishiriki katika tukio hilo , na kuwaokoa wale ambao walikuwa wamekwama ndani yake.

    Supt Jill Horsfall, mmoja wa maafisa wakuu wanaohusika na polisi Kensington & Chelsea, alisema: "Ujasiri na weledi wa maafisa wa polisi ambao waliitikia haraka shughuli ya kuzima moto huu wa kutisha unaonyesha polisi bora zaidi."

    Mwanamume mwenye umri wa miaka 25 ameshtakiwa kwa tuhuma za kuwasha moto huo kwa nia ya kuhatarisha maisha na anaendelea kuzuiliwa.

  16. Watu watatu wauawa katika shambulizi la kombora la Houthi kwenye meli ya mizigo - Jeshi la Marekani

    Kamandi Kuu ya Marekani imetoa picha ya meli hiyo ya mizigo

    Chanzo cha picha, CENTCOM

    Wafanyakazi watatu wameuawa katika shambulio la kombora la Houthi dhidi ya meli ya mizigo kusini mwa Yemen, maafisa wa Marekani wanasema, vifo vya kwanza ambavyo kundi hilo hushambulia meli za wafanyabiashara .

    True Confidence iliyokuwa na bendera ya Barbados ilikuwa imeachwa na ilikuwa ikiteketea kwa moto baada ya shambulio hilo.

    Ilipigwa katika Ghuba ya Aden mwendo wa 11:30 GMT, jeshi la Marekani lilisema.

    Wahouthi wanasema mashambulizi yao ni ya kuwaunga mkono Wapalestina katika vita kati ya Israel na Hamas huko Gaza.

    Kamandi Kuu ya Marekani (Centcom), inayosimamia operesheni katika Mashariki ya Kati, ilisema wafanyakazi watatu wameuawa na takribani wanne kujeruhiwa, wakiwemo watatu mahututi.

    "Mashambulizi haya ya Wahouthi yamevuruga biashara ya kimataifa na kugharimu maisha ya mabaharia wa kimataifa," ilichapisha kwenye mtandao wa kijamii.

    Katika taarifa, kundi linaloungwa mkono na Iran lilisema wafanyakazi wa True Confidence wamepuuza maonyo kutoka kwa vikosi vya wanamaji vya Houthi.

    Ubalozi wa Uingereza nchini Yemen ulisema vifo vya mabaharia hao ni "matokeo ya kusikitisha lakini yasiyoweza kuepukika ya Wahouthi kurusha makombora katika meli za kimataifa" na kusisitiza kuwa mashambulio hayo yanapaswa kukomesha.

    Maafisa wa Marekani na Uingereza walikuwa wameripoti awali vifo viwili na majeruhi sita. Meli hiyo ilikuwa na wafanyakazi 20, wakijumuisha raia mmoja wa India, wanne wa Vietnam na 15 raia wa Ufilipino. Walinzi watatu wenye silaha, wawili kutoka Sri Lanka na mmoja kutoka Nepal.

    Unaweza kusoma;

  17. Rais wa Senegal atangaza uchaguzi kufanyika Machi

    Senegal imeonekana kwa muda mrefu kama mojawapo ya nchi zenye demokrasia imara zaidi barani Afrika.

    Chanzo cha picha, AFP

    Serikali ya Senegal imetangaza kuwa uchaguzi wa rais wa nchi hiyo utafanyika tarehe 24 Machi.

    Tangazo hilo linafuatia hali ya mvutano nchini humo baada ya Rais Macky Sall kuahirisha uchaguzi mwezi uliopita, na hivyo kuzua maandamano makubwa.

    Rais, ambaye muhula wake unamalizika tarehe 2 Aprili, alikuwa amesisitiza kwamba hakunuia kugombea muhula wa tatu madarakani.

    Wapinzani wake walikuwa wamemshutumu kwa kuandaa mapinduzi ya kikatiba.

    Senegal imeonekana kwa muda mrefu kama mojawapo ya nchi zenye demokrasia imara zaidi barani Afrika.

    Ni nchi pekee katika Afrika Magharibi ambayo haijawahi kuwa na mapinduzi ya kijeshi.

    "Rais wa Jamhuri aliarifu Baraza la Mawaziri kwamba tarehe ya uchaguzi wa urais ilikuwa imepangwa Jumapili Machi 24," baraza la mawaziri lilisema katika taarifa.

    Kabla ya tangazo la Jumatano, viongozi walikuwa wamejaribu kuahirisha uchaguzi wa awali wa Februari 25 hadi Desemba, ambao ulisababisha machafuko mabaya mitaani.

    Lakini Baraza la Katiba baadaye liliamua kwamba uchaguzi wa urais lazima ufanyike kabla ya tarehe 2 Aprili.

    Mapema Jumatano jioni, Bw Sall alivunja serikali na kumweka Waziri Mkuu Amadou Ba na Waziri wa Mambo ya Ndani Sidiki Kaba.

    Hii ilikuwa ili Bw Ba, mgombea urais wa muungano tawala, aweze kuzingatia kampeni yake ya uchaguzi, ofisi ya rais ilisema.

    Rais Sall amehudumu kwa mihula miwili kama kiongozi wa Senegal na alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2012 aliahidi kuwa hatakaa kwa muda mrefu.

  18. Tishio kwa wapenzi wa jinsi moja Ghana: 'Tunaishi kwa hofu ya watekaji nyara'

    g

    Chuki kwa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsi moja si jambo la kawaida nchini Ghana, ambapo mapenzi ya watu wa jinsi moja tayari ni kinyume cha sheria na yanahukumiwa kwa kifungo cha miaka mitatu jela, lakini sasa jumuiya hiyo ya LGBTQ+ inahisi hofu.

    Mswada mpya, uliopitishwa na Wabunge wiki iliyopita, utaweka kifungo cha hadi miaka mitatu jela kwa mtu yeyote atakayejimbulisha tu kama anayeshiriki mapenzi ya jinsi moja au LGBTQ+ kwa ujumla na miaka mitano kwa kutangaza shughuli zao.

    "Jamaa aliniambia ikiwa mswada huu utapitishwa, nafasi yoyote atakayenipata, atanitia sumu kwa sababu mimi ni chukizo kwa familia," Mensah, ambaye jina lake limebadilishwa ili kulinda utambulisho wake, anaiambia BBC.

    Akiwa amevalia vazi jeusi kabisa, kijana huyo aliye katika umri wa mwisho wa balehe anaonekana kuwa na hofu kubwa: "Nina wasiwasi sana mtu yeyote anaweza kuniteka nyara hata katika majirani zangu wenyewe. Itakuwa vigumu sana kuishi hapa."

    Amekuwa akiishi kwa muda na marafiki wanaomhurumia katika mji mkuu wa Ghana, Accra, tangu alipokosana na familia yake.

    Haijulikani wazi jinsi jumuiya ya LGBTQ+ ilivyo kubwa nchini Ghana, taifa la kidini na la kimila, lakini wana mwelekeo wa kusaidiana wakati mmoja wao anakabiliwa na maisha kama mtu aliyetengwa.

    Mensah anasema mama yake alipogundua miaka kadhaa iliyopita kwamba alivutiwa na wavulana, alianza kumpeleka makanisani kwa maombi akiwa na matumaini kwamba angebadilika.

    "Hakuna marafiki isipokuwa marafiki zangu wa kanisa waliruhusiwa kuniona. Ilinibidi kujifunza Biblia 24/7, kuomba na ningekaa nyuma wakati wowote tunapoenda kwenye mikutano."

    Anasema alikuwa akizuiliwa nyumbani - familia kubwa haikuzungumza naye na alipata sura yao isiyoweza kuvumilika."Walihisi ningekuwa na ushawishi kwa binamu zangu na watoto wadogo."

    Unaweza pia kusoma:

    • Muswada wa Ghana wa kupambana na LGBTQ+ ni nini?
  19. Vita vya Ukraine: Milipuko yaitikisa Odesa wakati Zelensky akikutana na Waziri Mkuu wa Ugiriki

    g

    Chanzo cha picha, Reuters

    Milipuko mibaya imeutikisa mji wa bandari wa Odesa kusini mwa Ukraine wakati Rais Volodymyr Zelensky alipokuwa akikutana na Waziri Mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis.

    Jeshi la wanamaji la Ukraine linasema watu watano waliuawa. BBC imeambiwa hakuna yeyote kati ya wajumbe hao aliyejeruhiwa.

    Bw Mitsotakis alisema wawili hao walisikia sauti ya ving'ora na milipuko.

    Urusi ilisema ililenga kituo cha ndege zisizo na rubani katika eneo la bandari ya kibiashara ya mji huo wakati wa shambulizi siku ya Jumatano.

    Rais Zelensky aliishutumu Urusi kwa "kutojali ni nani wanawalenga", akisema Moscow "imekuwa wazimu au haidhibiti kile ambacho jeshi lao la kigaidi linakifanya".

    Wakati wa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari , waziri mkuu wa Ugiriki alisema "tulisikia sauti za ving'ora na milipuko iliyotokea karibu nasi. Hatukupata muda wa kufika kwenye makazi."

    "Ni uzoefu mkali sana... Ni tofauti sana kusoma kuhusu vita kwenye magazeti, na kusikia kwa masikio yako, kuiona kwa macho yako," aliongeza.

    Bw Zelensky shambulio hilo limesababisha "vifo na majeruhi", lakini akasema hana takwimu kamili.

    Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema kuwa imefanikiwa kushambulia kituo cha ndege cha kijeshi cha wanamaji cha Ukraine. Haijabainika mara moja ikiwa Moscow ilikuwa inazungumzia kuhusu milipuko ile ile iliyozungumziwa na viongozi hao wawili.

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi:

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine
  20. ‘Tunajua kitakachokuja’: Wakazi wa mashariki mwa Ukraine wanajipanga kwa mashambulio ya Urusi

    f

    Chanzo cha picha, BBC/XAVIER VAN PVENAEG

    Maelezo ya picha, Mashariki mwa Ukraine, wimbi la vita hivi halijabadilika - linakuja kwa kasi.

    Mashariki mwa Ukraine, wimbi la vita hivi halijabadilika - linakuja kwa kasi.

    "Tunajua kitakachokuja," anasema Mariya huku akifungasha televisheni kwenye nyumba yake katika mji wa Kostyantynivka. Anaipeleka Kyiv kabla ya kufunga safari kwenda huko pamoja na mwanaye.

    "Tumechoka siku nzima [na kuteseka] wasi wasi na mashambulizi. Inasikitisha mara kwa mara, na tunaogopa."

    Mnamo Februari, Urusi iliteka mji wa kimkakati wa Avdiivka. Tangu wakati huo, wavamizi wamesonga mbele zaidi magharibi, na kuchukua vijiji kadhaa.

    Ukraine inasema vikosi vyake "vinaishikilia". Lakini wanajeshi wa Urusi sasa wanashambulia katika maeneo matano kwenye mstari wa mbele wa kilomita 1,100 (maili 700).

    Na ni hapa katika eneo la mashariki la Donetsk ambapo watetezi wa Ukraine wanakabiliwa na changamoto zaidi.

    Watu katika miji kama Pokrovsk, Kostyantynivka na Kramatorsk sasa wanakabiliwa na mstari wa mbele unaokaribia haraka, na hata kazi.

    Mariya na mama yake Tetyana wanapata maisha magumu zaidi huku Warusi wakisonga mbele zaidi.

    g

    Chanzo cha picha, BBC/XAVIER VAN PVENAEG

    Maelezo ya picha, Tetyana anakataa kuondoka Kostyantynivka. "Tayari nimetoka mara mbili, kuna faida gani?" anasema

    Wafanyikazi hubadilisha paneli za dhahabu kwenye kanisa baada ya kulipuliwa na shambulio la kombora kwenye kituo cha treni jirani, ambacho sasa kimeharibiwa.

    Vita vya Ukraine: Mengi zaidi:

    • YA MSINGI:Mzozo wa Ukraine: Kwanini Urusi inaivamia Ukraine na Putin anataka nini?
    • UFAFANUZI:Mzozo wa Ukraine: Swift ni nini na kwa nini kuipiga marufuku Urusi ni muhimu sana?
    • UCHAMBUZI:Mzozo wa Ukraine: Putin humsikiliza nani?
    • KWENYE RAMANI:Uvamizi wa Ukraine: Shambulio la Urusi kwenye ramani
    • ZELENSKY:Volodymyr Zelensky: Mfahamu rais wa Ukraine aliyeacha umaarufu wake wa TV na kuingia kwenye siasa
    • PUTIN:Vladimir Putin: Rais wa Urusi aliyeagiza shambulio Ukraine