Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Ulikuwa ujanja mkubwa zaidi wa kukwepa jela katika miaka 30 ': Wanaume waliotoroka Alcatraz kutumia kijiko
Na Myles Burke
Mnamo tarehe 12 Juni 1962, wanaume watatu walitoroka kutoka Alcatraz, wasionekane tena. Hatima ya mwisho ya Frank Morris na kaka wawili Anglin inasalia kuwa kitendawili lakini werevu na uamuzi wa kutoroka kwao kwa ujasiri - kutoka kwenye gereza lililokuwa salama zaidi Marekani - unaendelea kuwashangaza wengi. Miaka miwili baadaye, BBC ilirejea katika eneo la uhalifu.
Mnamo Mei 1964, Michael Charlton wa BBC Panaroma alifanya "safari ya kuogopwa zaidi katika ulimwengu wa uhalifu" kuvuka bahari ya San Francisco Bay kuona kisiwa cha gereza maarufu cha Alcatraz. Kwa jina la utani "The Rock", gereza hilo la serikali lilikuwa limeshikilia baadhi ya wahalifu hatari zaidi nchini Marekani.
Ilizingatiwa kama ngome isiyoweza kushindwa. Lakini katika masaa ya mapema ya 12 Juni 1962, wanaume watatu walifanya kile kilichofikiriwa kuwa hakiwezekani: walitoroka kutoka gereza hilo.
Alcatraz hapo awali ilikuwa ngome ya ulinzi wa majini ili kulinda mlango wa ghuba. Wakati wa Vita vya Wenyewe kwa Wenyewe vya Marekani, kwa sababu ya kutengwa kwa kisiwa hicho, miamba mikali na mikondo ya baridi kali iliyokizunguka, wafungwa wa Muungano waliotekwa walizuiliwa huko.
Mapema katika Karne ya 20 ilijengwa upya kama gereza la kijeshi. Katika miaka ya 1930, Marekani ilipojaribu kukabiliana na uhalifu wa kupangwa uliokithiri ambao ulisitawi wakati wa Marufuku dhidi ya pombe Wizara ya Sheria ilichukua sehemu hiyo. Punde wafungwa wa kuogopwa zaidi kutoka kwa mfumo wa magereza wa serikali walianza kuwasili. Miongoni mwa wafungwa wake maarufu zaidi walikuwa majambazi mashuhuri Al Capone, Mickey Cohen na George "Machine Gun" Kelly, pamoja na muuaji aliyehukumiwa Robert Stroud, ambaye baadaye angejulikana zaidi kama "Birdman of Alcatraz". "Wanaume waovu sana na wasumbufu kuzuiliwa katika jela ya kawaida," ndivyo mwandishi wa BBC Charlton alivyowalezea .
'Kwa muda wa miezi kadhaa, wanaume hao walichimba ukuta wenye saruji iliyodhoofishwa na chumvi karibu na tundu la hewa chini ya sinki zao'
Miaka minne kabla ya Panorama kusafiri huko, Frank Lee Morris alikuwa amewasili kwenye kisiwa hicho. Akiwa yatima akiwa na umri wa miaka 11, na kuhukumiwa kwa uhalifu wake wa kwanza akiwa na umri wa miaka 13, Morris alikuwa ametumia muda mwingi wa maisha yake ndani na nje ya vituo mbalimbali vya kurekebisha tabia.
Alichukuliwa kuwa mwerevu sana, alikuwa mhalifu mwenye uzoefu, mwenye hati ya mashtaka kuanzia kupatikana na dawa za kulevya hadi unyang'anyi wa kutumia silaha .
Alikuwa ametumwa the Rock mnamo Januari 1960 kufuatia kutoroka kwake kutoka gereza la Jimbo la Louisiana. Mara tu alipofika Alcatraz, alianza kufikiria jinsi angeondoka. Alikutana katika chumba chake cha seli na ndugu waliohukumiwa kupora benki John na Clarence Anglin na Allen West, ambao walikuwa wafungwa wa Alcatraz tangu 1957. Wanaume hao wote walifahamiana kutokana na vifungo vya awali katika magereza mengine na kwa kuwa walikuwa na seli za zinazopakana katika jela waliweza kusemezana usiku.
Wakati mwandishi wa BBC Charlton alipotembelea eneo hilo , mwaka mmoja baada ya kufungwa kwake, alifahamu vyema sifa ya kutisha ya gereza hilo kwa walinzi wakali, hali ngumu na adhabu ya upepo wa bahari ambayo wafungwa walipaswa kuvumilia. "Upepo usiokoma ambao hauonekani kusimama kamwe, unavuma na mwangwi kupitia baa," alisema. "Imejengwa juu ya vijia vya ngome ya zamani ... misingi ya leo ya Alcatraz inaoza na kuvunjika."
Mpango kabambe
Wakiongozwa na Morris , wafungwa hao wanne walianza kubuni mpango madhubuti wa kutoroka. Kwa kipindi cha miezi kadhaa, wanaume hao walichimba ukuta wa saruji ulioharibiwa na chumvi karibu na tundu la hewa chini ya sinki zao. Wakitumia vijiko vya chuma vilivyochukuliwa kutoka kwenye jumba la kulia chakula, walichimba hadi kwenye eneo la matumizi lisilo na ulinzi.
Ili kuficha kelele za kuchimba ukuta Morris angecheza ala yake ya muziki wakati wa saa ya kila siku ilitolewa kwa muziki ulipopigwa kwa wafungwa. Mara baada ya kutengeneza shimo kubwa la kutosha kutambaa hadi kwenye korido, walipanda hadi ngazi ya juu ya kizuizi cha seli na kuanzisha karakana ya siri.
Ili kuficha mashimo ya ukuta wa seli, walitengeneza grill bandia za karatasi kutoka kwa majarida ya maktaba ya gereza. Mara tu walipokuwa kwenye karakana yao walianza kutengeneza rafu ya 6x14ft na vesti za kuokoa maisha zilizotengenezwa kwa zaidi ya makoti 50 ya mvua yaliyoibiwa. Ili kuziba mpira huo, waliyeyusha kwa kutumia mabomba ya mvuke ya gereza. Kisha walibadilisha eneo hilo kuwa karakana ya kuingiza rafu na kutengeneza padi kutoka kwa vipande vya mbao.
Lakini walipokuwa wakifanya kazi, walihitaji kuficha kutokuwepo kwao kwa walinzi ambao mara kwa mara walifanya ukaguzi wa usiku. Kwa hiyo, walichonga vipande vya karatasi kuunda sanamu ya vichwa vyao kutoka kwa sabuni na dawa ya meno .
Ili kuzifanya sanamu zionekane za kweli zaidi, walitumia nywele halisi kutoka kwenye kinyozi cha gereza na kuzipaka rangi za kwa kutumia vifaa vya sanaa vilivyoibiwa.
Kisha waliziweka sanamu hizo kwenye vitanda vyao, wakiwa na mabunda ya nguo na taulo chini ya blanketi zao katika umbo la miili yao ili waonekane wamelala. Walipokuwa wakifanyia kazi vifaa vyao vya kutoroka vya muda, pia walikuwa wakitafuta njia ya kutoka. Wakitumia mabomba kama ngazi, walipanda futi 30 (9.1m) na wakathamini kufungua kipumulio kilicho juu ya ufa wa gereza. Walitengeneza bolti bandia kutoka kwa sabuni ili kuifanya thabiti .
Hatimaye, usiku wa tarehe 11 Juni 1962, walikuwa tayari kutekeleza mpango wao wa kistadi. Wakiviacha vichwa hivyo vitandani ili kuwadanganya walinzi, Morris na wale ndugu wawili wa Anglin walitambaa nje kupitia mashimo kwenye kuta za seli.
West hakuweza kutoroka kutoka seli yake kwa wakati kwa hivyo wengine waliondoka na kumuacha. Walipanda hadi kwenye paa la chumba cha seli, wakakimbia juu yake - wakiwa wamebeba mashua yao ya muda, mbele ya mnara wa walinzi - wakashusha bomba la nje la maji, wakavuka ua wa gereza, wakapanda uzio wa nyaya mbili za miinuko wa futi 12 (3.7m) .. Chini ya tuta la mwinuko kuelekea ufuo wa kaskazini-mashariki wa kisiwa hicho. walianza safari yao.
Kwenye ukingo wa maji, walijaza hewa mashua yao na kutoweka gizani.
King'ora hakikulia hadi asubuhi iliyofuata, wakati midoli ya vichwa vyao ilipogunduliwa .
'Kuanzia wakati wa kutoroka kwao mnamo 1962, kulikuwa na ripoti za madai ya kuonekana kwa wanaume na jumbe kutoka kwao'
Kisiwa hicho pia kilikuwa makao kwa familia za walinzi waliofanya kazi katika gereza hilo. Baba ya Jolene Babyak, ambaye alikuwa kaimu mlinzi wa Alcatraz wakati huo, aliwasha king'ora. "Nilipoamka, king'ora kilikuwa bado kinakereza.
Kilikuwa kinatoa sauti ya juu, kilisikika sana, kilikuwa cha kutisha', aliiambia BBC Witness History mwaka wa 2013 .
"Nilishtuka unajua, na wazo langu la kwanza lilikuwa kwamba haliwezi kuwa jaribio la mfungwa kutoroka, na, bila shaka, ilibainika kwamba ni kweli wafungwa walitoroka"
Gereza lilifungwa mara moja na msako mkali wa majengo yote, pamoja na makaazi ya maafisa wa magereza. Wakati huohuo babake Jolene alianzisha msako mkali huku mamia ya maafisa wa polisi wakitafuta sana eneo jirani kwa siku. Mnamo tarehe 14 Juni, Walinzi wa Pwani walipata moja ya pala za wafungwa.
Siku hiyo hiyo, wafanyikazi walipata pakiti ya vitu vya kibinafsi vya Waanglin, ikiwa imefungwa kwa mpira. Siku saba baadaye baadhi ya mabaki ya rafu yalisombwa karibu na Daraja Golden Gate Bridge na siku iliyofuata moja ya vesti za kuokoa maisha baharini ziligunduliwa. Lakini wafungwa hao watatu hawakuonekana tena.
Kesi iliyo wazi
Ingawa wafungwa walitoroka gerezani, mamlaka ilihitimisha kuwa lazima waliangamia katika maji hatari wakijaribu kuondoka kisiwani.
Hayo hakika yalikuwa maoni ya mkuu wa gereza Richard Willard wakati BBC ilipomhoji mwaka wa 1964.
Kwa ufahamu wetu, hakuna mtu anayetembea mitaani leo akijigamba kuwa ametoroka kutoka kwa Alcatraz," alisema. "Kwa nini nina uhakika sana? Unasikia upepo, sivyo? Na unaona maji? Unafikiri unaweza kuyashinda?"
Gereza la Alcatraz lilifungwa mwaka 1963, mwaka mmoja baada ya wanaume hao kutoroka. Kwa kiasi fulani hii ilitokana na kuzorota kwa muundo wake na gharama ya kuiendesha lakini utawala mkali wa gereza hilo pia ulikuwa na utata kwa muda mrefu. Mapema kuanzia 1939, Mwanasheria Mkuu wa Marekani Frank Murphy alijaribu kuifunga, akisema: "taasisi nzima inazingatia saikolojia ambayo inajenga tabia mbaya kati ya wafungwa".
Katika Historia
Katika Historia ni mfululizo unaotumia kumbukumbu ya kipekee ya sauti na video ya BBC kuchunguza matukio ya kihistoria ambayo bado yanasikika leo. Jiandikishe kwa jarida la kila wiki .
Kwa miaka mingi, wafungwa walikuwa wamejiua au kujitia ulemavu - hawakuweza kukabiliana na hali hiyo ngumu - na kadiri miaka ya 1960 ilivyokuwa ikiendelea, Marekani ilitazamia kurekebishwa kwa wafungwa badala ya adhabu yao tu.
Kwa upande wa watatu waliotoroka, licha ya kuwa hakuna miili iliyowahi kupatikana kwenye ghuba hiyo, mwaka 1979 walitangazwa kuwa wamekufa kisheria. FBI ilifunga kesi hiyo na kukabidhi jukumu kwa Huduma ya Wanajeshi wa Marekani.
Lakini uvumi juu ya hatima yao haujawahi kukoma. Mwaka huo huo walitangazwa kuwa wamekufa, filamu ya Escape from Alcatraz ilitolewa huku Clint Eastwood akiigiza kma Frank Morris. Na tangu walipotoroka mwaka wa 1962, kulikuwa na ripoti za madai ya kuonekana kwa watu hao, na ujumbe kutoka kwao.
Mnamo 2018, polisi wa San Francisco walifichua kuwa walikuwa wametumiwa barua ya kushangaza miaka mitano mapema, kutoka kwa mtu anayedai kuwa John Anglin . Barua hiyo ilisema "Nilitoroka kutoka Alcatraz mnamo Juni 1962. Ndiyo sote tulifanikiwa (kukweoa)usiku huo, lakini kwa shida!" Barua hiyo ilishikilia kuwa watu hao walikuwa wakiishi kwa siri, huku Frank Morris akifariki Oktoba 2005, na Clarence Anglin mwaka wa 2008. Mwandishi wa barua hiyo alisema sasa anataka kujadiliana na serikali kuhusu kujisalimisha kwake ili kupata matibabu ya saratani. FBI ilitathmini barua hiyo lakini haikuweza kuthibitisha ikiwa ilikuwa ya kweli au la.
Kesi hiyo bado iko wazi kwa Huduma ya Wanajeshi wa Marekani. Hivi majuzi mnamo 2022, ilitoa picha zilizosasishwa za jinsi wafungwa hao watatu waliopotea wa Alcatraz wanavyooweza kuonekana kwa sasa, huku ikiomba habari yoyote kuwahusu, kwa matumaini kwamba mwishowe inaweza kulifumbua fumbo la hatima yao.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah