Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Zambia ilifanya elimu kuwa bure, sasa madarasa yamejaa
- Author, Marco Oriunto
- Nafasi, BBC News, Kafue
Ni saa moja asubuhi yenye baridi kali na kundi la wanafunzi limewasili hivi punde katika shule ya Msingi na Sekondari ya Chanyanya, umbali wa zaidi ya saa moja kwa gari kuelekea kusini-magharibi mwa mji mkuu wa Zambia, Lusaka.
"Unahitaji kufika shuleni mapema kwa sababu kuna uhaba wa madawati," anasema mwanafunzi mwenye umri wa miaka 16 Richard Banda. "Siku mbili zilizopita nilichelewa na niliishia kukaa sakafuni - kulikuwa na baridi sana."
Usumbufu wake unaelezea tatizo la ukosefu wa rasilimali na msongamano wa wanafunzi ambao umekuja kutokana na kutoa elimu ya bure ya shule za msingi na sekondari hapa.
Shule iko katika kiwanja kilicho na vyumba 10 vya madarasa vilivyopangwa kwa umbo la kiatu cha farasi kuzunguka uwanja wa michezo ambapo miti ya mshita na mimea inachipuka kutoka mchangani.
Miale ya jua la asubuhi na mapema inanaswa katika wingu la vumbi lililotikiswa na wavulana na wasichana wanaofagia madarasa.
Muda mfupi kabla ya kengele kulia, mmoja wa wanafunzi anakimbia hadi katikati ya uwanja wa michezo na kuinua bendera ya Zambia juu ya mlingoti mrefu.
Taratibu hizi za mwanzo wa siku zimekuwa sehemu ya utaratibu mpya kwa watoto milioni mbili wa ziada ambao tangu 2021 wameweza kwenda shule za serikali bila kulazimika kulipa, kwa sababu serikali ilifanya shule kuwa bure kwa kila mtu.
Lakini bila uwekezaji wa kutosha wa miundombinu, wataalamu wanasema msongamano wa wanafunzi sasa unatishia ubora wa elimu hasa kwa wanafunzi kutoka jamii za kipato cha chini.
"Niliacha kwenda shule mwaka wa 2016 nikiwa darasa la nne," anasema Mariana Chirwa mwenye umri wa miaka 18 akiwa amevalia sare za wasichana wa Chanyanya, shati la rangi ya samawati .
“Bila elimu ya bure sijui wazazi wangu wangewezaje kunirudisha shuleni. Hawafanyi kazi na wapo tu nyumbani."
Bango la idadi ya wanafunzi katika darasa linaloning'inia kwenye ukuta wa ofisi ya mwalimu mkuu linaonyesha changamoto zinazokabili shule kama Chanyanya.
Katika moja ya darasa, wavulana 75 na wasichana 85 wamebanwa kwenye nafasi ambayo ingetosha wanafunzi 30 tu.
"Nilipoanza mnamo 2019 nilikuwa na wanafunzi 40, lakini sasa ni karibu 100 zaidi, na hiyo ni katika darasa moja," anasema mwalimu Cleopatra Zulu mwenye umri wa miaka 33.
"Kila siku tunapokea wanafunzi wapya kwa sababu ya elimu ya bure. Kuzungumza moja kwa moja ni vigumu, hata kusahihisha vitabu ni changamoto. Tumepunguza hata idadi ya masomo tunayowapa”.
Masaibu ya mwanafunzi Richard Banda yanaonyesha hili.
"Hatujifunzi kwa njia sawa na nyakati zile ambazo tulikuwa tunalipa, kuna tofauti kidogo," anaambia BBC.
"Tulipokuwa wachache mwalimu alikuwa akifafanua mada tena ikiwa hauelewi, lakini sasa kwa sababu tuko wengi, mwalimu harudii tena. Hiyo ndiyo tofauti.”
Ongezeko la idadi ya wanafunzi linaonyeshwa kote barani Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na watoto wengi shuleni kuliko hapo awali, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto Unicef linasema.
Lakini kutokana na kuwa na wanafunzi tisa kati ya 10 wa shule za msingi katika sehemu hiyo bado wanatatizika kusoma na kuelewa maandishi rahisi, kulingana na Unicef, lengo la watunga sera sasa linahamia kwenye ubora wa elimu, kuajiri walimu wenye sifa na miundombinu na rasilimali.
"Usipoketi vizuri darasani, hiyo inaathiri jinsi unavyozingatia kufundisha, jinsi unavyoandika maandishi yako," anasema Aaron Chansa, mkurugenzi wa Kitengo cha Kitaifa cha Elimu ya Ubora nchini Zambia (NAQEZ) , ambayo huishauri serikali
"Tunaona wanafunzi wakiingia sekondari wakati hawawezi kusoma vizuri," anasema, akiongeza kuwa kuna matatizo kote nchini.
“Katika Jimbo la Mashariki tuna zaidi ya wanafunzi 100 katika darasa moja. Hii pia imezidisha uwiano wa kiasi cha vitabu-kwa-wanafunzi. Katika baadhi ya matukio unakuta kitabu kimoja kinapiganiwa na wanafunzi sita au saba.”
Serikali inasema inasikiliza na kuchukua hatua za kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kwa kuifanya elimu kuwa bure.
"Hili ni tatizo zuri," anasema Waziri wa Elimu Douglas Syakalima. "Ni afadhali kuwaacha watoto wawe katika darasa lenye msongamano kuliko mitaani."
"Rais alizindua uzalishaji mkubwa wa madawati, ujenzi wa miundombinu unafanyika.'
Zambia imewekeza zaidi ya $1bn (£784m) katika sekta ya elimu tangu kuanzishwa kwa elimu bila malipo miaka mitatu iliyopita - nyongeza inayohitajika sana baada ya miaka mingi ya kupungua kwa matumizi ikilinganshwa na Pato la Taifa katika sekta hii.
Serikali imetangaza mipango ya kujenga shule mpya zaidi ya 170 na imejitolea kuajiri walimu wapya 55,000 kufikia mwisho wa 2026, ambapo 37,000 tayari wameajiriwa.
Hatua hiyo imetoa nafasi mpya za kazi, lakini pia imesababisha uhaba wa makazi katika maeneo ya vijijini. Baadhi ya walimu wanaripoti kuishi katika nyumba zilizoezekwa kwa nyasi na kutumia vyoo vya shimo, ambavyo viko hatarini kufurika.
"Wakati wa msimu wa mvua hapa, hutaki kabisa kututembelea," asema Bi Zulu, ambaye anaishi katika eneo la shule na anakumbuka kuwa na wasiwasi kuhusu hatari ya kipindupindu wakati wa mlipuko wa mapema mwaka huu.
Nje kidogo ya nyumba yake, sehemu kubwa povu ya sabuni iliyokaushwa inaashiria mahali ambapo mmoja wa wakazi alioga mapema, mahali pa wazi, huku faragha ikitolewa tu na giza kabla ya jua kuchomoza.
"Nyumba tunazoishi ni kama mtego wa kifo," asema Bi Zulu. "Serikali inapaswa kufanya kitu kuhusu nyumba, haswa vyoo."
Wakiwa na wasiwasi kuhusu matokeo ya masomo haya ya bure, baadhi ya familia zimeanza kuchukua hatua kimyakimya.
Robert Mwape ni dereva wa teksi anayeishi Lusaka.
Mnamo 2022, alimhamisha mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 11 kutoka shule ya kibinafsi ya kulipia karo hadi shule ya umma ili kufaidika na elimu ya bure, lakini hivi karibuni alijutia hatua hiyo.
"Niliona matokeo [ya mwanangu] yalianza kushuka. Kwa hiyo siku moja niliamua kutembelea darasa lake. Kulikuwa na wanafunzi wengi . Unajua jinsi vijana walivyo - wengi wao, wanapoteza muda wakizungumza. Mwalimu hakuweza kuzingatia kinachoendelea katika darasa zima.”
Mwaka uliofuata Bw Mwape, ambaye hakutaka tutumie jina lake halisi, alibatilisha uamuzi wake wa awali. Sasa akiwa na umri wa miaka 13, mwanawe amerudi katika shule ya kibinafsi.
Huku Zambia ikiibuka polepole kutokana na kutolipa deni mwaka 2020, baadhi ya wataalam wametilia shaka uendelevu wa sera ya elimu ya bila malipo.
Ripoti ya mwaka 2023 kutoka Taasisi ya Zambia ya Uchambuzi wa Sera na Utafiti inasema kwamba kama wanafunzi wote wanaostahiki watapokea ofa ya elimu bila malipo, matumizi ya serikali yanakadiriwa kuongezeka maradufu, na "kuibua maswali juu ya dhamira ya serikali zinazofuata kuendelea na sera hii".
Lakini waziri wa elimu anasema ana imani kuwa utawala unaweza kumudu gharama.
"Mimi sioni [changamoto] mwenyewe. Elimu ndiyo sera bora ya kiuchumi,” anasema Bw Syakalima.
Kutoa elimu bila malipo kunaonekana kote kama hatua ya kwanza ya kuwapa Wazambia chipukizi nafasi nzuri ya maisha bora ya baadaye.
Lakini uzoefu wa nchi hadi sasa unaonyesha changamoto za kusimamia idadi inayoongezeka ya wanafunzi huku wakijaribu kudumisha ubora wa elimu wanayopokea.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah