'Ninajuta kuwekeza kihisia na kiuchumi katika mahusiano ambayo hayakudumu'

Muda wa kusoma: Dakika 4

Baada ya kuvunjika kwa mahusiano na mzazi mwenzangu,faraja pekee ilikuwa familia yangu. Kutofahamu wenza vizuri,ni moja kati ya makosa yanayoleta majuto katika mahusiano.

‘’Watoto wangu wananipa msukumo wa kupigania ndoto yangu kwa bidii zaidi’’anaeleza Grace Urassa mfugaji wa kuku kutoka Pwani Tanzania.

Malezi ya watoto yanayotegemea upande mmoja ni mojawapo ya changamoto inayokabili wanawake wengi katika jamii na kuwa kikwazo cha kuinuka tena mara mahusiano yanapoyumba au hata kuvunjika,kama anavyoeleza Grace Urassa.

‘’Ni kumbukumbu ya kuumiza ambayo imenifundisha katika maisha yangu,hasa kuwa mkweli na kufanya utatifi vizuri kumjua mtu kabla ya kumuamini na kuingia katika mahusiano ya kimapenzi,anaeleza Grace.

‘’2018 mzazi mwenzangu aliniambia ameamua kurudi kwa mkewe,dini zetu haziruhusu mitala’’anaeleza Grace. Ni maamuzi ambayo yalinishangaza na kunisikitisha,kwani hata mimi niligundua kuwa sikumfahamu vya kutosha,ilinipa darasa kubwa, anaongeza Grace.

Amelelewa mkoani Kilimanjaro na wazazi waliopenda maadili na nidhamu ya hali ya juu,anaeleza Grace kwamba kufanya kazi za nyumbani hasa za mikono ilikuwa ni utaratibu wa kawaida nyumbani na wala haikuwa kama adhabu kwake.

Malezi hayo yamemfanya kuweza kuyasimamia maisha yake hata katikati ya nyakati ngumu.

Alikutana kazini na aliyekuwa mzazi mwenzie,na baadae kushirikiana kiuchumi katika uwekezaji kabla ya penzi lao kuvunjika na kila kitu kubadilika.

Anasema baada ya kujifungua mtoto wake wa pili alipata changamoto ya kupoteza ajira yake katika taasisi aliyokuwa akifanya kazi na kulipwa stahiki zake.Penye nia pana njia Grace anasema kabla ya kukutana na mwenzake ailikuwa na ndoto zake za kumiliki shamba kubwa la ufugaji nchini Tanzania,aliamua kuzisimamia hata kama mwenzake amebadili uelekeo.

Aliamua kutafuta ushauri sahihi wa wataalamu wa ufugaji na kuelekeza nguvu kwenye ufugaji ambao ulikuwa ndoto yake ya miaka mingi.

Maisha yako yalibadilika kwa kiasi gani baada ya kuachana na mzazi mwenzako?

Grace anasema alikata tamaa na kupoteza nuru kabisa.Ndugu wazazi na watoto wake walikuwa faraja yake wakati huo.

‘’walinifariji na kunikumbusha kutozima ndoto zangu bali nisonge mbele’’anaeleza

Mtazamo wa jamii ukoje?

Grace anasema amejifunza mengi katika safari yake ya kuachwa na mzazi mwenzake.

''Ni vizuri kuchunguza vizuri kabla ya kuingia katika mahusiano ya kimapenzi na mtu,kwani nimejifunza sikutumia akili vizuri bali moyo''

'Sikuwahi kutegemea kuishia kwenye haya ambayo nimeyapitia’’niliyopitia mimi ni funzo kubwa nisingetamani mtu mwingine apitie haya.

Haikuwa rahisi kueleweka na kila mtu lakini Grace anasema familia yake ilikuwa naye bega kwa bega kuhakikisha hapotezi uelekeo wa maisha yake hata baada ya kupata changamoto ya kuachwa,hasara za kiuchumi na malezi ya peke yake.

‘’Ni vizuri mtu anapopitia kipindi kigumu cha changamoto za kimaisha,tusimuhukumu bali tutafute kujua kwanini?huenda tutawaokoa wengi ambao wameishia kukata tamaa na kushindwa kuinuka tena kutokana na aibu,kutojisamehe au hata kutojitambua.’’

Kuhusu kunyooshewa vidole ni jambo ambalo haliepukiki katika jamii.Ni vizuri jamii ikajifunza kufahamu jambo kabla ya kunyoosha kidole kwa mtu.

Nimeona wanawake wengi wanatamani ninachokifanya,wapo wanawake ambao huwa ninakutana nao ninawapatia elimu na kuwatia moyo kuhusu ufugaji.

Kwa kuwa zipo fursa nyingi katika ufugaji kama vile kuandaa vyakula vya mifugo,nimetumia muda wangu wa ziada kuwaonesha wanawake wenzangu fursa zilizopo katika kuandaa vyakula vya mifugo.

Grace anasema bado hajatosheka anasafari ndefu ya kukuza kazi yake hiyo kutoka kuku alionao sasa 11,000 hadi kufikia 50,0000.

‘’Nimegundua watu wengi wana uoga wa kuthubutu.Wanawaza kufanya mambo ya tija lakini wanaogopa kuchukua hatua jambo ambalo linawarudisha nyuma’’hakuna kitu kinachokuja kirahisi anaongeza Grace.

Anajivunia nini?

Kuweza kujitambua tena na kusimama kwa mara nyingine kichumi,nikihudumia watoto wangu mwenyewe kwani baba yao hatuna mawasiliano tena.

Ninajisikia vizuri kwani nimeweza kuinuka tena na kupigania ndoto yangu hii ambayo imeniwezesha kuajiri watanzania wenzangu kadhaa. Ninafurahi kwa kuweza kulisha familia chache kupitia ufugaji huu.

Kuleta mtazamo chanya kwenye sekta ya ndege wafugwao.Ninashukuru kwa hatua hizi ambazo nimezianza kuzungumza na watu mbalimbali wakiwemo watoto vijana na wanawake wenzangu.

Grace anasema kwa mfano kwa elimu ya Tanzania imemuwezesha kuangalia uwezo wake uko kwenye nini,na siyo kusubiri ajira aliyosomea.

Ameongeza kwamba kwa kuwa bado Afrika ina fursa nyingi za kujiajiri vijana wa kiafrika hawana budi kuacha uoga kutumia elimu yao kuibua fursa na kutengeneza ajira.

‘’Miaka kadhaa ijayo ninajua nitakuwa nimekua,ninajiona nikistaafu na kuwa na mradi mkubwa sana wa kuku utakaogusa maisha ya wanawake wengi na vijana wanaochipukia.’’anaeleza Grace

Grace anaeleza kwamba Kuna faida kubwa kumfundisha mtoto katika umri mdogo hasa shughuli hizi za kilimo na ufugaji.

Wengi wetu tunalaani jembe tukidhani ni adhabu lakini ni nyenzo kuu ya kutupatia utajiri,anasisitiza Grace.

Imehaririwa na Leonard Mubali