Kerala: Mji uliotelekezwa katika nchi yenye watu wengi zaidi duniani

India

Chanzo cha picha, ARUN CHANDRA BOSE

Wakati India ikiipita China kama taifa lenye watu wengi zaidi duniani, kuna mzozo wa idadi ya watu katika sehemu za nchi hiyo ambapo uzazi umeshuka chini ya viwango na uhamiaji umesababisha kutelekezwa kwa miji ambayo sasa inakaliwa na wazee. Mwandishi wa BBC Soutik Biswas amesafiri hadi Kumbanad, katika jimbo la Kerala mji ambao unakabiliwa na matokeo ya jamii inayozeeka.

Kwa miaka mingi, shule katika mji uliotulia huko Kerala zimekuwa zikikabiliwa na tatizo lisilo la kawaida: wanafunzi ni wachache na walimu wanapaswa kwenda kuwatafuta. Pia walimu wanalazimika kulipa pesa kutoka mifukoni mwao ili kuleta wanafunzi shuleni.

Shule ya msingi ya serikali yenye umri wa miaka 150 - ambayo inasomesha wanafunzi hadi umri wa miaka 14 - huko Kumbanad ina wanafunzi 50 kwenye orodha yake, kutoka takribani wanafuzi 700 idadi iliyokuwepo hadi mwishoni mwa miaka ya 1980. Wengi wao wanatoka katika familia maskini na maskini wanaoishi pembezoni mwa mji. Likiwa na wanafunzi saba pekee, darasa la saba ndilo darasa kubwa zaidi. Mnamo 2016, darasa lilikuwa na mwanafunzi mmoja tu.

Kupata wanafunzi wa kutosha shuleni ni changamoto. Kila mwalimu kati ya walimu wa wanane wa shule hiyo hulipa rupia 2,800 sawa na $34 kwa mwezi kulipia nauli za usafiri wa bajaji zinazosafirisha wanafunzi kutoka nyumbani hadi shuleni kwenda na kurudi.

Pia wanaenda nyumba kwa nyumba kutafuta wanafunzi. Hata shule chache za binafsi katika eneo hilo zinatuma walimu kutafuta wanafunzi - shule yenye wanafunzi wengi zaidi ni ile yenye wanafunzi 70 tu.

Katika alasiri moja hivi majuzi katika shule ya msingi, hukuna kusikia hekaheka za masomo na kelele za sauti zinazounda mandhari ya shule yenye shughuli nyingi.

Badala yake, walimu walifundisha watoto wachache katika madarasa yenye giza, tulivu. Nje, katika uliokuwa unapigwa, wanafunzi wachache walikuwa wakizungukazunguka huku na kule.

India

Chanzo cha picha, ARUN CHANDRA BOSE

"Tutafanya nini? Hakuna watoto katika mji huu. Ninamaanisha, hakuna watu wanaoishi hapa," Jayadevi R, mkuu wa shule, alisema kwa hasira.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Yuko sahihi. Kumbanad iko katikati mwa wilaya ya Pathanamthitta ya Kerala ambapo idadi ya watu inapungua na na waliokuwepo wanazeeka. Hii katika nchi ambayo asilimia 47% ya watu wako chini ya umri wa miaka 25; na theluthi mbili walizaliwa baada ya India kukomboa uchumi wake mapema katika miaka ya 1990.

Kumbanad na vijiji vingine karibu nusu dazeni vinavyoizunguka ni makazi ya watu wapatao 25,000. Karibu asilimia 15% ya nyumba 11,118 hapa zimefungwa kwa sababu wamiliki wamehama au kuishi na watoto wao nje ya nchi, anasema Asha CJ, Chifu wa halmashauri ya kijiji. Kuna shule 20, lakini wanafunzi wachache sana.

Hospitali moja, zahanati inayoendeshwa na serikali, zaidi ya vituo 30 vya uchunguzi na nyumba tatu za wazee ni vielelezo tosha juu ya idadi ya watu wanaozeeka. Zaidi ya dazeni mbili za benki - ikiwa ni pamoja na matawi manane ndani ya chini ya nusu kilomita - zinagombea fedha kutoka kwa watu wa mijini wanaoishi na kufanya kazi kote ulimwenguni.

Takriban asilimia 10% ya $100bn katika fedha zinazotumwa India kutoka kwa Wahindi wanaoishi nje ya nchi mwaka jana zilikuja Kerala.

Familia za wachache huhakikisha kwamba watoto wao wanasoma vizuri. Hii inasababisha vijana wengi kuhamia maeneo mengine ndani na nje ya nchi kutafuta fursa, wakiwaacha wazazi wao nyumbani.

"Elimu huwafanya watoto kutamani kazi na maisha bora, na wanahama," alisema KS James wa Taasisi ya Kimataifa ya Sayansi ya Idadi ya Watu yenye makao yake Mumbai.

"Maeneo yao ya asili yanakaliwa na wazazi wao wazee, wengi wao wakiishi peke yao."

India

Chanzo cha picha, ARUN CHANDRA BOSE

Akiwa ndani kwenye mlango wa chuma katika nyumba yake ya vigae nyekundu ya ghorofa mbili huko Kumbaud, Annamma Jacob, 74, amekuwa akiishi peke yake kwa muda mrefu.

Mumewe, mhandisi wa mitambo katika kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali, aliaga dunia mapema miaka ya 1980. Mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 50 amekuwa akiishi na kufanya kazi Abu Dhabi kwa zaidi ya miongo miwili. Binti yake anaishi maili chache, lakini mumewe binti huyo amekuwa akifanya kazi kama mhandisi wa programu huko Dubai kwa miongo mitatu.

Majirani zake hawapo: mmoja alifunga nyumba yake na kuwapeleka wazazi wake Bahrain, ambako alikuwa akifanya kazi kama nesi; mwingine alihamia Dubai na kupangisha nyumba yake kwa wenza wazee.

Hii ndiyo picha ya namna hali ilivyo na ujirani wa upweke.

"Ni maisha ya upweke sana. Pia sina afya njema," Bi Jacob alisema.

Licha ya ugonjwa wa moyo na asma, Bi Jacob amekuwa akisafiri nje ya nchi mara kadhaa kumtembelea mwanawe na wajukuu zake, na amewahi kwenda mapumzikoni Jordan, Abu Dhabi, Dubai na Israel akiwa na watoto wake.

India

Chanzo cha picha, ARUN CHANDRA BOSE

Nilimuuliza kwa nini alijenga nyumba kubwa yenye vyumba 12 ili kuishi peke yake. "Kila mtu anajenga nyumba kubwa hapa," alitabasamu. "Ni kuhusu hadhi."

Anatumia muda mwingi katika shamba lake ambako analima ndizi, tangawizi, viazi vikuu na mazao mengine. Nyakati nyingine, yeye hutafakari na kusoma magazeti. Ana mbwa anayeitwa Diana kwenye banda nje.

"Siku nyingine, mimi huzungumza na Diana tu. Ananielewa."

Umbali mfupi na anapoishi bibi huyu, Chacko Mammen, ambaye ana ugonjwa wa moyo na kisukari, anafanya kazi katika shamba lake dogo kwa saa nne kila siku, akilima ndizi.

Mzee huyu mwenye umri wa miaka 64 alifanya kazi nchini Oman kwa miongo mitatu kama mtu wa masoko kabla ya kurejea nyumbani. Alifunga biashara yake ya duka ndogo baada ya miaka sita kwa sababu hakupata watu wa kutosha wa kumsaidia kufanya kazi. Sasa, baada ya juhudi nyingi, analima na kuuza takriban kilo 10 za ndizi kila siku kutoka shambani mwake.

"Siwezi kumudu mfanyakazi," alisema.

Wakati mzee huyu akisema hawezi kumudu kulipa wafanyakazi, Bi Jacob yeye anasema hapendi kuajiri mhamiaji hofu ya usalama wake.

"Naishi peke yangu. Je wakiniua?" alisema.

India

Chanzo cha picha, ARUN CHANDRA BOSE

Katika mji huu tulivu wa wazee na nyumba zilizofungwa, kuna uhalifu mdogo sana.

Polisi wanasema matukio ya wizi ni machache sana kwa sababu watu hawaweki pesa nyingi na vitu vya thamani nyumbani. Hawakumbuki ni lini mara ya mwisho mauaji yalifanyika hapa.

"Hali ni ya amani sana. Tunapata tu malalamiko kuhusu kudanganya. Wazee kulaghaiwa na jamaa zao au wasaidizi wa nyumbani ambao hughushi saini zao na kutoa pesa zao benki," alisema Sajeesh Kumar V, mkaguzi mkuu wa kituo cha polisi cha eneo hilo.

Kwa sababu hakuna matukio ya uhalifu kunamaanisha kuwa polisi hutumia muda mwingi kuwaangalia tu wazee. Huwatembelea kwa mara wazee wasio na waume na wagonjwa; na wamekuwa wakiwapa vifaa vya kengele katika baadhi ya nyumba zao ili waweze kuwatahadharisha majirani wakati wa dharura.

Mnamo 2020, polisi walivunja mlango wa nyumba wakati hakuna mtu aliyejibu kengele ya mlango na kumpata mkazi, mwanamke mzee, amelala sakafuni.

"Tulimpeleka hospitalini, ambako alipata nafuu, Moja ya kazi zetu pia ni kuhamishia wakazi hadi kwenye nyumba za wazee. Tunawafuatilia wazee, tunawapeleka kwa madaktari," Bw Kumar alisema.

India

Chanzo cha picha, ARUN CHANDRA BOSE

"Uzee ndio tatizo pekee hapa," alisema Padre Thomas John, ambaye anaendesha kituo cha kuhudumia wazee kiafya huko Kumbanad.

Mji una nyumba tatu za wazee zinazoweza kufikiwa kwa viti vya magurudumu na nafasi kiasi ya wazi, milango mipana na barabara pana. Alexander Marthoma Memorial Geriatric Centre, jengo la orofa tano kando ya hospitali yenye vitanda 150, hutunza zaidi ya wazee 100, wenye umri wa kati ya miaka 85 na 101. Karibu wote wamelazwa, na familia zao hulipa rupia 50,000 kila mwezi kwa ajili ya utunzaji wao. Wakati mwingine watoto huja na kukaa nao katika kituo kilichojengwa miaka 16 iliyopita.

"Watoto wengi wanaishi nje ya nchi na hawana chaguo zaidi ya kuwahamisha wazazi wazee na kuwapeleka kwenye makazi ya wazee," alisema Padre John.

Wazee wanaougua, nyumba za wazee, uhaba wa vibarua, vijana kuhama mji, vyote huchangia kwa idadi ya watu kupungua, miji kutelekezwa.

"Hii ni simulizi ya mabadiliko yoyote ya idadi ya watu. Mwishowe hii itakuwa simulizi ya India nzima," alisema Bw James.