"Tunaweza kuishi bila misaada" - Msigwa

Chanzo cha picha, Msigwa
Baada ya ongezeko la wasiwasi kuhusu mustakabali wa msaada wa kimataifa kufuatia matukio ya Oktoba 29, msemaji wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa, ametolea ufafanuzi uhusiano wa Tanzania na wahisani, akisisitiza kuwa nchi inaweza kuendelea kusimama kwa miguu yake bila misaada, ingawa amekiri kupungua kwake huzua mtikisiko.
Katika mahojiano yake na mwandishi wa habari Edwin Odemba, Msigwa alieleza kuwa asilimia kubwa ya bajeti ya taifa inatokana na makusanyo ya ndani, hivyo misimamamo ya baadhi ya wahisani haitaiangusha Tanzania. "Mwaka huu bajeti yetu ni shilingi trilioni 56, kati ya hizo, trilioni 40 zinatokana na makusanyo yetu wenyewe. Misaada katika bajeti ni trilioni 1.07 tu," alisema.
Kwa mujibu wake, mikopo inayochangia shilingi trilioni 14 katika bajeti ni fedha ambazo "tunachukua na tunalipa", tofauti na misaada ambayo huweza kukatwa au kucheleweshwa kwa misingi ya kisiasa au kidiplomasia.
Alisisitiza kuwa takwimu hizo zinaonyesha nchi haitong'ang'ania msaada ili kuendelea kufanya kazi zake. "Ukiangalia hizi takwimu unaona hatuwezi kushindwa. Kama trilioni 55 ni za kwetu, tutakwama wapi?"
Hata hivyo, Msigwa hakupuuza umuhimu wa misaada na ushirikiano na wadau hao. Alisema ingawa Tanzania inaweza kuendesha bajeti yake kwa ndani, misaada husaidia kuharakisha maendeleo na kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi. "Ni kweli tunahitaji misaada, ni muhimu. Lakini si kwamba bila wao nchi hii hawezi kusonga," alifafanua.
Aidha, alizungumza kwa uwazi juu ya athari zinazoletwa na kupungua kwa misaada, akibainisha kuwa hata upungufu wa trilioni moja tu unaweza kuathiri mipango ya mwaka. "Ukisema inapungua trilioni moja, tayari kuna mtikisiko. Ni lazima kama nchi tuketi na kujipanga, tukae mkao wa kula kuona namna tutakavyoendelea na kile tulicho nacho."
Kauli hizi zinakuja wakati mjadala mpana unafukuta kuhusu uhusiano wa Tanzania na jumuiya ya kimataifa, huku Bunge la Ulaya tayari likipendekeza kusitishwa kwa zaidi ya euro milioni 156 za ufadhili wa 2026 chini ya mpango wa NDICI–Global Europe. Hatua hiyo imezua taharuki miongoni mwa wachambuzi wa uchumi, wanaosema pengo hilo linaweza kuathiri miradi ya kijamii na miundombinu.
Msigwa, hata hivyo, alisisitiza kwamba serikali inaendelea kujenga hoja na kufanya majadiliano na wadau wa kimataifa ili kuhakikisha uhusiano na ushirikiano unaendelea kwa manufaa ya pande zote. Alitumia nafasi hiyo kutetea msimamo wa serikali kwamba maamuzi ya ndani ya Tanzania hayapaswi kuendeshwa na shinikizo la nje.















