Je, Tanzania kutengwa kidiplomasia?

Chanzo cha picha, Samia Suluhu Hassan
Baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, mjadala kuhusu mustakabali wa Tanzania katika diplomasia ya kimataifa umeongezeka kwa kasi ambayo haijazoeleka katika miaka ya karibuni. Taarifa za kukamatwa kwa raia, madai ya kupotea kwa watu, matumizi ya nguvu kupita kiasi na mauaji yaliyotajwa na mashirika ya ndani na nje yamefungua ukurasa mpya wa mizozo ya kidiplomasia.
Ndani ya muda mfupi, nchi 16 za Ulaya zilitoa tamko la pamoja zikihimiza kuchukuliwa kwa hatua za haraka, huku Marekani ikitangaza kuwa inatathmini upya uhusiano wake na Tanzania. Umoja wa Mataifa (UN), Jumuiya ya Madola, Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pia zimeelekeza macho yao nchini humo kuhusu mwenendo wa uchaguzi na matukio yaliyoufuata.
Huu ni mwendelezo wa kile wachambuzi wanakieleza kama "presha ya kawaida ya kimataifa", lakini kwa Tanzania kiwango kilichoonekana safari hii kinaelezwa kuwa kikubwa zaidi kuliko ilivyozoeleka.
Kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyotoa jijini Dar es Salaam mbele ya wazee wa jiji imeongeza mjadala huo. Akirejea wakosoaji wa kimataifa, alihoji: "Nje huko wanakaa ooh Tanzania ifanye hivi, ifanye vile… who are you (nyie ni kina nani)? Wanadhani bado ni masters (watawala) wetu?"
Historia ndefu ya misuguano ya kidiplomasia

Chanzo cha picha, Getty Images
Sera za Ujamaa na Azimio la Arusha (1967) zilisababisha ubinafsishaji wa benki, viwanda, na makampuni makubwa, jambo lililofanya uhusiano wa kidiploasia hasa na baadhi ya nchi za Magharibi kuyumba hasa katika miaka ya 1960s' na 1970's. Hata hivyo, aina ya mizozo ya kidiplomasia wakati huo mpaka mwanzoni mwa miaka 1990's haikugusa sana eneo la haki za binadamu na kiraia zinazopiganiwa sana leo, kama ya kuishi, kujieleza, demokrasia na maandamano.
Wachambuzi wanaona kuwa hali ya sasa haijatokea ghafla. Katika kipindi cha utawala wa Rais hayati John Magufuli (2015-2021), Tanzania ilipitia sintofahamu kubwa na mataifa ya magharibi kuhusu masuala ya demokrasia, uhuru wa vyombo vya habari na nafasi ya mashirika ya kiraia. Baadhi ya wafadhili walipunguza misaada na serikali ikaelekeza nguvu katika kutegemea mapato ya ndani.
Utawala wa Rais Samia ulipoingia madarakani mwaka 2021, kulikuwa na ishara ya kurejea kwenye diplomasia laini; baadhi ya vikwazo visivyo rasmi vilipungua na uwekezaji ukarudi. Lakini uchaguzi wa 2025 umeifanya hali irejee kwenye ukinzani uliodhaniwa kuwa umeanza kupungua.
Kwa mujibu wa mchambuzi Mohamed Issa, matamko ya mataifa ya magharibi hayapaswi kuonekana kama matusi ya kisiasa, bali kama ukumbusho wa wajibu wa kimataifa.
"Matamko yana nguvu. Ni sehemu ya mikataba ambayo Tanzania imesaini kuhusu haki za binadamu, demokrasia, haki ya kutoa maoni na kuandamana," anasema.
Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kuwa tofauti haiko tu katika ukosoaji, bali katika namna Tanzania inavyojibu. Kauli kama "who are you?" zinatafsiriwa na baadhi kama kusisitiza uhuru wa taifa, lakini kwa wengine, ni ishara ya mwelekeo mpya wa msimamo mkali unaoweza kuongeza mvutano wa kidiplomasia.
Historia ya mataifa yaliyowahi kutengwa, na jinsi yalivyotoka

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika siasa za kimataifa, hakuna jipya kuhusu mataifa kukosolewa au kupoteza baadhi ya fursa za misaada kutokana na masuala ya uchaguzi. Ukiacha Urusi, Iran, China, Myanmar, Kora Kaskazini, Venezuela na zingine, nchi za kiafrika kama Zimbabwe, Ethiopia na Uganda zote zimepitia misuguano kama hiyo miaka ya karibuni.
Zimbabwe ilikabiliwa na vikwazo vizito baada ya kukosolewa kuhusu mazingira ya uchaguzi na haki za upinzani. Uchumi uliporomoka, lakini hatua ya kufungua milango kwa mazungumzo mapya na wahisani ilisaidia kupunguza shinikizo.
Ethiopia ilikumbwa na taharuki kimataifa baada ya vita vya Tigray. Misaada na makubaliano ya kibiashara yalipunguzwa kwa kiasi kikubwa, lakini hali ilianza kutengamaa baada ya kusaini makubaliano ya amani na kuruhusu uchunguzi wa kimataifa.
Uganda, baada ya kupitisha sheria kali kuhusu mapenzi ya jinsia moja, ilipoteza sehemu ya misaada ya sekta za kijamii na ikalazimika kutafuta ushirikiano zaidi na nchi za BRICS (Muungano wa nchi zinazokua kiuchumi) na washirika wake ikiwemo China na India.
Kwa Tanzania, wachambuzi wanaona njia tatu zinazoelekea mbele: Mazungumzo mapana na jumuiya ya kimataifa, kurejesha uwazi wa ndani kupitia tume huru ya uchunguzi, na kuegemea zaidi washirika mbadala kama China, India, Urusi, Brazil, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Iran.
Lakini wengi wanaonya kuwa njia ya tatu, ingawa inaweza kupunguza shinikizo la muda mfupi, inaweza kuathiri sekta zinazotegemea ushirikiano wa magharibi kama utalii na uwekezaji wa moja kwa moja.
Katika mjadala mpana kuhusu iwapo Tanzania inaweza kuhimili bila wahisani, Mohamed Issa anataja mifano ya mataifa ya Sahel. "Nchi inaweza kuishi bila wahisani… mfano Burkina Faso na Mali, ambazo zimeamua kutosikiliza Benki ya Dunia wala IMF. Lakini wananchi lazima wafunge mkanda," anasema.
Mtazamo huo unashabihiana na ule wa mchambuzi Ezekiel Kamwaga, ambaye aliandika kwenye mtandao wake wa X: "Ni muhimu kushughulikia matatizo yetu ya ndani, lakini ili tuwe salama zaidi tunahitaji kutafuta namna ya kutengeneza mkataba wa usalama wa pamoja na nchi za China na Urusi."
Hofu iliyoenea zaidi miongoni mwa wachambuzi ni kwamba hatari kubwa si suala la usalama na kupungua kwa misaada pekee, bali kupotea kwa uungwaji mkono wa kimataifa, hali inayoweza kuiweka Tanzania katika nafasi ya upweke wa kidiplomasia.
Msimamo wa Serikali ya Tanzania

Chanzo cha picha, URT
Serikali imesisitiza kuwa masuala ya ndani yanapaswa kuachwa yashughulikiwe na mifumo ya ndani. Kupitia taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje, serikali ilieleza kuwa Tume ya Uchunguzi iliyoanzishwa na Rais Samia ndiyo msingi wa kupata ukweli kuhusu matukio ya uchaguzi.
Hata hivyo, baadhi ya jumuiya za kimataifa zimeeleza wasiwasi juu ya uhuru wa tume hiyo, jambo ambalo limefanya matarajio ya kupungua kwa shinikizo yaonekane kuwa madogo.
Mnamo Novemba 28, 2025, serikali ilikutana na mabalozi wa mataifa 16 pamoja na mambo mengige kutaarifiwa kuhusu yaliyotokea wakati wa uchaguzi. Mchambuzi Godwin Gonde anasema licha ya kukaa na Serikali, hatua ya mabalozi kutoa tamko sasa kama kundi moja ina uzito mkubwa, kwamba 'hatukubaliani".
Ndani ya Tanzania, baadhi ya wachambuzi kama Kamwaga wanashauri kufikiria mkondo wa tatu wa ushirikiano wa kiusalama na mataifa yasiyoweka masharti ya kisiasa, ingawa wazo hilo linaendelea kuibua maswali kuhusu hatma ya haki zinazoonekana kuminywa sasa.
Kwa sasa, uwezekano wa Tanzania kukabiliwa na kutengwa kidiplomasia unaonekana kuwa mkubwa kuliko miaka ya karibuni. Lakini hatua hizo si hatima isiyoweza kubadilishwa. Na wala si mwisho taifa hilo, Burkina Faso japo mdau wake mkubwa kimaendeleo ni Ufaransa, ina miaka miwili sasa inapambana kujiongoza bila mkono wa ufaransa, iliyoitawala kwa miaongo mingi.
Wachambuzi wanaamini Tanzania inaweza kupunguza mvutano ikiwa itachagua dira ya diplomasia ya uwazi, mazungumzo ya moja kwa moja na wahisani, na mifumo ya uchunguzi yenye uaminifu wa kimataifa.
Njia yoyote nyingine inaweza kuimarisha msimamo wa ndani wa taifa kama taifa lisilotetereka, imara na lisiloingiliwa mambo yake, lakini ina hatari ya kuliweka katika upweke wa kimataifa hali ambayo madhara yake yanaweza kuonekana kwa muda mrefu kiuchumi na kijamii.















