Maandamano Tanzania: Balozi 16 za nchi za magharibi zataka uchunguzi huru wa matukio ya Octoba 29

Bendera
Muda wa kusoma: Dakika 4

Balozi 16 za nchi za magharibi zimetoa wito kwa Serikali ya Tanzania kufuatia ripoti za ukiukwaji mkubwa na wa mfumo wa haki za binadamu baada ya uchaguzi mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025.

Ripoti hizo zinajumuisha tuhuma za mauaji ya kiholela ya mamia ya watu, kutekwa nyara kwa nguvu, na kuwekwa kizuizini kiholela kwa maelfu hususan waandamanaji, viongozi wa upinzani na wanaharakati wa kiraia katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Walisisitiza kwamba Serikali ya Tanzania ina wajibu wa kutoa taarifa ya kina kuhusu hatima na mahali waliko watu wote waliotekwa nyara.

''Ukamataji watu kiholela na ufichaji wa mili ya waliopoteza maisha. Tunatoa wito kwa mamlaka husika kukabidhi mili ya marehemu kwa familia zao haraka iwezekanavyo, kuwaachia huru wafungwa wote wa kisiasa na kuhakikisha waliokamatwa wanapata misaada ya kisheria na matibabu''

''Zaidi, tunatoa wito kwa serikali kushughulikia mapendekezo yaliyotolewa katika ripoti za awali za waangalizi wa uchaguzi wa AU na SADC ambazo ziliweka bayana mapungufu yaliyojiri wakati wa mchakato wa uchaguzi''.

Unaweza kusoma

Aidha, walitaka serikali kuondoa mara moja vikwazo vyote vinavyokwamisha uhuru wa vyombo vya habari, wakisema vikwazo hivyo vinakiuka wajibu wa kimataifa wa Tanzania chini ya mikataba ya haki za binadamu.

''Tunatambua azma ya serikali ya kudumisha amani na utulivu wa nchi, na tunasisitiza umuhimu wa vyombo vya ulinzi kutekeleza majukumu yao''.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, uchaguzi ulifanyika katika mazingira yenye mashaka ya muda mrefu, ikiwemo kukamatwa kwa viongozi wa upinzani bila utaratibu wa kisheria, kutoweka kwa baadhi yao kwa kulazimishwa, na mabadiliko ya kisheria yaliyopunguza uadilifu wa mfumo wa uchaguzi.

Viongozi wa vyama viwili vikuu vya upinzani walizuiwa au kuenguliwa kugombea, na wengine waliwekwa kizuizini au kupotezwa kabla ya siku ya kupiga kura.

Balozi hizo zimeitaka Serikali pamoja na vyombo vya usalama kuhakikisha kulindwa kwa haki ya wananchi kukusanyika kwa amani, hasa kuelekea maandamano yaliyopangwa kufanyika tarehe 9 Desemba 2025.

Walionya kuwa hatua yoyote itakayokiuka haki hiyo inaweza kuongeza mgogoro wa kibinadamu na kisiasa.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamesema wako tayari kutoa msaada wa kiufundi kwa Serikali ya Tanzania ili kusaidia kurejesha mazingira ya kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.

Marekani kutathmini upya uhusiano wake na Tanzania

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hapo jana, Marekani ilisema kuwa inatathimini upya uhusiano wake na Tanzania kufuatia mauaji ya raia wengi wakati wa uchaguzi mkuu wa hivi karibuni.

Taarifa iliotolewa na ubalozi wa Marekani, ilisema kuwa licha ya uhusiano wake wa muda mrefu uliostawi kati yake na taifa hilo, hatua ya hivi karibuni ya taifa hilo imezua wasiwasi mkubwa kuhusu mwelekeo wa uhusiano huo.

Imesema kwamba matukio yanayoendelea kufanywa na serikali ya Tanzania ya kukandamiza uhuru wa dini na uhuru wa kujieleza , kuwepo kwa vikwazo vya mara kwa mara dhidi ya uwekezaji wa Marekani na ukatili dhidi ya raia kabla na baada ya uchaguzi ni mambo inalolifanya taifa hilo kutathmini upya uhusiano huo.

Taarifa hiyo ilisema kwamba vitendo hivyo vinawaweka raia wa Marekani , watalii na maslahi ya Marekani nchini tanzania hatarini na kutishia kudhoofisha ustawi na usalama wa pamoja ambao umekuwa alama ya ushirikiano wetu kwa miongo kadhaa.

Imeongezea kwamba Marekani haiwezi kufumbia macho 'vitendo vinavyohatarisha usalama wa raia wetu, au usalama na utulivu wa kanda'

Rais samia awanyooshea kidole 'mabeberu'

Katika mkutano uliofanyika Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wazee kutoka maeneo mbalimbali ya jiji hilo, Rais Samia Suluhu Hassan alitoa hotuba yenye uzito wa kisiasa ambayo imeibua mjadala mkali ndani na nje ya nchi.

Moja ya sehemu kali zaidi za hotuba hiyo ni pale Rais alipolenga mataifa ya nje, akisema yamekuwa yakitoa maagizo kuhusu jinsi Tanzania inavyopaswa kuendesha mambo yake. Alisema Tanzania haiwezi kukubali kudhibitiwa au kuwekewa masharti kwa kisingizio cha misaada au ushirikiano.

"Nje huko wanakaa ooh Tanzania ifanye hivi, ifanye vile… (wao kina nani) who are you? Wanadhani wao bado ni masters (watawala) wetu?" alihoji.

Alisisitiza kuwa baadhi ya mashinikizo ya kimataifa yanatokana na tamaa ya kutaka kufaidika na rasilimali za Tanzania, hususan madini adimu ambayo nchi inamiliki.

Kwa mujibu wake, Tanzania imekuwa ikilengwa kwa sababu ya utajiri wake wa kiasili, na iwapo wazawa hawatakuwa waangalifu, rasilimali hizo zinaweza kuwa chanzo cha migogoro ya kisiasa.

"Maumbile yetu na utajiri wetu isiwe laana tukauana sisi kwa sisi kwa kushawishiwa na wanaotolea macho nchi yetu," alisema.

Kwa msisitizo mkali, Rais aliwataka Watanzania kushikamana na kutoacha tofauti za kisiasa au ushawishi kutoka nje kuigawa nchi. Alisisitiza kuwa hakuna taifa linaloweza kujiendesha kwa amani kama raia wake wanatoa mwanya kwa nguvu za nje kuingilia mambo yao ya ndani.