Ajuza wa miaka 70 aolewa na mvulana wa miaka 16

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Ndoa isiyo ya kawaida imefanyika nchini Indonesia - mwanamke mwenye umri wa miaka 70 kaolewa na mvulana wa miaka 16. Ndoa hii lilidhihirika baada ya video ya harusi yao kusambaa mitandaoni.
Kwa mujibu wa sheria ya ndoa ya nchi hiyo, ndoa za utotoni haziruhusiwi, lakini wanandoa hao walisema wangejiua ikiwa hawataruhusiwa kuoana, ndio maana mamlaka ya kijiji iliidhinisha ndoa yao lakini haikusajiliwa kwenye daftari la serikali.
Kulingana na sheria ya Indonesia, umri wa chini wa kuolewa kwa wasichana ni miaka 16 na umri wa chini kwa wavulana ni 19.
Mapenzi yao yalianzaje?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kulingana na vyombo vya habari vya eneo hilo, watu hao wawili walianza ukaribu wakati mwanamke huyo mzee alipochukua jukumu la kumtunza mvulana huyo aliyekuwa akiugua malaria.
Sik Ani, mkuu wa kijiji katika kisiwa cha kusini cha Sumatra nchini Indonesia, ameliambia shirika la habari la AFP, ''kutokana na umri mdogo wa mvulana huyo, tuliruhusu ndoa hiyo isiandikishwe.''
Pia alisema ndoa hii ilifanyika tarehe 2 Julai ili kuzuia vitendo vya kuvunja sheria. Jina la mvulana huyo ni Salamat huku mkewe Rohaya mwenye umri kati ya miaka 71 na 75.
Inasemekana babake wa mvulana huyo alifariki miaka mingi iliyopita na kisha mama yake kuolewa tena na mwanaume mwingine.
Hii ni ndoa ya tatu ya Rohaya, na ana watoto wengi kutoka ndoa hizo mbili kabla ya mvulana huyo wa miaka 16 kumuoa.
Yenni Izzi, mfanyakazi wa kijamii katika kituo cha wanawake huko Palembang, anayefanya kampeni dhidi ya ndoa za utotoni, aliiambia BBC, ndoa hiyo haikuwa ya kawaida.
Anasema, "mvulana hakuchukua uamuzi wa kufunga ndoa kwa sababu yoyote ya kifedha au ya kimwili, lakini Rohaya alikuwa akimtunza na kumpa upendo."
Mamlaka zinasemaje?

Chanzo cha picha, Getty Images
Viongozi wa serikali za mitaa wameeleza kusikitishwa na suala hili lakini bado haijabainika iwapo hatua zitachukuliwa au la.
Gazeti la Jakarta Post likimnukuu Waziri wa Masuala ya Kijamii wa Indonesia, Khofifah Indar Parwansa anasema, ''haiwezekani kwake kutoa kibali cha ndoa hiyo, kwani mvulana huyo ni mdogo.''
Nalo Gazeti la Sriwijaya Post lilimnukuu gavana wa Sumatra Kusini akisema, ''kwa kawaida, wasichana huolewa wakiwa na umri mdogo, lakini sina la kusema kuhusu ndoa hii kwa sasa."
Indonesia ni nchi yenye Waislamu wengi duniani, ina takriban watu milioni 229, na asilimia 87% ni Waislamu.












