Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mkuu wa jeshi la Hamas aliuawa katika shambulizi la Julai, Israel yasema
Tom Bennett
BBC News
Jeshi la Israel linasema lilimuua mkuu wa jeshi la Hamas Mohammed Deif katika shambulio la anga huko Gaza tarehe 13 Julai.
Deif alilengwa katika shambulio la Israeli kwenye boma katika eneo la Khan Younis.
Jeshi la Israel wakati huo lilisema kuwa kamanda mwingine wa Hamas, Rafa'a Salemeh, aliuawa katika shambulio hilo , lakini lilisema halina uthibitisho wa mwisho juu ya hatima ya Deif.
Jeshi la Israel linasema kuwa limethibitisha kuwa mkuu wa jeshi la Hamas Mohammed Deif aliuawa katika shambulio la anga katika Ukanda wa Gaza mwezi uliopita.
Israel inasema Deif alikuwa mmoja wa watu waliohusika na kupanga mashambulizi ya Oktoba 7 kusini mwa Israel ambapo watu 1,200 waliuawa.
Tangazo la Israel linakuja siku moja baada ya kuuawa kwa kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismael Haniyeh, aliyeuawa mjini Tehran, na kamanda mkuu wa Hezbollah Fuad Shukr, ambaye aliuawa katika shambulio la anga la Israel katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut.
Taarifa kutoka kwa jeshi la Israel ilisema kuwa "kufuatia tathmini ya kijasusi, inaweza kuthibitishwa kuwa Mohammed Deif aliuawa" katika shambulio la Julai 13.
Mamlaka ya afya ya Gaza inayosimamiwa na Hamas ilisema wakati huo kwamba mashambulizi ya anga yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 90, lakini ikakana kuwa Deif alikuwa miongoni mwa waliofariki.
Mohammed Deif alikuwa mkuu wa Brigedi ya Izzedine al-Qassam, kitengo cha kijeshi cha kundi la Hamas.
Alifungwa gerezani na mamlaka za Israel mwaka 1989, ambapo baada ya hapo alianzisha Brigedi hiyo kwa lengo la kuwakamata wanajeshi wa Israel.
Israel ilimshutumu kwa kupanga na kusimamia mashambulizi ya mabasi yaliyoua makumi ya Waisraeli mwaka 1996, na kuhusika katika kuwakamata na kuwaua wanajeshi watatu wa Israel katikati ya miaka ya 1990.
Anajulikana pia kusaidia katika kufanikisha ujenzi wa mahandaki ambayo yamewaruhusu wapiganaji wa Hamas kuingia ndani ya Israeli kutoka Gaza.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah