Waridi wa BBC: Maisha ya uyatima utotoni yalinifanya niwahudumie watoto njiti

Mariam Joseph Mwakabungu anapenda kufahamika kama 'Mama Njiti'

Chanzo cha picha, Doris Foundation

    • Author, Martha Saranga
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Tanzania
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

‘’Mume wangu alinipa ruhusa bila kinyongo kukumbatia watoto njiti, tena hatua hii ni kwa sababu anafahamu namna ninavyopenda watoto,’’ Mariam Mwakabungu anaieleza BBC

Kwake Mariam anasema hajaona changamoto kwa sababu naye ni mzazi. “Hawa watoto ninawalea kama watoto wangu, nilikuwa nimejitolea kuwasaidia na ndiyo lengo langu kuu siku zote,” anasema.

Mwanamke huyo anasema kwa mara ya kwanza alifika katika hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam kumuona rafiki yake aliyekuwa amejifungua Watoto njiti, au pre mature kwa lugha ya Kiingereza.

‘’Katika wodi ile nilimuona muuguzi aliyevalia sare za kazi akiwa anambembeleza mtoto njiti aliyekuwa akilia nikamuuliza kuhusu mtoto yule aliyekuwa akilia sana, akanijibu kuwa mtoto yule alimpoteza mama yake, ’’anasema Mariam.

Muuguzi aliniuliza unaweza? Mariam anasema kuwa hata hakuwaza mara mbili alimijibu anaweza licha ya kutojua jinsi kazi hiyo ilikuwa ikifanywa.

Anasema: Mimi mwenyewe nilipoteza wazazi nikiwa mdogo sana, ninayajua maisha ya yatima yalivyo ninawahurumia sana.

Mariam mwenye umri wa miaka 26 ni mkazi wa jiji la Dar es Salaam, anasema haikumsumbua kujitolea muda na nguvu zake kuwakumbatia watoto njiti maarufu kama Kangaroo hususan waliotupwa ama kutelekezwa na mama zao katika hopitali ya Amana jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, anaeleza kuwa alilelewa na bibi yake baada ya kupoteza wazazi wake wote wawili.

Aacha kazi ya mama lishe na kuwa mama njiti

Mariam anayependa kufahamika kama Mama njiti anasema hakusita kuacha kazi yake ya mama lishe ili awakumbatie watoto njiti katika hospitali ya Amana.

‘’Mimi ni mama lishe, nilisitisha shughuli zangu ili nikakumbatie watoto njiti’’

Je, ana elimu na ujuzi kuhusu kukumbatia watoto njiti?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Anaeleza: Elimu yangu niliishia kidato cha pili baada ya bibi kushindwa kumudu gharama za kunisomesha. Ni kwamba hakuwa na elimu yoyote kuhusu utunzaji wa watoto njiti lakini baada ya hospitali ya Amana kumuhoji taarifa zake ikiwemo kupata kibali kutoka kwa mumewe alipigiwa simu ili kufika hospitalini hapo ili kukamilisha taratibu kabla ya kuanza kujitolea kukumbatia watoto njiti.

Anasema, mojawapo ya utaratibu uliofanyika ni kujiridhisha kuhusu afya yake kwa kufanya vipimo.

‘’Walinipima damu kitaalamu wanaita ‘full blood picture’ ambacho kiliangalia kama nina maradhi yanayoweza kuambukiza kwa njia ya hewa au kugusana, nashukuru nilikuwa vizuri kiafya”

Aliowakumbatia wakua vyema

Anasema hadi sasa watoto watatu aliowakumbatia wanakaribia kufikisha umri wa mwaka mmoja na wanaendelea na afya njema. ‘’Huwa nawafuatilia, ’’anaeleza Mariam kwa kujiamini.

Jamii inakuchukuliaje?

‘’Bibi yangu ananiombea niendelee kuwa na moyo huu japo watu walinishangaa kwamba nawezaje kuacha kazi zangu na kujitolea kukumbatia watoto njiti”, anaeleza.

‘’Uamuzi wangu ulipokewa kwa hisia mbalimbali wapo walionishangaa lakini wengine hunipongeza,” anasimulia.

unaweza pia kusoma

Atambuliwa na Rais Samia

Watu binafsi na taasisi mbalimbali wamekuwa wakinitafuta na kunipongeza kwa zawadi,fedha na ujumbe wa kunitia moyo

Chanzo cha picha, Doris Foundation

‘’Nilijiskia vizuri Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan naye aliponizawadia pesa kiasi cha shilingi milioni mbili baada ya vyombo vya habari kutangaza taarifa kuhusu kukumbatia watoto njiti waliotupwa na kutelekezwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa, Amana.

Anasema serikali ya Tanzania ilimpa ajira ya mkataba. ‘’Watu binafsi na hata taasisi mbalimbali zilinitafuta na kunipa pongezi mbalimbali ikiwemo fedha na hata ujumbe wa kunitia moyo,’’ anasema na kuongeza kuwa taasisi moja ya kiraia imempa zawadi ya nyumba.

Kuhusu kujiendeleza kielimu

‘’Nina mipango ya kujiendeleza kielimu lakini mwaka huu nilishindwa kutokana na kujifungua mtoto wangu wa tatu,ninasubiri akue kidogo.”

Pia anasema anatamani kumiliki kituo kikubwa cha utoaji huduma ya malezi kwa watoto njiti wanaotelekezwa au kutupwa.

Anasema suala la kujitolea kwa wahitaji ni jambo zuri, kuliko kukaa bila shughuli yoyote.

Ushirikiano wa mumewe

Mariam anasema familia yake imekuwa ikimuunga mkono na kumfurahia jambo ambalo linampa hamasa kuendelea na kujitolea. ‘’Mume wangu alinipa ruhusa bila kinyongo, anafahamu namna ninavyopenda watoto,” anafafanua.

Anasema anapokuwa kazini, mdogo wake wa kike humsaidia kuwahudumia watoto wake.

Mariam akiwa na mumewe na bibi yake

Chanzo cha picha, Doris Foundation

Kangaroo ama kukumbatia watoto njiti ni nini hasa?

“Kukumbatia watoto maarufu kama Kangaroo ilitokana na mfano wa mnyama Kangaroo ambaye hukumbatia mtoto wake kifuani wanakua,’’ anaeleza Mariam Machemba, afisa muuguzi katika kitengo cha watoto wachanga waliozaliwa kabla ya wakati katika hospitali ya rufaa Amana ya mkoa wa Dar es Salaam”.

Je ni watoto wa uzito gani huwahudumia?

Anasema kuwa huduma ya kukumbatia watoto njiti huwalenga watoto wenye uzito pungufu, kama vile chini ya kilo mbili na nusu.

Anasema mara nyingi watoto ambão hawana wazazi kutokana na kuachwa au kutelekezwa huwa wanakuwa wengi hapa Amana.

Anasema, yule mtoto wa kwanza Mariam alianza kumkumbatia alikuwa na gramu 900 baada ya wiki mbili yule mtoto alifikisha gramu 1500 yaani kilo moja na nusu.

Je, vigezo gani vilizingatiwa kwa Mariam?

Mariam anatamani kumiliki kituo kikubwa cha utoaji huduma ya malezi kwa watoto njiti wanaotelekezwa au kutupwa nchini Tanzania

Chanzo cha picha, Doris Foundation

Machemba anaeleza kwamba wito wa kufanya kazi hii ni kigezo mojawapo lakini ni lazima taratibu muhimu za kuzingatiwa kwa mtoa huduma zifanyike hususan vipimo vya kiafya.

‘’Tulizingatia kwamba Mariam hakuwa na elimu ya utoaji wa huduma hii, baada ya vipimo vya afya kuturidhisha kuwa yuko salama tulimfunza namna ya kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi’’

Mbali ya kuwakumbatia majukumu yake mengine wodini hapo ni kukoroga maziwa kwani watoto njiti hupewa maziwa ya kopo na kutoa taarifa ikiwa atabaini tatizo kwa mtoto.

Ripoti ya 2023 ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF iliarifu kwamba Kusini mwa Asia na Kusini mwa Jangwa la Sahara kuna viwango vya juu zaidi vya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati, na watoto hao wanakabiliwa na hatari kubwa ya vifo.

Maeneo haya mawili yanachangia zaidi ya asilimia 65 ya watoto wanaozaliwa njiti kote duniani.

Unaweza pia kusoma

Imehaririwa na Alfred Lasteck na Florian Kaijage