Wanasoka 10 waliong'ara duniani mwaka 2025

Muda wa kusoma: Dakika 4

Mwaka mwingine wa 2025 umemalizika na kuanza mwaka mpya wa 2026....lakini mwaka 2025 umekuwa mwaka mzuri kwa wanasoka wengi wa soka. Ukiacha mchezaji kama Declan Rice ambaye ameanza msimu huu mpya vizuri, makala hii inaangalia wachezaji waliofanya vyema katika kalenda nzima ya mwaka kuanzia Januari mpaka Disemba 2025.

Kutoka kwa vipaji vipya vinavyopaa hadi wachezaji wenye uzoefu kuonyesha bado wako kileleni, BBC Sport inachambua baadhi ya wanasoka bora wa kiume katika mchezo wa soka katika miezi 12 iliyopita.

Harry Kane (Bayern Munich)

Nahodha wa England amekuwa katika kiwango chake bora cha maisha yake ya soka kwa mwaka 2025, akiendelea kupachika mabao akiwa na Bayern Munich.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Spurs, mwenye umri wa miaka 32, amefunga mabao 60 kwa klabu yake na taifa mwaka 2025.

Hata hivyo, bado mabao hayo haifikii rekodi ya mabao mengi zaidi katika mwaka mmoja, ambayo Lionel Messi aliiweka aalipofunga mabao 91 mwaka 2012.

Lamine Yamal (Barcelona)

Lamine Yamal ana umri wa miaka 18 tu, lakini amekuwa akijulikana kwa muda mrefu kutokana na kiwango chake cha kushangaza.

Alikuwa bora akiwa na timu ya taifa la Hispania waliposhinda Euro 2024 mwaka na mwaka uliopita, ameendelea kufanya vyema.

Mchezaji huyu mdogo amefunga mabao 7 na kutoa pasi za bao 8 kwenye michezo 14 ya La Liga kwa Barcelona msimu huu.

Nusu ya kwanza ya mwaka huu, ameshafunga mabao 11 na kutoa pasi za bao 10 kwa klabu na timu ya taifa.

Ousmane Dembele (Paris St-Germain)

Ousmane Dembele alianza mwaka 2025 kwa kiwango cha ajabu, akiwa amefunga mabao 15 katika michezo yake 8 ya kwanza, akiimalizia kampeni ya 2024-25 akiwa na mabao 35 katika michezo 53, kiwango bora kabisa katika maisha yake ya soka.

Mchezaji huyu mwenye miaka 28 alipata tuzo ya kwanza ya Ballon d'Or kutokana na kiwango chake bora uwanjani, na ingawa mabao hayajaendelea kupatikana kama alivyoanza mwaka, bado mwaka 2025 umeonekana wa kushangaza kwake.

Erling Haaland (Man City)

Ni mtu jasiri sana asiyemchagua Erling Haaland kama kapteni katika timu yake ya Fantasy Premier League, kwa sababu mshambuliaji huyu wa Manchester City, mwenye umri wa miaka 25, amekuwa wa kushangaza mbele ya goli msimu huu.

Amefunga mabao 25 katika michezo 24 tu huku pia akiwa na kiwango sawa cha ajabu na kuisaidia Norway kufuzu kombe la dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998, akiwa amefunga mabao 16 katika michezo 8 ya kufuzu.

Cole Palmer (Chelsea)

Msimu huu umekuwa mgumu kwa Cole Palmer kutokana na majeraha kupunguza muda wake wa kucheza, lakini alikuwa mchezaji wa kuangazia katika Kombe la dunia la klabu msimu wa joto na alikuwa mchezaji muhimu kwa Chelsea msimu uliopita.

Aliwasaidia Blues kurudi katika Ligi ya Mabingwa, kutoa pasi muhimu 2 katika ushindi wa Chelsea dhidi ya Real Betis katika fainali ya UEFA Conference league na kisha akawa mchezaji bora wa mashindano ya dunia ya klabu, akiwapiku baadhi ya timu na wachezaji wakubwa zaidi wa soka duniani.

Palmer, mwenye miaka 23, alifunga mabao 3 na kutoa pasi 2 za mabao, huku hakuna mchezaji mwingine aliyemzidi kwa mchango wa mabao 5.

Nuno Mendes (Paris St-Germain)

Kwa kuwa PSG walishinda makombe matatu mwaka 2025, wachezaji wa klabu hiyo kuwepo kwenye orodha hii haikwepeki, mmoja wapo ni Mendes.

Mabao na pasi za mabao mara nyingi hutawala vichwa vya habari, lakini Nuno Mendes mwenye umri wa miaka 23 amejiweka kama mmoja wa mabeki wa kushoto bora zaidi duniani kwa kiwango chake bora mwaka uliopiwa akiwa na PSG.

Gianluigi Donnarumma (Paris St-Germain/Man City)

Kipa Gianluigi Donnarumma, aliyesajiliwa Manchester City kutoka PSG msimu wa joto, alitwaa tuzo ya FIFA ya kipa bora wa mwaka 2025.

Mchezaji huyu wa taifa la Italia alitambuliwa kwa mwaka wa kipekee ambapo alishinda Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza na vikombe vitatu vya ndani akiwa na PSG.

Miezi michache baadaye, amejijenga kama sehemu muhimu ya timu ya Pep Guardiola Man City, ambayo kwa sasa iko nafasi ya pili katika msimamo wa ligi kuu ya England na ya nne Ligi ya Mabingwa.

Pedri (Barcelona)

Pedri, mwenye miaka 23, ambaye alifurahia msimu bora kabisa wa taaluma yake mwaka 2024-25 akiwa msaada mkubwa kwa Barcelona kushinda makombe matatu ya ndani, sasa anachukuliwa kuwa mmoja wa wachezaji bora wa nafasi ya kiungo duniani.

Alikuwa na idadi kubwa ya kupora mipira (254) kati ya wachezaji wa ligi tano bora za Ulaya msimu uliopita na pia alionyesha kuwa ni mchezaji bora wa kutengeneza nafasi za mabao akitengeneza nafasi 70 kwa wachezaji wenzake wa Barcelona.

Kwa kuwa matatizo ya majeraha yamepita, sasa anaendelea kuwa sehemu muhimu ya Barcelona msimu huu na amesaidia klabu hiyo kuwa kileleni La Liga, mbele ya wapinzani wao Real Madrid.

Kylian Mbappe (Real Madrid)

Mwaka 2025 umekuwa mwaka wa mafanikio kwa Kylian Mbappe, mfaransa aliyefunga mabao 59 katika mashindano yote akiwa na Real Madrid.

Hii inamaanisha mshambuliaji huyo mwenye miaka 27 amefungana rekodi ya idadi ya mabao katika mwaka mmoja ambayo Cristiano Ronaldo aliweka mwaka 2013.

Vitinha (Paris St-Germain)

Kwa kuwa nafasi ya kiungo wa kati wa kujihami haiwezi kutajwa sana kama washambuliaji, mchezaji wa nafasi hiyo lazima awe wa kipekee ili kuweza kuzingatiwa na kutajwa kama mchezaji bora zaidi duniani. Vitinha, mwenye miaka 25, hakika amekuwa na mwaka wa kipekee sana, mwaka 2025.

Ikilinganishwa na kiungo maarufu wa zamani wa Barcelona, Andres Iniesta, Vitinha ana mbinu bora na nafasi sahihi ya kucheza ambayo inamwezesha kutawala mechi kutoka katikati ya uwanja akiwa na PSG.