Matumaini na mashaka: Mashariki ya Kati ikisubiri kurejea kwa Trump

    • Author, Frank Gardner
    • Nafasi, BBC News World
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Wakati viongozi wa mataifa kadhaa ya Kiarabu na Kiislamu wakikusanyika katika mji mkuu wa Saudia kwa mkutano wa kilele, kuna swali juu ya muhula wa pili wa Trump kwa eneo hilo.

Kinyume kabisa na hofu iliyopo barani Ulaya kuhusu kutotabirika kwa Donald Trump, nchi za Kiarabu za Ghuba zinamwona kama nguvu ya utulivu.

Katika makala yake ndani ya Arab News, mfanyabiashara mashuhuri wa UAE, Khalaf al-Habtoor anasema: "Mashariki ya Kati ambako usalama ni muhimu, mtazamo wa Trump wa kuimarisha miungano na kuzuia vikundi vya itikadi kali – ni mtazamo mzuri."

Hapa Saudi Arabia, Trump anatazamwa vyema zaidi kuliko Joe Biden.

Trump alikwenda Riyadh kwa safari yake yake ya kwanza nje ya nchi kama Rais mwaka 2017, wazo linaloelezwa ni kutoka kwa Rupert Murdoch.

Kupitia mkwe wake Jared Kushner, Trump anafurahia mahusiano mazuri na mtawala wa Saudia, Mwanamfalme Mohammed bin Salman. Mwanamfalme huyo hajawahi kusamehe au kumsahau Biden pale aliposema Saudi Arabia inapaswa kutengwa kwa kukiuka haki za binadamu.

Pia unaweza kusoma

Trump na Mashariki ya Kati

Sera za Trump juu ya Mashariki ya Kati ni za mchanganyiko.

Kwa upande mmoja aliifurahisha Israel na kuuvuruga ulimwengu wa Kiarabu kwa kuutambua mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel na vile vile kulitambua eneo la Milima ya Golan linalokaliwa kimabavu kuwa ni la Israel.

Lakini kwa upande mwingine, aliwezesha Makubaliano ya Abraham mwaka 2020 ambayo yalishuhudia UAE, Bahrain na Morocco zikianzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia na Israel na Sudan pia ikafanya hivyo.

Lakini mwaka 2018, aliiondoa Marekani katika mapatano ya nyuklia na Iran. Akiuita ni “mkataba mbaya zaidi katika historia. Maoni hayo yaliakisi maoni ya serikali nyingi za eneo hilo, kwamba makubaliano hayo, yenye lengo la kuizuia Iran kuwa na silaha za nyuklia, yalishindwa kuizuia Iran kuwa na makombora ya balistiki ya Iran, huku ikilifanya jeshi la Walinzi wa Mapinduzi kuwa na fedha ambazo zilitumika kufadhili wanamgambo katika eneo hilo.

Mwaka 2020, kuikasirisha Iran lakini kuyafurahisha mataifa ya Ghuba ya Kiarabu, Trump aliamuru kuuawa kwa Qasem Soleimani, kiongozi wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi cha Quds.

Lakini Mashariki ya Kati ya leo si sawa na ile ya wakati Trump anaondoka Ikulu ya White House.

Israel iko vitani na Hamas na Hezbollah, pia ikashambuliana na kundi la Wahouthi nchini Yemen na Iran yenyewe.

Chini ya utawala wa Biden ushawishi wa Marekani katika eneo hilo unaonekana kupungua huku Ikulu ya White House kwa kiasi kikubwa ikishindwa kumzuia mshirika wake wa karibu, Israel, kusimamisha vita huko Gaza na Lebanon.

Kurudi kwa Trump

Kurudi kwa Trump katika Ikulu ya White House kunaelezwa kuwa kutaipa Israel uhuru zaidi wa kulenga nchini Iran - kama vile mafuta na maeneo ya nyuklia - ambayo utawala wa Biden ulisema haiwezi kufanya hivyo.

"Uungaji mkono wake kwa Israel na msimamo mkali dhidi ya juhudi za Iran - ulimfanya kuwa mshirika mkuu katika eneo hilo, na kurejea kwake madarakani kunatarajiwa kuongeza juhudi za kupunguza ushawishi wa Iran," afisa wa zamani wa kijasusi wa Israel, Joshua Steinrich anasema.

Lakini kuna kitu kimebadilika katika eneo hilo. China, Saudi Arabia na Iran zimekubali kuweka kando tofauti zao, na kumaliza uhasama wa miaka saba, uliochangiwa zaidi na vita vya Yemen ambapo jeshi la anga la Saudi liliwashambulia kwa mabomu waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran.

Siku ya Jumapili, mkuu wa jeshi la Saudi Arabia alisafiri kwa ndege hadi Tehran kukutana na mwenzake wa Iran, na nchi zote mbili sasa zinazungumza juu ya kuimarisha ushirikiano wao katika ulinzi na usalama.

Tangu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mwaka 1979, Saudi Arabia na majirani zake wa Kiarabu wa Kisunni katika eneo hilo wamekuwa wakiitazama Iran kuwa tishio kubwa kwa usalama wao.

Lakini shambulio la kushangaza la ndege zisizo na rubani mwaka 2019 dhidi ya vituo vya mafuta vya Saudia, lililohusishwa na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran nchini Iraq, ni ukumbusho mbaya kwa mataifa ya Ghuba ya Kiarabu kuhusu jinsi yalivyo hatarini kushambuliwa na Iran.

Pamoja na mkutano wa kilele wa nchi za Kiarabu na Kiislamu unaotaka kukomeshwa vita huko Gaza na Lebanon, kuna matumaini na mashaka juu ya kipi kitaokea katika muhula wa pili wa urais wa Trump kwa Mashariki ya Kati.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi