Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
"Je, Iran Imebadilisha mstari wake mwekundu Mashariki ya Kati?"
Leo, katika mapitio ya magazeti yetu, tunapitia makala kutoka Jerusalem Post ambayo inazungumzia mabadiliko ya mistari myekundu ya Iran katika Mashariki ya Kati, na kuibua suala la mzozo juu ya ukanda wa Zangezur na uhusiano kati ya Iran, Armenia, Azerbaijan na pande nyingine.
Tunasoma makala katika gazeti la Guardian kuhusu chaguzi za Hezbollah na jinsi chaguzi hizi zitakavyoamua hatima ya Lebanon.
Tunahitimisha kwa makala kutoka gazeti la Asharq Al-Awsat, ambapo mwandishi anauliza swali kuhusu jinsi idara ya kijasusi ya Israel ilivyoshughulikia tukio la tarehe 7 Oktoba.
Iran na Suala la Ukanda wa Zangezur
Tunaanza kuangazia Jerusalem Post, ambapo mtafiti wa Mashariki ya Kati Mordechai Kedar aliandika makala ambayo alishangaa ikiwa Iran imebadilisha mistari yake myekundu katika Mashariki ya Kati.
Mwandishi alitoa mfano wa suala la Azerbaijan, Armenia na ukanda wa Zangezur kati ya nchi hizo mbili kama mfano wa mistari hii.
Mwandishi anashangaa kuhusu siri ya kushughulishwa kwa Iran na ukanda wa Zangezur na uungaji mkono wa hivi karibuni wa Urusi “katika wakati ambapo Tehran inajikuta ikikabiliwa na mapigo yanayoongezeka katika eneo la Mashariki ya Kati, na katika wakati ambapo Israel inapigana dhidi ya Hezbollah huko Lebanon. Hamas na Islamic Jihad huko Gaza, na hata Houthis huko Yemen''.
Mwandishi anarejelea hapa ukanda wa Zangezur unaounganisha Azabajani na Jamhuri ya Nakhchivan inayojiendesha. Ukanda huo utairuhusu Azerbaijan kuungana moja kwa moja na Uturuki bila kupitia Armenia.
Ukanda huo ulielezewa na Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev kuwa "unaounganisha ulimwengu wa Kituruki." Iran inapinga ujenzi wa ushoroba huu, ambao unapitia jimbo la Syunik la Armenia, eneo ambalo liko moja kwa moja kwenye mpaka na Iran.
Mwandishi huyo anasema kwamba sehemu kubwa ya ukanda huo "haiathiri Iran hata kidogo" na kwamba "ukanda huo, ambao Urusi imeidhinisha hivi karibuni, unatarajiwa kuwa chini ya usimamizi na udhibiti wa Urusi."
Kedar anaongeza kuwa kwa miongo kadhaa, "Vikosi vya Urusi vimekuwa kwenye mpaka wa Iran na Armenia, na uwepo huu wa Urusi haujasumbua Iran hata kidogo."
Mwandishi anakisia sababu halisi ya Iran kuuchukia ukanda huo wakati ambapo inakabiliwa na "changamoto nyingi katika Mashariki ya Kati," akisema kwamba ukanda huo "unaweza kuwa kisingizio tu cha Iran kuelezea chuki yake dhidi ya Urusi juu ya masuala ambayohakuna uhusiano wowote na eneo la Caucasus."
Azerbaijan, ambayo ina Washia wengi, kwa muda mrefu imekuwa "mwiba kwa Iran," anasema Kedar, "ikikataa tafsiri ya kimsingi ya Tehran ya Uislamu na badala yake kushirikiana na Israeli."
Mwandishi anaongeza kuwa kwa muda mrefu imekuwa ikifadhaisha kwa Iran kwamba imeweza "kupanua ushawishi wake huko Baghdad, Damascus, Sanaa na Beirut, lakini sio Baku," mji mkuu wa Azerbaijan.
Kisha anabainisha kuwa hivyo ndivyo ilivyo licha ya ukweli kwamba "Iran ina Waazeri wengi miongoni mwa wakazi wake, na kwamba rais wa Iran mwenyewe ni Muazeri."
Kedar anasema kwamba sababu ya upinzani wa Iran kwa ukanda wa Zangezur inaweza kuwa inahusiana na "mstari mwekundu uliochorwa na Tehran kuhusu jaribio lake la kudumisha udhibiti katika eneo hilo, wakati ambapo Armenia inasonga karibu na Magharibi ," ambapo mwandishi baadaye anadokeza kwa kusema kwamba Armenia "itakuwa na chaguo bora zaidi la kibiashara, ikiwa ukanda utawekwa kama sehemu ya makubaliano."
Mwandishi anaongeza kuwa Azerbaijan "inafurahia ushirikiano wa kimkakati na Israeli, adui mkuu wa Iran, na Uturuki na Urusi zote zinaongezeka katika eneo hilo.
Katika mazingira haya yote, Iran inapoteza! ndiyo maana inapinga ukanda wa Zangezur.”
Njia panda ya Hezbollah
Katika gazeti la The Guardian la Uingereza, mwandishi Bilal Saab anauliza swali na kulijibu kupitia kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.
Saab anaanza makala yake kwa kuuliza: "Je, Lebanon inawezaje kushughulikia uhusiano wake wenye matatizo na usio na tija na Hezbollah bila kurejea kwenye mzozo wa ndani wa kimadhehebu?"
Saab anajibu swali kwa niaba ya Netanyahu, akimnukuu: “Walebanon lazima kwanza waikomboe Lebanon kutoka kwa Hezbollah. Una nafasi ya kuokoa Lebanon kabla haijaanguka kwenye dimbwi la vita virefu ambavyo vitaleta uharibifu na mateso, kama tunavyoona huko Gaza.
Netanyahu, Saab anasema, "ambaye anakana mashtaka ya uhalifu wa kivita ya ICC, anatishia waziwazi kutumia mbinu za kijeshi za uharibifu alizotumia huko Gaza dhidi ya Walebanon."
Mwandishi anaongeza kwamba ikiwa Netanyahu angetaka kweli kuwasaidia Walebanon kukabiliana na Hizbollah, "hangeamuru jeshi lake kuivamia kusini mwa Lebanon, kwa sababu hilo lingeifufua Hezbollah na kuipa uhai mpya."
"Netanyahu anaijua historia vizuri, lakini anachagua kuipuuza," Saab anasema: Hezbollah ilizaliwa kwa sehemu ili kupinga uvamizi wa Israel kusini mwa Lebanon kati ya mwaka 1982 na 2000.
Lakini Saab alirejea kusema kwamba matamshi ya Netanyahu, ambayo aliyataja kuwa "matupu," hayabadili ukweli kwamba "Hezbollah imekuwa mzigo mzito kwa Lebanon tangu 2000."
"Kwa miongo kadhaa, chama kilisisitiza kuwa ndicho pekee kinacholinda Lebanon dhidi ya uvamizi wa Israel," Saab anasema. "Kujiondoa kwa Israeli kutoka Lebanon miaka 24 iliyopita kuliimarisha dai hilo."
Lakini tangu Israel ilipoondoka Lebanon, "Jukumu la kijeshi la Hezbollah limekuwa si la ufanisi wala halali. Imeshindwa kuzuia mashambulizi ya Israel, na hatua zake zimetoa mwanya wa uhasama wa Israel, kama mwaka 2006 na kama ilivyo sasa.
Mwandishi anaongeza kuwa jukumu na ushawishi wa Hezbollah haukuwa kazi yake yenyewe. "Kwa miaka mingi, kimefurahia uungwaji mkono wa kisiasa na kijeshi kutoka Iran na Syria.
"Miaka kumi na saba baada ya vita vya 2006, ni wazi kwamba Hezbollah haijajifunza lolote," Saab anasema.
Saab anaibua kitendawili kwamba chama "kimechagua njia inayokileta karibu na kujiangamiza," na analinganisha na Netanyahu, ambaye "amechagua kupuuza ukweli." Lakini mwandishi anaendelea kusema kwamba "ni ujinga kudhani kwamba mabadiliko ya Hezbollah kuwa chama cha kisiasa na ujumuishaji wa vikosi vyake katika jeshi la Lebanon kutaondoa vitisho vya Israel."
Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Seif Abdalla