Mambo matatu yanayoweza kufanya mpango wa kusitisha mapigano Gaza kufanikiwa

Muda wa kusoma: Dakika 4

Muhtasari wa mpango wa kusitisha mapigano na kuachiliwa kwa mateka wa Gaza unaojadiliwa hivi sasa na Israel na Hamas katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja huko Doha umekuwa mezani tangu Mei.

Kwa hivyo kwa nini kuna matarajio mapya kwamba unaweza kufanya kazi, baada ya kusimama kwa miezi minane ya vita?

Kuna mambo kadhaa ambayo yamebadilika, kisiasa na kwenye maeneo ya mapigano.

Kwanza ni kuchaguliwa kwa Donald Trump kuwa rais ajaye wa Marekani.

Ametishia kuchukua hatua kali ikiwa mateka hawataachiliwa kabla ya kuchukua madaraka Januari 20.

Hamas wanaweza kuliona hilo kama ishara kwamba hatua ndogondogo ambazo utawala wa Biden ulitumia kujaribu kudhibiti serikali ya Israeli zitaondolewa, ingawa ni ngumu kufikiria nini inaweza kumaanisha kwa eneo ambalo tayari limeharibiwa na miezi 15 ya vita. .

Israel pia inahisi shinikizo kutoka kwa rais ajaye kumaliza mzozo huko Gaza, ambao unatishia kuingilia kati matumaini ya Trump kupata makubaliano mapana ya kikanda, na taswira yake kama rais anayemaliza vita.

Kwa upande mwingine, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anakabiliwa na shinikizo linaloendelea kutoka kwa washirika wake wa mrengo mkali wa kulia ili kuendeleza vita.

Lakini Trump pia anaweza kuwa nyenzo kwake katika kuwashawishi washirika wake kukubaliana na mpango huo na kusalia serikalini; rais mpya wa Marekani na mtu aliyemchagua kuwa balozi wa Israel wanaonekana kuunga mkono makazi ya Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, ambao Waziri wa Fedha wa mrengo wa kulia wa Israel, Bezalel Smotrich, amesema anataka kunyakua.

Lakini baada ya mkutano na waziri mkuu jana usiku, Smotrich alionekana kutoshawishika, akiandika kwenye mitandao ya kijamii kwamba makubaliano ya sasa ni "janga" kwa usalama wa taifa la Israeli na kwamba hataunga mkono.

Baadhi ya Waisraeli, ingawa, wanaamini kuwa Smotrich na mshirika wake wa mrengo mkali wa kulia, Waziri wa Usalama wa Kitaifa Itamar Ben-Gvir, wanaona jukumu lao la sasa katika serikali ya Israeli kama fursa yao bora ya kuudhibiti Ukingo wa Magharibi.

Jambo la pili ambalo limebadilika ni kuongezeka kwa shinikizo kwa Netanyahu kutoka kwa taasisi yake ya kijeshi.

Takwimu muhimu zinaripotiwa kwa kiasi kikubwa kumpinga mara kwa mara juu ya kupungua kwa malengo ya kijeshi katika kuendeleza vita, baada ya kuuawa kwa uongozi wa juu wa Hamas, na kuharibiwa kwa Gaza.

Wiki iliyopita, wanajeshi 10 wa Israel waliuawa huko Gaza, wakiangazia upya gharama za vita kwa Israeli, na juu ya swali la kudumu la kama "ushindi kamili" dhidi ya Hamas ambao Netanyahu ameahidi unaweza kufikiwa.

Baadhi ya wachambuzi sasa wanadokeza kuwa Hamas inajijenga upya kwa kasi zaidi kuliko Israel inavyoishinda, na kwa hivyo Israel inapaswa kutafakari upya mkakati wake.

Na kuna badiliko la tatu la kikanda, linalochangia mabadiliko ya matarajio hapa pia: kudhoofika na mmomonyoko wa washirika wa Hamas katika "mhimili wa upinzani" wa Iran, kutoka Hezbollah huko Lebanon hadi Bashar al-Assad huko Syria, pamoja na mauaji ya kiongozi wa Hamas. Yahya Sinwar huko Gaza.

Kwa sababu hizi zote, sasa inaonekana kama nafasi nzuri zaidi katika miezi kadhaa ya kuziba mapengo kati ya Israel na Hamas na kukomesha vita.

Kile ambacho hakijabadilika katika kipindi cha miezi minane tangu wafanye mazungumzo mara ya mwisho ni mapengo kati yao.

Miongoni mwao ni mzozo wa moja kwa moja kati ya Hamas, ambayo inataka kumaliza vita, na ile ya Israel, ambayo inataka kuweka mlango wazi wa kuanzisha tena mzozo huo, iwe kwa sababu za kisiasa au za kijeshi.

Makubaliano hayo, kama yalivyoainishwa na Rais Joe Biden mwezi Mei, yamegawanyika katika awamu tatu, huku usitishaji vita wa kudumu unaanza kutekelezwa katika awamu ya pili.

Mafanikio sasa yatategemea kama dhamana inaweza kupatikana ili kuondoa hofu ya Hamas kwamba Israeli itajiondoa kwenye mpango huo baada ya awamu ya kwanza ya kutolewa kwa mateka.

Maswali kuhusu jinsi ya kusimamia eneo ambalo Israeli inajiondoa pia hayako wazi katika hatua hii.

Lakini mtandao wa diplomasia unaovuka eneo hilo kwa muda wa wiki moja iliyopita, na ukweli kwamba Netanyahu ametuma wakuu wa mashirika ya usalama ya Israel kwenye mazungumzo ya Doha, pamoja na mshauri mkuu wa kisiasa, ni ishara za kutia moyo.

Ndivyo ilivyo pia kuondoka Doha kwa mratibu wa wafungwa wa Kipalestina, Qadoura Fares.

Mkataba huu wa zamani unachochea matumaini mapya kwa kiasi fulani kwa sababu mazungumzo yanafanyika katika muktadha mpya wa kikanda, na shinikizo zinazoongezeka ndani na kutoka kwa washirika wakuu nje ya nchi.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga