Maandamano Tanzania: Shughuli zarejea leo, ulinzi ukiimarishwa

s
Maelezo ya picha, Hapa ni Moshi, Kilimanjaro shughuli zinaendelea kama kawaida
Muda wa kusoma: Dakika 2

Shughuli za kila siku zimeanza kurejea katika maeneo mengi ya Tanzania, baada ya tahadhari iliyotolewa kufuatia wito wa maandamano uliopangwa kufanyika Desemba 9.

Kupitia mitandao ya kijamii, baadhi ya vijana maarufu wa kizazi cha Gen Z walihamasiana kushiriki maandamano yaliyoitishwa yasiyo na kikomo kudai mabadiliko ya kisiasa, ikiwemo katiba mpya, demokrasia, haki za binadamu, na mapendekezo ya kurejea kwa uchaguzi uliompa ushindi Rais Samia Suluhu Hassan kwa asilimia 97. Hata hivyo, Serikali imesema maandamano hayo ni haramu na hayaruhusiwi.

Polisi Tanzania wameonyesha kuwa hali ya usalama nchini ni shwari, huku hatua za ulinzi zikiwa zimeimarishwa kuhakikisha usalama na utulivu. Huku Serikali ikiwataka wananchi kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

"Hali hii (ulinzi) itaendelea na wananchi wawe huru kuendelea kufanya shughuli zao wakati huo huo jeshi la Polisi linaendelea kuchukua jukumu la kuhakikisha wanabaki salama na wanasheherekea sikuu hizi zote mpaka tufike mwaka mpya tutapita salaama", ilikuwa kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri George Simbachawene alipokuwa anaangalia hali jijini Dar es Salaam.

BBC ilifuatilia hali hiyo katika mikoa kadhaa na kuzungumza na wananchi. Thabita Paschal wa Dodoma alisema: "Tumeamka shwari, watu wametoka na wanaendelea na shughuli zao hapa Chamwino Dodoma. Shughuli ziliendelea kama kawaida tangu jana jioni. Nimepumzika hadi baadae mchana ndio nitaingia kazini kwangu."

Mama Jonathan wa Mwanza alisema: "Mume wangu ametoka kwenye shughuli zake na ameniambia baadhi ya shughuli zinaendelea huku wilaya ya Nyamagana. Hapa nyumbani niko shwari."

Juliana Paul, mkazi wa Majumbasita, Dar es Salaam, alisema: "Ninawasiliana na wenzangu, ofisi imefunguliwa, lakini bado baadhi yetu hatujaweza kufika kutokana na changamoto ya usafiri kuelekea Tabata Shule."

Hata mkoa wa Mara, Ayubu Mela wa Tarime, aliiambia BBC kwamba huko hali ni shwari ila wanafanya shughuli zao kwa tahadhari kubwa.

Siku moja kabla ya Desemba 9, Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba aliwaasa wananchi kutumia siku hiyo kwa utulivu na kusherehekea maadhimisho ya Uhuru kwa kutotoka, isipokuwa wale wenye majukumu ya kazi.

Kutokana na athari za maandamano ya Oktoba 29, yaliyosababisha vifo na uharibifu mkubwa wa mali, shughuli za kila siku zilisimama jana Disemba 9, wengi wakichukua tahadhari.