Vita vya Taarifa: Namna akili mnemba inavyotumika wakati wa vita

Muda wa kusoma: Dakika 4

Vita kati ya Iran na Israel vilitokea kwa siku 12, lakini "vita vya taarifa" vinaendelea. Vyombo vya habari na akaunti zinazounga mkono pande zote mbili zilihusika sana katika vita.

Hata kama vita hivi vya kisaikolojia havitabadili moja kwa moja mkondo wa mzozo wenyewe, lakini vinaathiri mtazamo wa umma na uhalisia wa mambo.

Kwa mujibu wa David Miller, afisa wa zamani wa ujasusi na mjumbe wa zamani wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, anasema "wengine wanaamini kwamba hatimaye ni simulizi juu ya vita ndio zinazoshinda, si tu nguvu za kijeshi."

Juni 19, wakati wa vita vya Iran na Israel, tovuti ya "D-New Arab" iliandika katika makala kwamba "ukweli ndio mwathirika wa kwanza wa vita: "Serikali, raia, na watazamaji wa kimataifa kwa pamoja wamenaswa katika wimbi la habari za uwongo na za kupotosha, na akili bandia na habari mpya za uwongo zimeibuka."

"Kwa miaka mingi, serikali na makundi yenye silaha yametumia vyombo vya habari vya kawaida kuchagiza maoni ya umma, kuleta mkanganyiko, kuongeza ari na kuhalalisha vita," imeandika D-NewArab, ambayo makao yake makuu yapo London na inamilikiwa na kampuni ya Qatar Fidat Media. "

Pia unaweza kusoma

Propaganda za Iran

Uchunguzi wa BBC ilihitimisha kwamba wafuasi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walitumia akili bandia kuunda idadi kadhaa ya video ghushi, tatu kati ya hizo zilikuwa na maoni zaidi ya milioni 100 kwenye majukwaa mbalimbali.

Baadhi ya video ghushi za uharibifu wa ndege za kivita za F-35 za Israel zilikuwa nyingi sana, kulingana na Lisa Kaplan, Mkurugenzi Mtendaji wa kikundi cha uchambuzi wa masuala ya usalama cha Altia.

Moja ya video zilizotazamwa zaidi, ni ile iliyotazamwa mara milioni 27, ikionyesha makumi ya makombora yakipiga Tel Aviv, lakini ilikuwa ni video bandia. Video inayoonyesha ndege ya kivita ya F-35 ikianguka, iliyotazamwa zaidi ya milioni 21, ilichukuliwa kutoka katika gemu na kutumwa kwenye mtandao wa kijamii wa TikTok, lakini iliondolewa baada ya BBC kutoa onyo.

Ripoti zinaonyesha kuwa baadhi ya akaunti, kama vile "Daily Army of Iran," imepata ongezeko kubwa la wafuasi, kutoka 700,000 hadi milioni 1.4 katika muda wa chini ya wiki moja, na haina uhusiano wowote na serikali ya Iran.

Emmanuel Seliba wa kikundi cha utafiti cha Get Real anaeleza kwa: "Kwa mara ya kwanza, tunaona matumizi makubwa ya akili bandia wakati wa mzozo wa kijeshi."

Vyombo vya habari vya Iran pia vilichapisha picha iliyodai kuwa imenasa rubani wa Israel anayeitwa Sara Ahronoth, lakini Newsguard, kampuni inayofuatilia habari potofu kwenye vyombo vya habari, iligundua kuwa picha hiyo ilipigwa mwaka 2011 na ilikuwa ya Luteni wa Jeshi la Wanamaji la Chile.

Propaganda za Israel

Kwa upande mwingine, wafuasi wa Israel pia wameweka tena sehemu za zamani za maandamano nchini Iran, wakisingizia kwamba Wairani wanaunga mkono mashambulizi ya Israel; video moja ya uwongo hata ilionyesha watu mjini Tehran wakiimba "Tunaipenda Israel."

Moja ya mifano ya kushangaza zaidi ni shambulio la gereza la Evin; shambulio kweli lilifanyika, lakini taarifa na video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii zilikuwa za uwongo na ni zilkuwa ni sehemu ya ujasusi wa wa Israeli wa kutumia akili bandia kutoa maudhui ghushi. Yakiwa na hastaga Free Evin. Na yalikuwa ni maandalizi ya kisaikolojia kwa mashambulizi ya kweli ya gereza hilo."

Maudhui ya uwongo yaliyochapishwa katika kipindi hiki ni pamoja na picha ghushi za kiongozi wa Irani, waziri mkuu wa Israel, video ya mlipuko wa bandia kwenye Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion, na picha za mabaki ya ndege za Israel na Marekani, ambazo zote zilitoka kwenye vyombo vya habari vya serikali ya Iran.

BBC pia ilitathmini video ya Gereza la Evin na kuhitimisha kuwa picha ya lango la Gereza la Evin iliongezewa mlipuko wa uwongo.

Kwa kawaida, serikali zilizo katika hali ya vita na wakati wa vita hujiona kuwa na haki katika kusimamisha baadhi au uhuru wote wa kijamii na haki za kiraia kwa kisingizio cha "umoja wa kitaifa," "mshikamano wa kitaifa," na usalama wa kitaifa, hapo sasa vyombo hivyo huwa sehemu ya propaganda za serikali.

Kwa ujumla, wataalamu wanaona wimbi hili la propaganda kuwa ni onyo kwa siku zijazo; ambapo vita vitaamuliwa sio tu kwa risasi, lakini pia na machapisho bandia, video za uwongo, na akili bandia.