Uchunguzi huu wa DNA kwenye mifupa ya kale kubadili historia?

Chanzo cha picha, Liverpool John Moores University. Nature
- Author, Pallab Ghosh
- Nafasi, Science Correspondent
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Uchunguzi wa DNA uliofanywa kwenye mfupa wa mwanamume aliyeishi miaka 4,500 iliyopita katika Bonde la Nile, Misri umetoa mwanga mpya kuhusu historia ya kale.
Uchambuzi wa mifupa yake unaonyesha alikuwa na umri wa miaka 60 na huenda alifanya kazi kama mfinyanzi, lakini pia kwamba asilimia ishirini ya DNA yake ilitoka kwa mababu walioishi kilomita 1,500 mbali katika ustaarabu mwingine mkuu wa wakati huo, huko Mesopotamia au Iraq ya sasa.
Huu ni ushahidi wa kwanza wa kibiolojia unaoonyesha uhusiano kati ya maeneo haya mawili na unaweza kusaidia kueleza jinsi Misri ilivyobadilika kutoka makundi mbalimbali ya jamii za wakulima na kuwa mojawapo ya jamii ya watu wenye nguvu zaidi duniani.
Matokeo haya yanaongeza uzito mpya kwa mtazamo unaosema kuwa uandishi na kilimo viliibuka kupitia kubadilishana kwa watu na mawazo kati ya jamii hizi mbili za kale.

Chanzo cha picha, Liverpool John Moores University/Nature
Mtafiti mkuu, Profesa Pontus Skoglund kutoka Taasisi ya Francis Crick jijini London, aliiambia BBC kuwa uwezo wa kutoa na kusoma DNA kutoka kwenye mifupa ya kale unaweza kutoa mwanga mpya juu ya matukio na watu binafsi huko zamani, kuruhusu ukweli wa kihistoria ulioonekana kuwa mweusi na mweupe kujaa maisha na maelezo ya rangi.
"Ikiwa tutapata habari zaidi za DNA na kuziweka sambamba na kile tunachojua kutoka kwa habari za kiikiolojia, kitamaduni, na zilizoandikwa tulizo nazo kutoka wakati huo, itakuwa ya kusisimua sana," alisema.
Uelewa wetu wa zamani zetu unatokana na sehemu na kumbukumbu zilizoandikwa, ambazo mara nyingi ni za matajiri na wenye nguvu. Njia za kibiolojia zinawapa wanahistoria na wanasayansi chombo kipya cha kuona historia kupitia macho ya watu wa kawaida.
DNA ilichukuliwa kutoka mfupa katika sikio la ndani la mabaki ya mwanamume aliyekuwa amezikwa Nuwayrat, kijiji kilicho kilomita 265 kusini mwa Cairo. Alifariki kati ya miaka 4,500 na 4,800 iliyopita, wakati muhimu wa mabadiliko katika kuibuka kwa Misri na Mesopotamia.
Ushahidi wa kiikiolojia ulionyesha kuwa maeneo hayo mawili huenda yalikuwa yanamuingiliano angalau miaka 10,000 iliyopita wakati watu wa Mesopotamia walipoanza kulima na kufuga wanyama, na kusababisha kuibuka kwa jamii ya wakulima.
Wasomi wengi wanaamini kuwa mapinduzi haya ya kijamii na kiteknolojia huenda yaliathiri maendeleo kama hayo katika Misri ya kale , lakini hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja wa mawasiliano au muingiliano, hadi sasa.

Chanzo cha picha, Garstang Museum/Liverpool University/Nature
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Adeline Morez Jacobs, ambaye alichambua mabaki hayo kama sehemu ya masomo ya shahada yake ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Liverpool John Moores, anasema huu ni ushahidi wa kwanza wazi wa uhamiaji mkubwa wa watu kati ya maeneo hayo mawili kwa wakati huo.
"Una maeneo mawili yanayoendeleza mifumo ya kwanza ya uandishi, kwa hivyo wanaikiolojia wanaamini kuwa walikuwa wakiwasiliana na kubadilishana mawazo. Sasa tuna ushahidi kwamba walikuwa hivyo.
Tunatumai kuwa sampuli za DNA za baadaye kutoka Misri ya kale zinaweza kupanua juu ya lini hasa harakati hii kutoka Asia Magharibi ilianza na ukubwa wake."
Mwanamume huyo alizikwa kwenye chungu cha udongo katika kaburi lililochongwa kwenye mlima. Namna Mazishi yake yalivyofanyika huenda iliisaidia DNA yake kuhifadhiwa. Kwa kuchunguza kemikali kwenye meno yake, timu ya utafiti iliweza kubaini alichokula, na kutoka hapo, walifikia maamuzi kuwa huenda alikulia Misri. Lakini simulizi ya upelelezi wa kisayansi haiishii hapo.

Chanzo cha picha, The Metropolitan Museum of Art
Profesa Joel Irish katika Chuo Kikuu cha Liverpool John Moores alifanya uchambuzi wa kina wa mifupa hiyo ili kupata picha kamili ya mwanamume huyo.
"Nilichotaka kufanya ni kujua huyu jamaa alikuwa nani, tujifunze mengi iwezekanavyo kumhusu yeye, umri wake, kimo chake, alichofanya kwa ajili ya riziki na kujaribu kubinafsisha jambo zima badala ya kumchukulia kama sampuli," alisema.
Muundo wa mifupa ulionyesha kuwa mwanamume huyo alikuwa kati ya miaka 45 na 65, ingawa ushahidi mwingine ulionyesha umri wa juu zaidi. Alikuwa na urefu wa futi 5 na inchi 2 tu.
Profesa Irish pia aliweza kubaini kuwa huenda alikuwa mfinyanzi. Mfupa wenye umbo la ndoano nyuma ya fuvu lake ulikuwa umekuzwa, ikionyesha kuwa alikuwa akitazama chini sana. Mifupa yake ya makalio ilikuwa imepanuka, ikipendekeza kwamba alikuwa akiketi kwenye sehemu ngumu kwa muda mrefu. Mikono yake ilionyesha ushahidi wa harakati nyingi za mbele na nyuma, na kulikuwa na alama kwenye mikono yake ambapo misuli yake ilikuwa imekua, ikionyesha kuwa alikuwa amezoea kuinua vitu vizito.
"Hii inaonyesha alifanya kazi kwa bidii sana. Amefanya kazi maisha yake yote," msomi huyo mzaliwa wa Marekani aliiambia BBC. Dk. Linus Girdland Flink alieleza kuwa ilikuwa ni kwa bahati kubwa sana kwamba hiki kilipatikana kwa ajili ya kusoma na kufichua siri kubwa za kihistoria.
"Mifupa ilichimbuliwa mwaka 1902 na kuhifadhiwa katika Makumbusho ya dunia ya Liverpool. Sasa tumeweza kusimulia sehemu ya hadithi ya mtu huyo", alisema















