Mashambulizi ya droni ya Ukraine yatuma ujumbe muhimu kwa Urusi na Magharibi

    • Author, Paul Adams
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Hatuwezi kuthibitisha madai ya Ukraine kwamba mashambulizi yake katika kambi za anga za Urusi yamesababisha uharibifu wa dola za kimarekani bilioni 7 (£5.2bn), lakini ni wazi kwamba "Operesheni ya Spider's Web" ni ya kimapinduzi na ya kuvutia.

Raia wa Ukraine wanalinganisha mashambulizi hayo na mafanikio mengine ya kijeshi tangu uvamizi wa Urusi, ikiwa ni pamoja na kuizamisha manowari ya Urusi ya Moskva katika Bahari Nyeusi, na kulipua Daraja la Kerch, mwaka 2022, pamoja na shambulio la kombora kwenye bandari ya Sevastopol mwaka uliofuata.

Kwa kuzingatia maelezo yaliyofichuliwa na vyombo vya habari na shirika la ujasusi wa kijeshi la Ukraine (SBU), operesheni ya hivi karibuni ndiyo yenye mafanikio zaidi kufikia sasa.

Pia unaweza kusoma

Operesheni ilivyofanyika

Katika operesheni inayoelezwa kuchukua miezi 18 ya kujiandaa, ndege nyingi ndogo zisizo na rubani ziliingizwa nchini Urusi kinyemela, zikihifadhiwa katika sehemu maalum ndani ya malori ya mizigo, na kupelekwa maeneo manne tofauti, maelfu ya maili, na kisha kurushwa kuelekea katika kambi za karibu za anga.

"Hakuna operesheni ya kijasusi duniani iliyofanya jambo kama hili hapo awali," anasema mchambuzi wa masuala ya ulinzi Serhii Kuzan katika TV ya Ukraine.

"Ndege za kivita za Urusi zina uwezo wa kufanya mashambulizi ya masafa marefu dhidi yetu," anasema. "Kuna ndege 120 na tumezipiga 40 kati ya hizo. Hiyo ni idadi kubwa."

Ni vigumu kutathmini uharibifu uliotokea, lakini mwanablogu ya kijeshi wa Ukraine, Oleksandr Kovalenko anasema, “ukubwa wa uharibifu ni kwamba, jeshi la anga la Urusi, katika hali yake ya sasa, halina uwezo wa kuzirejesha ndege hizo katika siku za usoni," aliandika kwenye chaneli yake ya Telegraph.

Ndege za kivita zenye uwezo wa kubeba makombora zinazozungumziwa ni, Tu-95, Tu-22, na Tu-160, alisema, hazizalishwi tena. Kuzikarabati itakuwa ni vigumu, kubadilisha na ndege nyingine ni jambo lisilowezekana.

Ujumbe kwa Magharibi

Mbali na uharibifu huo, ambao unaweza kuwa au usiwe mkubwa kama wachambuzi wanavyoeleza, Operation Spider Web inatuma ujumbe mwingine muhimu, sio tu kwa Urusi lakini pia kwa washirika wa magharibi wa Ukraine.

Mfanyakazi mwenzangu Svyatoslav Khomenko, mwandishi wa tovuti ya BBC Ukrainian Service, katika mahojiano ya hivi karibuni na afisa wa serikali huko Kyiv.

"Tatizo kubwa," ofisa huyo alimwambia Svyatoslav, "ni kwamba Marekani inaamini tayari tumeshindwa vita."

Mwandishi wa habari wa masuala ya ulinzi wa Ukraine, Illia Ponomarenko, kupitia X, akirejelea moja kwa moja mkutano wa Rais Volodymyr Zelensky na Donald Trump katika Ikulu ya Marekani, amesema.

"Hiki ndicho kinachotokea pale taifa linaloshambuliwa linapoacha kuwasikiliza wale wote wanaosema: 'Ukraine imebakiwa na miezi sita tu'. ‘Haina nguvu.’ 'Ijisalimishe kwa ajili ya amani, Urusi haiwezi kupoteza.'

Jarida la Business Ukraine, kupitia X nalo limeweka ujumbe, "Baada ya yote, inaonekana Ukraine ina nguvu kadhaa. Leo Zelensky alikuwa Mfalme wa Droni."

Ujumbe ambao wajumbe wa Ukraine wataubeba wanapowasili Istanbul kwa duru mpya ya mazungumzo ya kusitisha mapigano na wawakilishi kutoka Kremlin: Ukraine bado iko kwenye mapambano.

Marekani "inatenda kana kwamba jukumu lake ni kujadiliana kwa ajili yetu kupitia masharti rahisi ya kujisalimisha," afisa wa serikali alimwambia Svyatoslav Khomenko.

"Na kisha wanachukia, tusipowashukuru. Ni kweli hatuwashukuru - kwa sababu hatuamini kuwa tumeshindwa."

Licha ya kusonga mbele polepole kwa Urusi katika uwanja wa vita huko Donbas, Ukraine inaiambia Urusi, na serikali ya Trump, wasitupilie mbali kirahisi matarajio ya Kyiv.