Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Ukraine: NATO yaonya kuanguka kwa mji wa Bakhmut kutafungua njia ya mashariki kwa Warusi
Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg alionya Jumatano kwamba mji wa Bakhmut mashariki mwa Ukraine unaweza kuangukia mikononi mwa vikosi vya Urusi katika siku zijazo baada ya miezi kadhaa ya mapigano makali.
Stoltenberg alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari huko Stockholm, pembezoni mwa mkutano uliojumuisha mawaziri wa ulinzi wa Umoja wa Ulaya: "Tunachoona ni kwamba Urusi inatuma wanajeshi zaidi, vikosi zaidi, na kile ambacho Urusi inakosa katika suala la ubora inachotaka ni kufidia kwa wingi."
Aliongeza, "Walipata hasara kubwa, lakini wakati huo huo hatuwezi kukataa kuanguka kwa Bakhmut katika siku zijazo."
"Pia ni muhimu kusisitiza kwamba hii haimaanishi mabadiliko yoyote katika kipindi cha vita," Stoltenberg, katibu mkuu wa muungano wa kijeshi unaounga mkono Ukraine, alisisitiza.
"Hii inaangazia tu kwamba hatupaswi kudharau Urusi. Ni lazima tuendelee kutoa msaada kwa Ukraine," alisema.
Haya yanajiri wakati ambapo kundi la mamluki wa Urusi "Wagner" lilidai siku ya Jumatano kwamba limeteka eneo la mashariki mwa mji wa viwanda wa Bakhmut, kutokana na kushadidi mapigano kati ya vikosi vya Urusi na Ukraine kwa miezi kadhaa.
Tangazo hilo lilikuja baada ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kuonya kwamba kuanguka kwa mji wa Bakhmut kutaipa Urusi "njia ya wazi" ya kuanzisha mashambulizi ndani zaidi nchini humo.
Ikiwa mkuu wa Wagner, Yevgeny Prigozhin, yuko sahihi, ina maana kwamba vikosi vya Urusi sasa vinadhibiti karibu nusu ya jiji katika kampeni yao ya kupata ushindi wao wa kwanza mkubwa katika miezi kadhaa.
Mapigano makali karibu na mji wa Bakhmut yametajwa kuwa ya muda mrefu na ya umwagaji damu zaidi ya uvamizi wa Urusi uliodumu zaidi ya mwaka mmoja, ambao umeharibu maeneo makubwa ya Ukraine na kusababisha mamilioni ya watu kuyahama makazi yao.
Mkuu wa Vikosi vya Wanajeshi wa Ukraine alisema katika ripoti yake Jumatano asubuhi: "Adui, licha ya kupata hasara kubwa, anaendelea kuuvamia mji wa Bakhmut."
"Kila kitu mashariki mwa Mto Pakhmutka kiko chini ya udhibiti wa Wagner," Prigozhin alisema kwenye mtandao wa Telegraph.
Jeshi la Ukraine lilisema hapo awali kwamba kazi kuu ya vikosi vyake huko Bakhmut ni kusababisha hasara nyingi iwezekanavyo kati ya Warusi na kudhoofisha uwezo wao wa kupigana.
Urusi, ambayo inadai kutwaa takriban asilimia 20 ya eneo la Ukraine, inashikilia kuwa kutekwa kwa mji wa Bakhmut kutakuwa hatua kuelekea kutwaa eneo lote la viwanda la mashariki la Donbass, lenye mikoa ya Donetsk na Luhansk.
Wachambuzi wa nchi za Magharibi wanasema kuwa mji wa Bakhmut una thamani ndogo ya kimkakati, lakini kukamatwa kwake kutaimarisha Rais wa Urusi, Vladimir Putin, na jeshi lake, baada ya mfululizo wa vikwazo.
Ukraine inasema kwamba hasara iliyopatikana na Urusi huko inaweza kuamua mkondo wa vita, kwa matarajio ya vita vikali kwa kuzingatia uboreshaji wa hali ya hewa, na Ukraine kupata msaada zaidi wa kijeshi wa Magharibi, pamoja na vifaru vizito vya mapigano.
Chini ya raia 4,000, ikiwa ni pamoja na watoto 38, kati ya wakazi wapatao 70,000 kabla ya vita walisalia katika mji huo, Irina Vereshuk, naibu waziri mkuu wa Ukraine, alisema, na sasa ni magofu baada ya miezi kadhaa ya mashambulizi ya mabomu.
"Hali ya jiji ni ngumu. Adui anavamia nafasi zetu kikamilifu. Licha ya hili, hawakufanikiwa, lakini walipata hasara kubwa," alisema mmoja wa walinzi wa mpaka wa Ukraine katika matangazo ya video na Huduma ya Mpaka wa Serikali.
Gavana wa Luhansk Serhiy Haidai alisema mkakati wa Urusi mashariki mwa Ukraine ni kuyateka maeneo yaliyosalia ya Donetsk na Luhansk ambayo haiyadhibiti.
Aliongeza kwa TV ya Ukraine: "Kuhusu mbinu za kupigana, wanatambua kwamba hawana uwezo wa kufikia maendeleo yoyote ya haraka, kwa hiyo wana mbinu moja, wanasonga popote wanaweza. Na wakiona mafanikio yoyote mahali fulani, wanajeshi wote wanakwenda huko."
Mipango ya ulinzi
Mawaziri wa Umoja wa Ulaya walijadili mipango ya kuimarisha uzalishaji wa ulinzi na kusambaza silaha nzito kwa haraka kwa Ukraine kwani inatumia maelfu ya silaha kila siku.
"Sasa ni vita vya mvutano," Stoltenberg alisema. "Ni vita ya vifaa."
Aliongeza, "Kiwango cha sasa cha matumizi ikilinganishwa na kasi ya uzalishaji wa silaha sio endelevu, na hivyo tunahitaji kuongeza uzalishaji."
Katibu Mkuu wa NATO alikaribisha msukumo wa nchi kutoka Umoja wa Ulaya kuimarisha ulinzi. “Hili ni jambo ambalo tunalifanyia kazi, tumeona hatua muhimu zikichukuliwa,” alisema.
"Lakini tunahitaji kufanya zaidi, kwa sababu tunahitaji kuhakikisha kwamba Ukraine inapata risasi inazohitaji ili kujilinda dhidi ya uvamizi wa kijeshi wa Urusi, na tunahitaji kuongeza tena hifadhi zetu," alisema.
Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Oleksiy Reznikov alisema Kiev inahitaji kwa dharura vifaa vingi vya mizinga ili kuanzisha mashambulizi ya jumla dhidi ya jeshi la Urusi.
Aliwataka wanachama wa EU kuunga mkono mpango wa Estonia wa ununuzi wa pamoja wa silaha.
Alisema anaunga mkono pendekezo lililotolewa na Estonia kwa Umoja wa Ulaya la kununua makombora milioni moja ya 155 mm kwa Ukraine mwaka huu kwa gharama ya euro bilioni 4.
Reznikov alisema wakati wa mkutano na waandishi wa habari kabla ya mkutano huo: "Tunahitaji kusonga mbele haraka iwezekanavyo."