Kombe la Dunia 2034: Uamuzi kombe la dunia kufanyika Saudia haupaswi kukushangaza

Matarajio ya Kombe la Dunia kufanyika nchini Saudi Arabia yamekuwepo kwa muda mrefu, kutokana na uwekezaji usio na kifani wa nchi hiyo katika michezo ndani ya miaka ya hivi karibuni.

Jinsi nchi hiyo ilivyoukamata ulimwengu wa mchezo wa gofu, au kuanza kutawala uandaaji wa ngumi za kulipwa, ama namna inavyohamisha wachezaji wa soka wa kimataifa kwenda katika ligi yake.

Mikutano ya mara kwa mara ambayo rais wa Fifa Gianni Infantino amekuwa nayo na Mwana Mfalme wa Saudia katika miaka ya hivi karibuni - ilikuwa ni ishara ya ushawishi unaoongezeka wa nchi hiyo katika michezo.

Mamlaka za Saudia zinakanusha kwamba mipango yao ni kwa lengo la kujisafisha kwa kutumia michezo. Nchi hiyo inasisitiza ombi lao ni kwa ajili ya kusaidia nchi hiyo kuwa ya kisasa, kukuza michezo, kukuza utalii, kuleta uchumi mseto kabla ya kuachana na uchumi wa kutegemea mafuta na kwa ajili ya kuwaleta watu pamoja.

Maswali yanayotaka jawabu

Lakini bila kujali nia ya kweli ya watawala wa Saudi Arabia, kuibuka kwake kama mzabuni pekee kwa mwaka wa 2034 kutaongeza ufuatiliaji juu ya michakato na maamuzi wa Fifa.

Kwanza tangazo la Fifa lilikuwa la ghafla sana - mapema mwezi huu, iliuleta mapema mchakato wa zabuni ya 2034 na kuamuru nchi mwenyeji lazima itokee Asia au Oceania, na kutoa siku 26 tu kwa zabuni kutangazwa.

Ndipo likaja tangazo rasmi la Saudi Arabia la kutoa ombi la kuandaa mashindano hayo, likifuatiwa na kuungwa mkono upesi na Shirikisho la Soka la Asia.

Kama Fifa ingeweka mkutano na waandishi wa habari na kujibu maswali kufuatia tangazo lake mapema mwezi huu - labda ingesema njia hii ya 'kupata waandaji' kupitia zabuni ambazo hazipingwi - ni bora kuliko njia ya zamani.

Kwani mashindano ya kupata uenyeji yaliyokuwa yakichukua miaka mingi na kujumuisha nchi nyingi - yalikuwa hatarini kukumbwa na kubadilishana kura, hongo na ufisadi.

Ukosoaji

Mwezi Machi, Jukwaa la Ligi za Dunia - ambalo linawakilisha ligi za nyumbani kote ulimwenguni - lilionyesha "wasiwasi" wake juu ya kile ilichodai - Fifa haikushauriana nao juu ya kalenda ya kombe la dunia na kulipanua kombe hilo kuanzia 2026.

Human Rights Watch pia imeishutumu Fifa kwa kupuuza sheria zake yenyewe, ikisema: "Fifa kuipa Saudi Arabia uenyeji wa Kombe la Dunia la 2034 licha ya rekodi yake ya kutisha ya haki za binadamu na kukataa kufuatiliwa - kunafichua kwamba ahadi za Fifa juu ya haki za binadamu ni za uongo."

Fifa imekataa kutoa maoni, lakini inasisitiza haki za binadamu zinasalia kuwa sehemu muhimu ya mchakato wa zabuni. Hakika Saudi Arabia haitakuwa mwenyeji pekee mwenye utata katika miaka ya hivi karibuni.

Mahusiano ya watu wa jinsia moja ni kinyume cha sharia. Je, kutakuwa na maandamano ya wachezaji kama yaliyoonekana nchini Qatar, wakati timu ya Ujerumani ilipoonyesha kuunga mkono LGBTQ+? Je, baadhi ya nchi zinaweza kufikiria kugomea tukio hilo?

Kilicho wazi ni kwamba kuna mabadiliko ya ajabu kuhusu nguvu ya michezo Mashariki ya Kati. Mfano, Qatar nchi ndogo na nchi jirani ya Saudi Arabia – iliweza kuandaa Kombe la Dunia ndani ya kipindi cha miaka 12 tu.

Saudi Arabia itasemaje?

Wasaudi nao wataendelea kujitetea dhidi ya kile wanachokiona kuwa ni unafiki. Wanafanya biashara na nchi nyingi za Magharibi na zinafurahia biashara hiyo.

Wataugusia pia ujinga uliopo, kama alivyosema hivi karibuni bondia Tyson Fury baada ya kupigana huko Riyadh; watu wasihukumu ufalme kabla ya kuutembelea wenyewe.

Saudi Arabia itafanya ulinganisho na Qatar, licha ya kukosolewa sana, iliweza kuandaa Kombe la Dunia ambalo lilielezwa na wengi waliohudhuria kuwa lilifanikiwa.

Na wengine watasema ufichuaji wa vyombo vya habari unaoambatana na maandalizi ya Kombe la Dunia unaweza kusaidia kuharakisha mageuzi - kama alivyosema Jordan Henderson hivi karibuni alipokuwa akijibu ukosoaji kwa kuhamia katika Ligi ya Saudi Arabia.

Mamlaka ya Saudia na Fifa sasa wana miaka 11 kujaribu kuwashawishi wenye shaka.