Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waridi wa BBC:'Saratani ilinitoa hamu ya tendo la ndoa'
Na Anne Ngugi
BBC Swahili
Kati ya mwaka jana na mwaka huu wa 2023 maisha yake Connie yamechukua mkondo tofauti ambao hangetarajia.
Ikiwa ndio miaka ya mwanzo baada ya kutimiza miaka thelathini na pia Miaka minne tu katika ndoa yao, Connie alipokea habari za kuogofya za utambuzi wa saratani inayoathiri damu kwa jina Acute Lymphoblastic Leukemía.
Aina hii ya saratani ya damu inaanzia katika sehemu ya uboho.
Jinsi alivyogundua kwamba ana saratani
Kuanzia mwaka jana , Connie alikuwa anapitia mabadiliko mengi katika mwili wake, na hakuweza kuelewa ni kwanini.
Sehemu moja ya mabadiliko hayo makubwa ilikuwa ni uchovu mwingi licha ya kwamba hakuwa amebadilisha mfumo wa kazi aliyokuwa akiifanya kama mshauri katika shule moja ya sekondari nchini Kenya.
Vilevile anasema kuwa alianza kuumwa na sehemu ya mgongo na maumivu yalikuwa yanapungua pindi anapopata lepe la usingizi.
Masaibu haya yote yalimsukuma kutaka kufahamu zaidi kilichokuwa kinamuuma. Harakati za kuwaona wataalamu kadhaa zilianza na wote waligundua kuwa alikuwa anaugua saratani ya damu .
Habari za matokeo hayo zilimpa Connie na jamii yake hofu na kiwewe huku fikra nyingi zikimjia kuhusu hatma ya maisha yake.
Mojawapo ya fikra hizo ilikuwa ile ya kwamba alikuwa anakaribia kifo.
Hatahivyo rafiki yake mkuu hakuruhusu hilo na kumshauri “Ni wakati wa kukabiliana na ugonjwa huo'' , anakumbuka akiongezea kwamba maongezi hayo yalimpa mwamko mpya na ari ya kupigania maisha yake .
Hali ya saratani kwenye ndoa
Mojawapo ya masomo makubwa ambayo mwanadada huyu ameyavalia njuga na hata kufunza watu wengine ni kuhusu mahusiano kati ya mume na mke baada ya saratani kugunduliwa kati yao na jinsi maisha yanavyobadilika ghafla.
Jambo la kwanza ambalo ana fahari nalo ni usaidizi usioyumba wa mume wake ambao umekuwa ngao muhimu katika kudumisha uthabiti wake katika nyakati hizi ngumu anapo pitia matibabu sugu ya saratani.
Ila anasema kuwa pindi alipoanza matibabu ya saratani hasa yanayofahamika kama (Chemotherapy) yaani mfumo maalum ambao wagonjwa wa saratani huwekwa madawa ya kuangamiza seli , hedhi ya kila mwezi ilipotea na , hivyo basi kupelekea hisia za kufanya tendo la ndoa kushuka .
“Unajua hakuna kitu mtu anaweza kufanya uwe kwenye ndoa au la , ikiwa unapitia matibabu haya hisia za kujamiana zinakuwa kitu cha mwisho akilini , sio kupenda kwa mtu ”anasema Connie
Vilevile anaongezea kuwa uchovu wa mwili pia huchangia hisia za ngono kushuka na mara nyingi wagonjwa hupendelea kupumzika au kulala kutokana na maumivu wanayopitia.
Ila anasema kuwa mshauri aliyekuwa anaandamana nao alimpa mume wake ushauri wa kutosha kuhusiana na matukio kama hayo kuwepo, akiongezea kuwa mume wake alimuelewa .
“Kwa hiyo ilikuwa rahisi kwa mume wangu kukabiliana na hisia za kujamiana kwasababu tayari alikuwa ametayarishwa na washauri kuhusu mabadiliko ambayo saratani ingeleta kwenye jamii yetu ”anasema Connie.
Lakini licha ya yote hayo, hatma ya ndoa yake, ulezi wa mtoto mchanga, hali kadhalika hofu ya kuwa angeaga na kuacha jamii changa pia ni masuala yaliomkosesha usingizi .
Maumimivu na uchovu wa mara kwa mara hatahivyo ulimfanya kushindwa kumpakata na kumuonesha mapenzi mwanae mchanga.
“Kubeba mwanangu au kucheza naye ni kitu kilichokuwa kinanisumbua sana ”anasema.
Suala jingine lililomkosesha usingizi ni lile la kupoteza nywele ambapo muda mwingi alisalia bila nywele kichwani.
“Mbali na kupoteza nywele zote kichwani nilikuwa na hasira sana , vitu vidogo vidogo vilinishinikiza kukasirikia watu kila wakati, hata mtu akipita mbele yako unakuwa tu umekasirika , na wakati mwingi unakasirikia maisha bila sababu ” Anakumbuka Connie
Kujikubali
Yote tisa kumi Connie anasema kuwa imekuwa karibu miezi kumi ya kujikubali upya baada ya mabadiliko mengi kuletwa na uwepo wa saratani ya damu maishani mwake .
Mwanadada huyu ni mwingi wa shukrani kwa mume wake ambaye amesimama naye kipindi hiki kigumu cha kujikubali na kujipenda upya .
Wazo lake la mwisho ni kuwa kwa mtizamo wake wagonjwa wengi wanakata tamaa kwa kukosa watu wa karibu wa kusimama nao wakati wanauguza ugonjwa huo hatari .
Kwasasa malengo yake ni kutaka kutoa usaidizi kwa wengine ambao pia wanapambana na saratani.