Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, silaha za nyuklia za Marekani zinaweza kurejeshwa Uingereza?
- Author, Matt Precey
- Nafasi, BBC News, Suffolk
Silaha za nyuklia huenda zikarejeshwa katika kambi ya Jeshi la Wanahewa la Marekani mjini Suffolk miaka 15 baada ya nchi hiyo kuripotiwa kuondoa silaha zake za mwisho.
Nyaraka zinaonyesha kuwa kambi ya RAF Lakenheath inatayarisha vifaa vya kuweka na kulinda mabomu yenye nguvu zaidi ya ile iliyodondoshwa huko Hiroshima mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia.
Tunajua nini kuhusu mipango hiyo?
RAF Lakenheath kwa sasa ni makao ya 48 wa ndege za kivita, pia inajulikana kama Liberty Wing, na ndege ya hivi karibuni ya F-35A Lightning II imewekwa hapo.
Kulingana na USAF ndege hizi za kivita zimejaribiwa kwa mafanikio ili kubeba bomu la nyuklia aina ya B61-12, silaha ya kimkakati iliyoundwa kwa ajili ya uwanja wa vita.
Nyaraka zinazoelezea mkataba uliotolewa wa kujenga makao ya ulinzi kwa ajili ya "ujumbe ujao wa nyuklia" wa RAF Lakenheath zilichapishwa, na kisha kuondolewa, na Idara ya Ulinzi ya Marekani.
Vitengo hivi tamba vitalinda wanajeshi waliopewa jukumu la kulinda kambi, Kitengo cha 48 cha Vikosi vya Usalama.
Kando na hilo, mamilioni ya dola yametengwa kujenga kituo kinachojulikana kama "surety dormitory" katika kambi hiyo, ambayo inasadikiwa kuwa hifadhi ya silaha za nyuklia, kulingana na waraka wa bajeti ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani.
Kambi ya RAF kilifunguliwa Lakenheath mnamo 1941 na kilifanya kazi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.
Wakati Vita Baridi kati ya Nato na Muungano wa Soviet vilipozidi, USAF ilichukua udhibiti wa kiutawala wa kituo hicho mwaka 1951.
Kuna maafisa 4,000 wa kijeshi wa Marekani na wafanyakazi wengine 1,500 wa Uingereza na Marekani katika kambi hiyo.
Je, silaha zitafika Suffolk?
Sir Lawrence Freedman, profesa mstaafu wa masomo ya vita katika Chuo cha King's College London, alisema kuna "mapendekezo kadhaa" mipango hiyo ilikuwa ya tahadhari.
Makazi hayo yanaweza kuwa na uwezo wa ziada endapo silaha nyingine zilipaswa kuondolewa kwenye maeneo ya uhifadhi huko Ulaya, aliongeza.
"Ni jambo moja kujenga kituo cha kuhifadhi, ni jambo lingine kuficha ukweli kwamba silaha za Marekani zitakuwa nchini Uingereza, kwa hivyo inaweza kuwa na maelezo ya kawaida badala ya kuwa aina fulani ya kuongezeka kwa kasi ya ununuzi wa silaha, " alisema.
Uingereza na Nato wana sera ya muda mrefu ya kutothibitisha au kukataa kuwepo kwa silaha za nyuklia katika eneo fulani.
Kwa nini mpango huu unafanyika sasa?
Sir Lawrence alisema haoni ikiwa mipango hii inahusiana na hali ilivyo nchini Ukraine.
"Ni sehemu ya, nadhani, ongezeko la jumla la mvutano na Urusi," alisema.
"Pia inaonyesha kipaumbele cha juu kilichopewa mifumo ya masafa mafupi katika mafundisho ya Kirusi."
Lakini William Alberque, afisa mkuu wa zamani wa NATO ambaye sasa anafanya kazi na Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kimkakati, alisema ni "jibu kwa mazingira hatarishi yanayozidi kuwa tishio kote Ulaya kwa sababu ya hatua za Urusi".
Hii ina maana gani kwa kambi?
Hans Kristensen, kutoka Shirikisho la Wanasayansi wa Marekani, alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kugusia uwezekano wa silaha za nyuklia kurejeshwa katika kambi ya RAF Lakenheath.
"Bila shaka ikiwa una silaha za nyuklia kwenye kambi, kuna uwezekano mkubwa wa kambi kulengwa katika mzozo wa nyuklia na Urusi," alisema.
"Mara tu itakapobainika una silaha za nyuklia ndani ya kambi, mambo yanabadili."
Bw Alberque alisema kuna uwezekano mkubwa kwamba kambi hiyo tayari ilikuwa inalengwa na Urusi.
"Ikiwa mimi ni mpangaji wa jeshi la Urusi, tayari nitaipiga. Ukitazama televisheni ya Urusi, wanazungumza sana kuhusu Uingereza; wanazungumza juu ya kuinukisha Uingereza sana."
Bw Alberque anaamini Rais wa Urusi Vladimir Putin angeidhinisha matumizi ya silaha hizo.
"Kusema ana uwezo itakuwa ni kutoelewa. Ikiwa anaona ukosefu wa suluhu na ukosefu wa matokeo nadhani angeweza," alisema.
Nini kitatokea baadaye?
Wanaharakati wa kundi la kupigania Kupunguzwa kwa Silaha za Nyuklia (CND) tayari wameandamana nje ya kambi hiyo.
Katibu Mkuu wa CND Kate Hudson alisema: "Ikiwa ziko hapa, tutaziondoa."
Kundi hilo limeiagiza kampuni ya mawakili ya Leigh Day kuangalia iwapo ujenzi wa kambi hiyo ni halali.
Wakili Ricardo Gama alisema: "Wizara ya Ulinzi ya [Uingereza] inasema kwamba matukio ya Lakenheath hayatasababisha athari kubwa za mazingira, lakini katika kufikia hitimisho hilo mteja wetu anahoji kuwa wamepuuza athari za kimazingira zinazoweza kutokana za kuweka silaha za nyuklia kwenye uwanja wa ndege. , ikiwa ni pamoja na uwezekano wa ajali za nyuklia".
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi