Japan: Wasiwasi na hasira juu ya mpango wa maji taka ya nyuklia

dd

Chanzo cha picha, Getty Image

Maelezo ya picha, Tangu tsunami ya 2011 ambayo iliharibu vibaya mtambo huo, zaidi ya tani milioni za maji taka yamekusanyika hapo

Mpango tata wa Japan wa kutoa maji machafu kutoka kinu cha nyuklia cha Fukushima kuyapeleka Bahari ya Pasifiki umezua wasiwasi na hasira ndani na nje ya nchi.

Tangu tsunami ya 2011 ambayo iliharibu vibaya mtambo huo, zaidi ya tani milioni za maji taka yamekusanyika hapo. Japan imesema itaanza zoezi hilo siku ya Alhamisi.

Licha ya kuidhinishwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya nyuklia, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), mpango huo umekuwa na utata mkubwa nchini Japan huku jumuiya za ndani zikielezea wasiwasi wake kuhusu uchafuzi huo.

Vikundi vya uvuvi nchini Japani wameelezea wasiwasi wao kuhusu maisha yao, kwani wanahofia walaji wataepuka kununua samaki.

Uchina imeishutumu Japan kwa kuchukulia bahari kama "mfereji wa maji taka wa kibinafsi", na kuikosoa IAEA. Wakati serikali ya Korea Kusini imesema inaunga mkono mpango huo, wananchi wengi wanaonekana kuupinga.

Je, maji hayo ni salama?

Tangu kutokea kwa maafa hayo, kampuni ya kuzalisha umeme ya Tepco imekuwa ikisukuma maji ili kupoza vinu vya nyuklia vya Fukushima. Hii ina maana kila siku kiwanda hicho hutoa maji machafu, ambayo yanahifadhiwa katika matangi makubwa.

Zaidi ya matangi 1,000 yamejazwa, na Japan inasema hili si suluhisho endelevu. Inataka kutoa maji haya hatua kwa hatua katika Bahari ya Pasifiki katika kipindi cha miaka 30 ijayo, ikisisitiza kuwa ni salama kutolewa.

Kutoa maji taka na kusafirishwa baharini ni utaratibu wa kawaida kwa vinu vya nyuklia. Tepco huchuja maji ya Fukushima, na kupunguza vitu vingi vya mionzi hadi viwango vinavyokubalika vya usalama.

Tepco na serikali ya Japan wamefanya tafiti kuonyesha maji yaliyotolewa yataleta hatari ndogo kwa wanadamu na viumbe vya baharini.Wanasayansi wengi pia wameunga mkono mpango huo.

"Maji yatakayo tolewa yatakuwa tone kwa bahari, katika suala la ujazo na mionzi. Hakuna ushahidi kwamba viwango hivi vya chini sana vya mionzi vitaleta athari mbaya kiafya," alisema mtaalamu wa magonjwa ya molekuli Gerry Thomas, ambaye alifanya kazi na wanasayansi wa Japan - kuhusu utafiti wa mionzi na kuishauri IAEA kuhusu ripoti za Fukushima.

Wakosoaji wanasemaje?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wataalamu wa haki za binadamu walioteuliwa na Umoja wa Mataifa wamepinga mpango huo, sawa na wanaharakati wa mazingira. Greenpeace imetoa ripoti zinazoeleza shaka juu ya mchakato huo wa Tepco, kwa madai kuwa vitu vyenye mionzi havijaondolewa vya kutosha.

Wakosoaji wanasema Japan inapaswa, kuweka maji taka kwenye matangi. Ili kutafuta teknolojia mpya za usindikaji, na kuruhusu mionzi iliyobaki kuzidi kupungua.

Pia, kuna baadhi ya wanasayansi ambao hawafurahishwi na mpango huo. Wanasema kunahitajika tafiti zaidi juu ya jinsi maji hayo yangeathiri bahari na viumbe vya baharini.

"Tumeona tathmini isiyotosheleza ya athari za mionzi, kiikolojia - ambayo inatufanya tuwe na wasiwasi mkubwa kwamba Japan haitaweza kugundua kile kinachoingia kwenye maji, mchanga na viumbe, lakini ikiwa yatayamwaga, hakuna njia ya kuyazoea. Hakuna njia ya kumrudisha jini kwenye chupa," mwanabiolojia wa baharini Robert Richmond, profesa katika Chuo Kikuu cha Hawaii, aliambia kipindi cha Newsday cha BBC.

Tatsujiro Suzuki, profesa wa uhandisi wa nyuklia kutoka Chuo Kikuu cha Nagasaki, aliiambia BBC kuwa mpango huo "hautasababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira au kudhuru umma - ikiwa kila kitu kitakwenda sawa".

Lakini kutokana na kwamba Tepco ilishindwa kuzuia maafa ya 2011, bado ana wasiwasi kuhusu uwezekano wa kutolewa kwa maji machafu kwa bahati mbaya, alisema.

Majirani wa Japan wamesema nini?

gh

Chanzo cha picha, CHUNG SUNG-JUN

Maelezo ya picha, Maelfu wamehudhuria maandamano mjini Seoul wakitaka serikali ichukue hatua

China imeitaka Japan kufikia makubaliano na nchi za kikanda na taasisi za kimataifa kabla ya kutoa maji hayo. Beijing pia imeishutumu Tokyo kwa kukiuka "majukumu ya kimataifa ya kimaadili na kisheria," na kuonya kwamba ikiwa itaendelea na mpango huo, "lazima itabeba matokeo yote".

Nchi hizo mbili kwa sasa zina uhusiano mbaya. Tokyo imefanya mazungumzo na majirani zake, na kuwa mwenyeji wa timu ya wataalamu wa Korea Kusini katika ziara ya kiwanda cha Fukushima mwezi Mei. Lakini haina uhakika ni kwa kiasi gani ingejitolea kupata idhini ya nchi jirani kabla ya kuendelea na mpango huo.

Tofauti na China, Seoul - ambayo imekuwa na nia ya kujenga uhusiano na Japan - imepunguza wasiwasi wake na Jumanne ilisema "inaheshimu" matokeo ya IAEA.

Lakini mbinu hii imewakasirisha umma wa Korea Kusini, 80% ambao wana wasiwasi kuhusu kutolewa kwa maji kulingana na kura ya maoni ya hivi majuzi.

"Serikali inatekeleza sera kali ya kutotupa takataka baharini. Lakini sasa serikali haisemi neno kuhusu maji machafu ya Japan yanayotiririka baharini," Park Hee-jun, mvuvi wa Korea Kusini aliiambia BBC Korea.

"Baadhi ya maafisa wanasema tunapaswa kukaa kimya ikiwa hatutaki kuwafanya watumiaji wawe na wasiwasi zaidi. Nadhani huo ni upuuzi."

Maelfu wamehudhuria maandamano mjini Seoul wakitaka serikali ichukue hatua, huku baadhi ya wanunuzi wakihofia kukatizwa kwa usambazaji wa chakula wamerundika chumvi na mahitaji mengine.

Kujibu, bunge la Korea Kusini lilipitisha azimio mwishoni mwa Juni kupinga mpango wa kutolewa kwa maji. Maafisa pia wamezindua "ukaguzi mkali" wa samaki. Na wanashikilia marufuku iliyopo ya uagizaji wa samaki wa Kijapani kutoka maeneo karibu na kiwanda cha Fukushima.

Ili kupunguza hofu ya umma, waziri mkuu Han Duck-soo alisema atakuwa tayari kunywa maji ya Fukushima ili kuonyesha kuwa ni salama, huku afisa mmoja alisema wiki iliyopita kwamba ni sehemu ndogo tu ya maji yanayotiririka yataishia kwenye maji ya Korea.

Mataifa kadhaa ya visiwa pia yameelezea wasiwasi wao na kundi la Visiwa vya Pasifiki likiuita mpango huo "janga kubwa la uchafuzi wa nyuklia."

Japani imeitikiaje?

Japani na Tepco wamejaribu kuwashawishi wakosoaji kwa kutoa maelezo ya kisayansi juu ya mchakato huo, na wataendelea kufanya hivyo kwa uwazi wa hali ya juu, aliahidi waziri mkuu Fumio Kishida siku ya Jumanne.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya wizara yake ya mambo ya nje, Japan pia ilisema vinu vingine vya nyuklia katika eneo hilo - haswa vile vya Uchina - vinamwaga maji yenye viwango vya juu zaidi ya mionzi. BBC iliweza kuthibitisha baadhi ya takwimu hizi kwa data inayopatikana katika mitambo ya nyuklia ya China.

Ripoti ya IAEA, iliyokuja baada ya uchunguzi wa miaka miwili, iligundua Tepco na Japan walifikia viwango vya usalama vya kimataifa katika vipengele kadhaa ikiwa ni pamoja na vifaa, ukaguzi na utekelezaji, ufuatiliaji wa mazingira, na tathmini za mionzi.

Hata hivyo uamuzi wa Japan kuanza kumwaga maji ya Fukushima umeweka mazingira ya mchuano mkali na wakosoaji wake.