Timu gani yenye uwezekano zaidi wa kupambana na Liverpool

Muda wa kusoma: Dakika 5

Liverpool watakuwa na wakijiamini kutetea taji lao la Ligi Kuu ya England baada ya kuvunja rekodi ya kwa usajili.

Majogoo hao wa Anfield, katika msimu wao wa kwanza chini ya kocha Arne Slot, walishinda taji la Ligi Kuu wakiwa wamesalia na mechi nne - wakimaliza kwa pointi 10 mbele ya Arsenal iliyoshika nafasi ya pili.

Kikosi cha Slot kimetumia pauni za Uingereza milioni 269 kufikia sasa ikiwa ni pamoja na usajili uliovunja rekodi ya klabu wa pauni milioni 100 zilizotumika kumpata kiungo wa Bayer Leverkusen Florian Wirtz - Kiwango hicho kinaweza kupanda hadi pauni milioni 116.

Mshambulizi wa Eintracht Frankfurt, Hugo Ekitike (pauni milioni 69 za awali), beki wa kushoto wa Bournemouth, Milos Kerkez (£40m) na beki wa kulia wa Leverkusen, Jeremie Frimpong (£29.5m) ni wachezaji wengine muhimu waliosajiliwa, huku kipa wa Valencia, Giorgi Mamadashvili amejiunga kwa uhamisho wa pauni milioni 25 mwaka jana.

Lakini wengi wa wapinzani wao wa taji wametumia pesa nyingi msimu huu pia.

BBC Sport inaangalia jinsi timu tano bora za msimu uliopita zilivyosajili na iwapo kuna yoyote anayoweza kuikamata Liverpool.

Unaweza kusoma

Arsenal (ya pili, ikizidiwa lama 10 kutoka kileleni)

Baadhi ya waliosajiliwa: Viktor Gyokeres (Sporting), Martin Zubimendi (Real Sociedad), Noni Madueke na Kepa Arrizabalaga (Chelsea), Christian Norgaard (Brentford), Cristhian Mosquera (Valencia).

Baadhi ya walioondoka: Kieran Tierney, Jorginho, Thomas Partey, Takehiro Tomiyasu (wote wameachwa)

Fedha zilizotumika: £201m

Mwandishi wa Michezo wa BBC, Alex Howell: "Msimu huu ni muhimu kwa Arsenal na hakuna mtu aliye karibu na klabu anaogopa kuusema. Wachezaji, meneja na hata uzinduzi wa jezi zote wamerejelea kauli mbiu ya 'fikia mafanikio mapya' - huku wakiwa na matumaini ya kushinda kombe kwa mara ya kwanza tangu 2020.

"The Gunners wametumia zaidi ya pauni milioni 190 katika ada za awali huku wakitafuta kukisuka vilivyo kikosi kwa kuleta wachezaji wapya, ikiwa ni pamoja na matarajio makubwa ya kumpata Viktor Gyokeres kutoka Sporting ya Ureno.

"Mikel Arteta amefanya kazi nzuri sana kuibadilisha Arsenal kuwa washindani kwa muendelezo katika ligi na kutandaza soka safi Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini sasa ni wakati wao kupiga hatua zaidi. Huu utakuwa msimu wenye shinikizo baada ya kukaribia kutwaa ubingwa katika misimu kadhaa ya hivi karibuni.

"Arteta anaonekana kubadilisha jinsi Arsenal wanavyocheza, pia. Wakati wa maandalizi ya msimu mpya The Gunners wamecheza mpira kwa kasi, wakipeleka mpira mbele katika maeneo ambayo wanaweza kufunga magoli.

"Yote hayo yamefanywa ili kukamilisha mtindo wa uchezaji wa Gyokeres na, ingawa inaweza kuchukua muda, ikiwa itazaa matunda, Arsenal itakaribia tena kutwaa ubingwa."

Manchester City (ya 3, alama 13 kutoka kileleni)

Baadhi ya waliosajiliwa: Tijjani Reijnders (AC Milan), Rayan Cherki (Lyon), Rayan Ait-Nouri (Wolves), James Trafford (Burnley), Sverre Nypan (Rosenborg).

Walioondoka: Kevin de Bruyne (ameachwa), Kyle Walker (Burnley)

Fedha zilizotumika: £154m

Mwandishi wa Michezo wa BBC, Shamoon Hafez: "Manchester City watakuwa mnyama aliyejeruhiwa baada ya msimu mbaya, bila shaka, bila kushinda taji kubwa, na kuhitimisha na kutupwa nje ya kombe la Kombe la Dunia la Vilabu hatua ya 16 bora.

"Bosi Pep Guardiola amekiimarisha kikosi na kusajili wachezaji watano wapya, ikiwa ni pamoja na kuipa nguvu tena safu ya kiungo kwa kumnunua Tijjani Reijnders kutoka AC Milan.

"Tangu 2017 City wamemaliza nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu, kwa hiyo kunaweza kuwa na sintofahamu kuhusu jinsi watakavyofanya na jinsi damu mpya inavyoingia kikosini.

"Mabingwa Liverpool na Arsenal wanazungumziwa kama vinara wa ubingwa msimu huu, kwa hiyo inaweza kuwafaa City kuchupa, huku huku macho yakielekezwa kwa wapinzani wengine wawili.

Chelsea (ya 4, alama 15 kutoka kileleni)

Baadhi ya waliosajiliwa: Liam Delap (Ipswich), Joao Pedro (Brighton), Jamie Gittens (Borussia Dortmund), Jorrel Hato (Ajax).

Mikataba iliyokamilishwa awali na kutekelezwa msimu huu: Dario Essugo (Sporting), Estevao Willian (Palmeiras).

Baadhi ya walioondoka: Kepa Arrizabalaga (Arsenal), Joao Felix (Al-Nassr), Djordje Petrovic (Bournemouth), Mathis Amougou (Strasbourg).

Fedhaa zilizotumika: £249m

Mwandishi wa Michezo wa BBC, Nizaar Kinsella: "Ushindi wa Chelsea wa mabao 3-0 katika fainali ya Kombe la Dunia la Vilabu dhidi ya mabingwa wa Ulaya Paris St-Germain ulituma ujumbe wenye uzito unaopaswa kutiliwa maanani kuwa ni kikosi cha kuchungwa.

"Meneja Enzo Maresca ameunganisha kundi la wachezaji ambao waligharimu hadi pauni bilioni £1.4, kulingana na amana za klabu yenyewe, na ingawa wachezaji 11 walioanza walikuwa vijana zaidi kuwahi kucheza msimu wa Ligi Kuu ya England msimu uliopita, wanaonekana kuwa wazuri vya kutosha kushinda mataji.

"Miongoni mwa wachezaji nyota ni Cole Palmer, Enzo Fernandez, Moises Caicedo na Marc Cucurella lakini The Blues pia wamewaongeza Joao Pedro, Liam Delap, Jamie Gittens, Estevao Willian na Jorrel Hato msimu huu ili kukabiliana na mzigo ulioongezeka wa kurejea Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

"Ndani ya klabu, Chelsea wameweka tena malengo yao kumaliza ndani ya nafasi ya nne bora kwenye ligi, lakini beki Levi Colwill ni miongoni mwa wale wanaoona kuwa wako tayari kunyakua taji la Ligi Kuu au Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao."

Newcastle (ya 5, alama 18 kutoka kileleni)

Baadhi ya wachezaji wapya: Anthony Elanga (Nottingham Forest), Aaron Ramsdale (Southampton, mkopo)

Aliyeondoka: Sean Longstaff (Leeds)

Makubaliano ya awali yaliyotekelezwa majira ya kiangazi: Lloyd Kelly (Juventus)

Fedha zilizotumika: £55m

Mwandishi wa Michezo wa BBC Ciaran Kelly: " Ni rahisi kusahau kwamba Newcastle United kiufundi, walikuwa na bado wapo katika mbio za kumaliza nafasi ya pili hadi ilipokuwa imesalia michezo michache kabla ya ligi kufikia tamati.

"Newcastle ilimaliza nafasi ya tano, lakini klabu hiyo ilikuwa imara kuelekea majira ya kiangazi baada ya kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya na kumaliza ngoja ngoja ya muda mrefu ya kunyakua taji.

" Hili pekee halijathibitisha mageuzi.

"Newcastle imewakosa wachezaji wengi iliyotaka kuwasajili, wakiwemo Hugo Ekitike, Joao Pedro, James Trafford, Liam Delap na Dean Huijsen.

"Sakata la Alexander Isak saga linaendelea kuwa kizungumkuti na kumekuwepo mzozo kwenye uongozi wa klabu hiyo kufuatia kuondoka kwa mkurugenzi wa ufundi Paul Mitchell.

"Limekuwa jambo lisilofaa.

"Newcastle bado ina kikosi chenye uwezo wa kushindana na timu bora kabisa, kama walivyodhihirisha dhidi ya Liverpool katika fainali ya kombe la Carabao, lakini kikosi hiki chenye wachezaji wachache wa kiwango cha juu kinahitaji maboresho ya haraka ili kuwa na uwezo wa kushindani na timu vigogo kwa ufanisi."