Mtu wa nne duniani mwenye figo nne apatikana nchini Somalia

Watu wenye figo za ziada huwa hawajitambui mpaka pale wanapopatwa na hali ya kiafya inayowalazimu kumtembelea daktari, bila kujua juu ya ukuu wa ziada ambao Mungu amewapa, lakini hugundua tu wanapopima, na wanafahamu baada ya uchunguzi wa ultrasound au baada ya upasuaji.

Kuna watu watatu pekee wenye figo za ziada zilizorekodiwa duniani kote na mtu wa nne amepatikana nchini Somalia.

Mvulana mdogo ambaye madaktari hawajataja jina lake, aliugua baada ya uchunguzi wa muda mrefu na kugundulika kuwa ana figo nne.

Hospitali ya Mafunzo na Utafiti ya Kituruki nchini Somalia, iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Digfeer, ilitembelewa na mgonjwa huyu akilalamikia maumivu kwenye figo yake ya kushoto, na madaktari waliamuru uchunguzi ufanyike ambao ulibaini kuwa mgonjwa huyo ana figo nne.

Dk. Abdikarin Hussein Mohamed Gabayre, daktari wa mfumo wa mkojo na upasuaji wa uzazi wa kiume ambaye alimfanyia mgonjwa upasuaji, aliambia BBC jinsi walivyofahamu hali hii.

"Mgonjwa aliyetembelea hospitali aligundulika kuwa na hali hii baada ya kufanyiwa uchunguzi, ilishangaza kwa sababu watu watatu tu ndio walikuwa wanajulikana duniani na atakuwa mtu wa nne, baada ya hapo tukatafuta njia bora ya matibabu ya mgonjwa huyu kwani ni tofauti na watu wengine".

Mgonjwa huyo pia alifanyiwa upasuaji kutokana na maumivu aliyokuwa akiyalalamikia kutokana na jiwe lililokuwa kwenye fupanyonga lake la kushoto.

Faida na hasara ya kuwa na figo nne

Mgonjwa huyo alikuwa akisumbuliwa na mawe kwenye figo kwa muda na madaktari walisema kuwa kunywa maji machafu na kula nyama nyekundu, pamoja na mambo mengi ni chanzo cha mawe kwenye figo.

Kwa mgonjwa huyu mwenye figo nne, figo zake ziko na afya nzuri na zinafanya kazi kwa kawaida, ni dhahiri kwamba figo mbili za upande wa kulia hazitegemei kila mmoja, wakati figo mbili za upande wa kushoto zimeunganishwa kwa sehemu.

Figo ambayo mara nyingi huwa inakabiliana na pombe na bidhaa taka, huwa inakabiliwa na ukuaji wa mawe, jambo ambalo madaktari walieleza kuwa ndio sababu mgonjwa huyu anaathirika zaidi na mawe kuliko watu wa kawaida ambao wana figo mbili.

“Siyo athari au tatizo maalum mgonjwa huyu kuwa na figo nne, bali ni rahisi kupata matatizo ya figo yanayohusiana na mawe, kwa kuwa ana figo nne, anaweza kuhisi maumivu kama watu wa kawaida wana figo mbili lakini maumivu yake ni zaidi ya kawaida,” alisema Dk Gabayre.

Je walio na figo nne ni bora kuliko walio na mbili?

Mgonjwa aliyezaliwa na hali hii ya figo nne anahojiwa kuhusu ubora wa figo zake na iwapo ana manufaa zaidi kuliko watu wenye figo mbili.

Madaktari wanasema kwamba ubora wa figo zake nne ni sawa na mtu mwenye figo mbili na hakuna faida zaidi ya watu wa kawaida, kama ni kwa utendaji na kazi.

Inafaa pia kuzingatia kwamba ikiwa figo zake mbili zitatolewa, ni sawa na mtu aliye na figo mbili, ambayo inamaanisha kuwa ana upungufu.

Madaktari hao waliishauri familia ya mgonjwa kufuatilia na kuchukua uangalizi maalum, na pia walisema kila inapohitajika matibabu anahitaji huduma tofauti na ilivyozoeleka kwa kuwa hali yake ni tofauti na watu wengine.

Unaweza Pia Kusoma

Imetafsiriwa na Jason Nyakundi na Kuhaririwa na Yusuf Jumah