Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kufanana na kutofautiana kwa Kwaresma na Ramadhan
Kwaresma na Ramadhani zimekutana mwaka huu kwa siku kadhaa. Kwaresma ilianza Februari 14 na kumalizika Machi 28 wakati Waislamu wanaanza mfungo wao wa siku 29 au 30.
Kwaresma ni kipindi cha siku 40 ambacho Wakristo hukumbuka matukio yaliyotangulia kifo cha Yesu Kristo, ambaye maisha na mafundisho yake ndio msingi wa Ukristo.
Wakristo wanaamini funga inawakilisha Yesu Kristo alipokwenda jangwani kuomba na kufunga kwa siku 40 kabla ya kufa msalabani.
Ni wakati wa kutafakari na kuomba msamaha, ambapo Wakristo wanajiandaa kusherehekea kufufuka kwa Yesu wakati wa Sikukuu ya Pasaka inayofanyika mwishoni kabisa mwa Kwaresma.
Ramadhani ni jina la Kiarabu kwa mwezi wa tisa wa kalenda ya Kiislamu. Ina umuhimu mkubwa katika Uislamu.
Ni katika mwezi huu ambapo Waislamu wanaamini aya za kwanza za Quran - kitabu kitakatifu cha Uislamu - ziliteremshwa kwa Mtume Muhammad.
Wakati huu, Waislamu wanahimizwa kufunga na kutoa swadaka kwa wingi, kutenda wema na kuimarisha uhusiano wao na Mungu.
Kufanana Ramadhani na Kwaresma
Kufunga na kujizuia
Kufunga ni muhimu kwa dini zote mbili, ingawa ufungaji hutofautiana. Wakati wa Kwaresma, Wakristo hufunga kwa kujiepusha na nyama siku ya Ijumaa na kupunguza ulaji wa vyakula vingine kwa siku 40.
Wakati wa Ramadhani, Waislamu hujizuia kula, kunywa, kuvuta sigara na kufanya ngono kuanzia mawio hadi machweo.
Tafakari ya kiroho
Vipindi vyote viwili vinahimiza kutafakari na kufanya ibada kwa wingi. Waumini wanahimizwa kumkaribia Mungu zaidi, kutafakari uhusiano wao na Mungu, na kutafuta utakaso wa kiroho.
Kutoa sadaka
Kwaresma na Ramadhani zote mbili zinasisitiza kutoa sawadaka na kuwapa wale wasiokuwa navyo. Waamini na waumini wanahimizwa kufanya ukarimu kwa wale wanaohitaji, na hivyo kuimarisha uhusiano na mshikamano wa kijamii.
Kwaresma na Ramadhan zina tofauti gani?
Muda na ratiba
Kwaresma huchukua siku 40, kuanzia Jumatano ya Majivu na kuishia Jumapili ya Pasaka. Wakristo hawafungi siku ya Jumapili.
Kwa upande mwingine, Ramadhani hudumu mwezi mmoja wa mwandamo, kwa hivyo ni siku 29 au 30, kulingana na kalenda ya mwezi ya Kiislamu.
Tabia ya kufunga
Ingawa dini zote mbili zinahusisha kufunga, ufungaji wao unatofautiana. Kufunga katika mwezi wa Ramadhani ni nguzo ya nne kati ya nguzo tano za Uislamu, ambazo zinaunda msingi wa jinsi Waislamu wanavyopaswa kuishi maisha yao.
Nguzo nyingine ni kukiri Mungu ni mmoja, kusali mara tano kwa siku, kutoa zaka kwa mwenye uwezo na kuhiji katika mji mtakatifu wa Makka mara moja katika maisha.
Waislamu hula chakula cha mwisho kabla jua kuchomoza, kinachoitwa daku. Wakati wa mchana, hawatakiwi kula au kunywa chochote - ikiwa ni pamoja na maji au kufanya ngono hadi jua linapozama, na wanafungua saumu yao kwa mlo wa jioni, unaoitwa futari.
Hata hivyo, baadhi ya Waislamu wamesamehewa kufunga. Mfano wanawake wajawazito au wanaonyonyesha na wanawake walio katika hedhi.
Wengine ni wagonjwa au ambao afya zao zinaweza kuathiriwa na kufunga na watu wanaosafiri. Watatakiwa kulipa funga zao au kulisha masikini.
Wakati wa Kwaresma, Wakristo wanaitwa kufanya toba, ambayo msingi wake ni kufunga na kujizuia. Kufunga ni lazima tu kwa waumini siku ya Jumatano ya Majivu na Ijumaa Kuu. Wanaofunga wanaruhusiwa kula mlo mmoja kwa siku.
Kando na Jumatano ya Majivu na Ijumaa Kuu, kujizuia lazima kuzingatiwe kila Ijumaa. Sheria ya kujizuia inakataza ulaji wa nyama, lakini samaki wanaweza kula.
Umuhimu wa Funga kwa Dini Hizi
Vipindi viwili vina maana tofauti za kiimani kwa wafuasi wao. Kwaresma inaadhimisha siku 40 za mfungo wa Yesu jangwani na kuwatayarisha waumini kwa ajili ya kusherehekea Pasaka,
Ramadhani inaeleza uhusiano kati ya Waislamu na waumini wengine waliopita: “Mmefaradhishiwa kufunga kama walivyofaradhishiwa wale walio pita kabla yenu, ili mpate uchamungu” (Qur’ani 2/183) na inaashiria kuteremshwa kwa Qur’ani kwa Mtume Muhammad.
Qur’ani iliteremka katika mwezi wa Ramadhani. Ni mwongozo kwa binaadamu na dhihirisho la wazi la mwongozo na sheria” (Quran 2/185).
Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi