Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, unywaji pombe ni hatari kiasi gani kwa afya?
Katika sehemu nyingi za ulimwengu karamu itakuwa haijakamilika bila pombe. Kwa wengine glasi ya pombe ni njia nzuri ya kuanzisha mazungumzo na watu usiowajua.
Watu hunywa pombe kwa sababu nyingi - kusherehekea, kujumuika, kujiliwaza na hata kuondoa mawazo.
Katika siku za nyuma baadhi ya tafiti zilisema kuwa matumizi ya wastani ya baadhi pombe kama ile nyekundu inaweza kuwa nzuri kwa afya.
Lakini sasa Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema hakuna kiwango salama cha unywaji pombe kwa afya yako.
BBC imechunguza hatari za unywaji pombe.
Saratani na vifo
Unywaji wa pombe huchangia vifo vya watu milioni 2.6 duniani kote kila mwaka, kulingana na ripoti ya hivi karibuni kutoka WHO.
Pombe husababisha aina saba za saratani ikiwa ni pamoja na saratani ya utumbo na matiti.
Utafiti wa kina wa WHO uligundua, hata unywaji mdogo na wa wastani wa pombe, yaani chini ya lita 1.5 ya mvinyo au chini ya lita 3.5 ya bia au chini ya mililita 450 za pombe kali ni hatari kwa afya.
Mwongozo mpya wa WHO unasema, hakuna kiasi salama na hatari kwa afya ya mnywaji huanza na tone la kwanza la kinywaji chochote cha kileo.
Sayansi ilikosea?
Takwimu za WHO pia zinaonyesha, jumla ya unywaji wa pombe kwa kila mtu duniani kote umepungua kidogo kutoka lita 5.7 mwaka 2010 hadi lita 5.5 mwaka 2019. Wanaume ni wanywaji wakubwa na hutumia wastani wa lita 8.2 ikilinganishwa na lita 2.2 za wanawake kwa mwaka.
Dk Tim Stockwell ni mwanasayansi katika Taasisi ya utafiti wa matumizi ya madawa ya kulevya kutoka Canada, na anasadikisha kuhusu usahihi wa onyo la WHO.
"Pombe kimsingi ni kemikali hatari na ni hatari mara tu unapoanza kuinywa."
Alifanya uchambuzi wa kisayansi wa tafiti mia moja na saba, ili kupata uhusiano kati ya unywaji pombe na kifo.
Ikiwa kuna hatari ya kifo kimoja kati ya watu mia moja, inapewa lebo ya wastani na kifo kimoja kati ya watu elfu moja inapewa lebo ya chini ya hatari, linasema jarida la British Medical Journal.
Serikali ya Uingereza inapendekeza kunywa si zaidi ya uniti kumi na nne kwa wiki, ambayo ni karibu glasi sita za wastani za mvinyo au bia.
Stockwell anasema wazo kwamba unywaji pombe wa kiasi ni nzuri lilikuja kwa sababu ya mbinu duni za utafiti. Maswali hayakuwa ya kitaalamu. Na baadhi ya mambo muhimu yalipuuzwa.
Wanywaji wanasemaje?
Lakini sio kila mtu anafikiria hatari zinazohusiana na pombe ni jambo kubwa.
“Kwa kweli sielewi msisitizo huu wa kujaribu kuelewa hatari za kunywa kinywaji kimoja au viwili kwa siku,” anasema Profesa Sir David Spiegelhalter.
Yeye ni Profesa Mstaafu wa Takwimu katika Chuo Kikuu cha Cambridge nchini Uingereza, anaelezea jinsi ambavyo tunaweza kuzielewa hatari.
"Hakuna kiwango salama cha kuendesha gari. Hakuna kiwango salama cha kuishi, lakini hakuna mtu anayependekeza kuacha. Tunahitaji kuangalia kubadilisha madhara kuwa faida."
Dk Spiegelhalte ana shaka kuhusu uwezo wetu wa kukadiria hatari kwa usahihi.
"Nadhani tunapaswa kukubali tu kwamba watu wanakunywa ili kufurahia."
Huku akisisitiza kuwa yeye si sehemu ya watu wanaoshawishi unywaji wa pombe wala kushawishi watu kuwa na kampeni dhidi ya pombe.
Aliambia BBC kwa nini anafurahia unywaji wa kiasi. "Hatari inamaanisha inapunguza wastani wa umri wa kuishi kwa asilimia moja."
"Zaidi ya miaka hamsini ya kunywa, kinywaji hicho kwa wastani kwa siku, kitachukua muda wa miezi sita tu ya maisha yako au kupunguza dakika kumi na tano kila siku."
Dk Spiegelhalte anataja hata kutazama TV kwa saa moja kwa siku au kula mkate wa nyama ya nguruwe, mara mbili kwa wiki pia kuna hatari za kiafya.
Na anataka watu wazima wafanye uamuzi wao wenyewe kuhusu yale yanayowafaa.
Dkt Tim Stockwell, pia anafurahia kinywaji chake na hapendekezi kuacha kunywa.
"Ukinywa pombe, kitu cha kufurahisha sana, ingawa ina hatari kidogo kwa afya yako."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah