Doria na vikosi vya Kenya nchini Haiti katikati ya eneo linalomilikiwa na magenge

Muda wa kusoma: Dakika 4

Shaina mwenye umri wa miaka miwili amefungwa dripu kwenye mishipa katika mojawapo ya hospitali chache zinazofanya kazi katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince. Mama yake, Venda, anatumai sana kwamba itapunguza utapiamlo ambao msichana huyo aliyedhoofika anaugua.

Shaina ni mmoja wa watoto 760,000 ambao wanakabiliwa na njaa nchini Haiti.

Akiwa na hofu ya vita vya magenge vilivyokuwa vikiendelea eneo jirani , kwa wiki kadhaa Venda aliogopa sana kuondoka nyumbani kwake kumtafutia matibabu binti yake.

Kwa kuwa sasa amefanikiwa kufika katika wodi ya watoto, anatumai hajamchelewesha Shaina.

"Nataka nipate matibabu yanayostahili kwa mtoto wangu, sitaki kumpoteza," anasema huku akitokwa na machozi.

Haiti imekumbwa na wimbi la ghasia za magenge tangu kuuawa kwa rais wa wakati huo Jovenel Moïse mwaka 2021, na sasa inakadiriwa 85% ya mji mkuu uko chini ya udhibiti wa magenge.

Hata ndani ya hospitali hiyo, raia wa Haiti hawako salama kutokana na mapigano hayo, ambayo Umoja wa Mataifa unasema yamesababisha vifo vya watu 5,000 mwaka huu pekee na kuiacha nchi hiyo ikiwa kwenye hatari ya kusambaratika.

Mkurugenzi wa matibabu wa hospitali hiyo anaeleza kuwa siku iliyotangulia, polisi walipambana na washiriki wa genge katika wadi ya dharura miongoni mwa wagonjwa waliojawa na hofu.

Waathiriwa wa ghasia hizo wako kila mahali. Wodi moja imejaa vijana wenye majeraha ya risasi.

Pierre ni mmoja wao.

Anasema alikuwa akirejea nyumbani kutoka kazini aliponaswa katika mapigano ya barabarani, huku risasi ikipenya kwenye mfupa wa ukosi.

"Nadhani kama serikali ingekuwa na utulivu zaidi na kuweka mipango bora ya vijana, wasingejihusisha na magenge," anasema kuhusu vijana ambao wanaunda sehemu kubwa ya vikundi vinavyotishia mji mkuu.

Ili kukabiliana na ongezeko la vurugu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinisha kuanzishwa kwa Ujumbe wa Kimataifa wa Usaidizi wa Usalama (MSS) mnamo Oktoba 2023.

Kikifadhiliwa kimsingi na Marekani, kikosi kinachoongozwa na Kenya kilitumwa Haiti miezi sita iliyopita kikiwa na jukumu la kurejesha sheria na utulivu.

Katika doria katikati ya jiji la Port-au-Prince, uwepo wa ghasia za magenge unaonekana.

Maafisa wa Kenya wanatembea barabarani wakiwa na magari ya kujilinda dhidi ya risasi (APC) kupitia maeneo yenye shughuli nyingi ya mji mkuu ambayo sasa yameachwa bila watu. Maduka na nyumba zimefungwa.

Magari yaliyoteketezwa na vifusi vimerundikwa kando ya barabara kama - vizuizi vilivyojengwa na magenge ili kuzuia kuyafikia magenge hayo.

Msafara huo unapita kwenye vifusi wakati ghafula unaposhambuliwa.

Risasi zilishambulia magari ya APC huku polisi wa Kenya wakijibu kwa bunduki zao kupitia mianya iliopo katika kuta za bandari gari hilo.

Baada ya takriban saa moja ya majibizano ya milio ya risasi, msafara unaendelea.

Lakini si muda mrefu kabla kuna dalili za vurugu za kutisha zaidi za magenge. Mwili wa mwanadamu unaonekana ukiungua katikati ya barabara.

Mmoja wa polisi wa Kenya katika gari letu la APC anasema anashuku kuwa ni mmoja wa mwanachama wa genge la upinzani aliyepatikana na kuuawa na , mwili wake ukachomwa moto ili kutoa onyo la kutisha.

Maafisa wa Kenya kwenye doria yetu kwa sasa wamezoea kuona aina hii ya ukatili katika mitaa ya Port-au-Prince, lakini pia wanatuambia wamechoka.

Maafisa mia nne waliwasili mwezi Juni - lakini ni wachache sana. Mnamo Julai, serikali ya Haiti ilikadiria kuwa kulikuwa na wanachama 12,000 wa magenge yenye silaha nchini humo.

Wakenya hao waliahidiwa polisi wa ziada. Wakati Umoja wa Mataifa uliidhinisha ujumbe huo, kikosi cha 2,500 kilifikiriwa, lakini msaada huo, ambao ulipaswa kuwasili Novemba, bado haujatekelezwa.

Licha ya hali hiyo, uongozi wa kikosi hicho bado una matumaini. Kamanda Godfrey Otunge yuko chini ya shinikizo kutoka kwa serikali ya Kenya kufanikisha misheni hii.

Kamanda wa misheni anasema kuna "uungwaji mkono ni mkubwa" kwa MSS nchini Haiti.

"Idadi kubwa ya watu inadai timu yetu iongezeke na kwenda sehemu zingine ili kutuliza hali," anasema.

Mapambano yanayowakabili yanaonekana wazi katika kituo cha polisi cha zamani cha Haiti, ambacho kilikuwa kimekaliwa na genge lakini sasa kimechukuliwa tena na vikosi vya Kenya.

Bado eneo hilo limezungukwa na magenge na, maofisa wanapoelekea juu ya paa la gari, wanakumbana na milio ya risasi

Maafisa hao wa Kenya walifyatua risasi huku wakitoa wito kwa kila mtu kusalia chini.

Maafisa hao wa Kenya wanasema baadhi ya vikosi vyao vya ziada vilivyocheleweshwa sana vitawasili mwishoni mwa mwaka huu, na hivyo kufikisha jumla ya maafisa1,000.

Na msaada unahitajika haraka. Kuna maeneo huko Port-au-Prince ambayo yako chini ya udhibiti mkali wa magenge ambayo kwa hakika hayawezi kupenyeka kwa polisi.

Katika eneo moja kama hilo, Wharf Jérémie, karibu raia 200 waliuawa na genge moja katika muda wa wikendi moja mapema mwezi wa Desemba.

Kwa jumla, magenge 100 yanakadiriwa kufanya kazi katika eneo la Port-au-Prince, huku wavulana wa chini ya miaka tisa wakijiunga na safu zao.

Na shida inaonekana tu kuwa inaongezeka. Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, Unicef, idadi ya watoto waliosajiliwa katika magenge hayo imeongezeka kwa asilimia 70 kwa mwaka.

Mmoja wa viongozi wa genge ambao wanamiminika ni Ti Lapli, ambaye jina lake halisi ni Renel Destina.

Akiwa mkuu wa genge la Gran Ravine, anaongoza zaidi ya wanaume 1,000 kutoka makao yake makuu yenye ngome juu ya Port-au-Prince.

Magenge kama yake yamezidisha hali mbaya tayari nchini Haiti, na yanajulikana kwa kuchinja, kubaka na kuwatishia raia.

Gran Ravine ni maarufu kwa kutekeleza utekaji nyara ili kupata fidia, kitendo ambacho kimemfanya Ti Lapli apate nafasi kwenye orodha inayotafutwa na FBI.

Imetafsiriwa na kuchapishwa na Seif Abdalla