Utata unaozunguka uhusiano kati ya Kenya na Jamhuri ya Sahrawi

State House Kenya

Chanzo cha picha, State House Kenya

Maelezo ya picha, Brahim Ghali, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Sahrawi (SADR) alihudhuria hafla ya kuapishwa kwa William Ruto huko Kasarani.

Uhusiano wa kidiplomasia wa Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Sahrawi (SADR), ambayo pia inajulikana kama Sahara Magharibi, umezongwa na utata.

Hii ni baada ya Rais William Ruto, kufuta ujumbe aliouchapisha katika ukurasa wa twitter, uliosema Kenya imebatilisha utambuzi wake wa SADR na kuchukua hatua za kuondoa uwepo wa uwakilishi wao nchini humo.

Katika taarifa, Ufalme wa Morocco ulisema uamuzi huo ulifikiwa baada ya Rais Ruto kukutana na Nasser Bourita, mwakilishi wa Mfalme Mohammed VI, ambaye pia ni Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Morocco, katika Ikulu ya Nairobi.

Iwapo uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia kati ya Kenya na Sahara Magharibi ungeathirika, wanadiplomasia wote walioidhinishwa wangepewa notisi ya kuondoka nchini. Hii ina maana kwamba uwakilishi wa kidiplomasia, kimsingi, ungefungwa.

Ikulu ya rais Kenya , haijafafanua sababu iliochangia kufutwa kwa ujumbe huo na haijabainika iwapo wawakilishi wa taifa hilo wataathirika.

Katika ulimwengu wa diplomasia, kusitishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kawaida hufanyika kama matokeo ya kuanza kwa vita au kutokana na matatizo makubwa katika uhusiano kati ya nchi.

State House Kenya

Chanzo cha picha, State House Kenya

Maelezo ya picha, Alitoa tangazo hilo muda mfupi baada ya kupokea salamu za pongezi kutoka kwa Mfalme Mohammed VI, mfalme wa Morocco.

Kwa mujibu wa Mkataba wa Vienna wa 1961 kuhusu uhusiano wa kidiplomasia, uhusiano unapovunjika, nchi mwenyeji lazima itoe usaidizi kwa ajili ya kuondoka haraka kwa wafanyakazi wa kidiplomasia na familia zao.

Hadi wakati ujumbe huo wa twitter uliobatilisha uhusiano huo ulipochapishwa na kufutwa, Kenya ni miongoni mwa nchi 41 wanachama wa Umoja wa Mataifa zilizoitambua Sahrawi na imekuwa mstari wa mbele, kupigania kusitishwa kwa mzozo kati ya Sahrawi na Morocco.

Kwa takriban miaka 35, Nairobi imeunga mkono Jamhuri ya Sahrawi katika harakati zake za kujitawala na kujitegemea.

Wakati wa Uongozi wa Kenya katika Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika Februari mwaka huu, Kenya ilitetea na kuweka kipaumbele mazungumzo katika eneo lenye migogoro la Sahara Magharibi huku Rais wa zamani Uhuru Kenyatta akiitisha majadiliano ya ngazi ya juu Februari 16.

Foreign Affairs Kenya

Chanzo cha picha, Foreign Affairs Kenya

Maelezo ya picha, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Sahrawi Brahim Ghali alipowasili Kenya kuhudhuria kuapishwa kwa William Ruto
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Sahrawi imekuwa ikitaka kujiondoa na kujitawala, msukumo ambao Morocco imepinga vikali na kutupilia mbali mapendekezo ya Sahara Magharibi kuamua mustakabali wake kupitia kura ya maoni.

Cha kufurahisha ni kwamba, Rais wa Sahara Magharibi Brahim Ghali alihudhuria hafla ya kuapishwa kwa William Ruto kama rais wa tano mnamo Jumanne katika uwanja wa Kasarani.

Hii ilikuwa mara yake ya pili jijini Nairobi. Alikuja miaka miwili iliyopita katika ibada ya mazishi ya aliyekuwa rais wa Kenya marehemu Daniel Moi.

Rais Ghali alitoa salamu zake kwa Mzee Moi kwa Kiarabu huku mkalimani akimfuatia. Alimsifu marehemu rais wa zamani kama mwanaharakati wa Afrika ambaye alikuwa na jukumu muhimu katika kuondoa ukoloni wa bara hilo.

Kuhudhuria kwa ujumbe kutoka Sahara Magharibi kulitarajiwa kutaisukuma Morocco kusababisha mzozo mwingine wa kidiplomasia na Kenya . Hata hivyo, uamuzi wa Ruto haujashangaza, mwaka jana uongozi wa juu uligawanyika kuhusu suala la uhuru wa Sahara Magharibi, huku Naibu Rais wakati huo ambaye sasa ni Mkuu wa nchi akiwa na misimamo inayokinzana na aliyekuwa bosi wake, Uhuru Kenyatta.

Mnamo Machi mwaka jana alipokutana na aliyekuwa balozi wa Morocco nchini Kenya El Mokhtar Ghambou, naibu wa Rais wa wakati huo William Ruto alionekana kushikilia msimamo tofauti.

"Mpango wa kujitawala chini ya mamlaka ya Morocco ndio suluhu bora zaidi kwa suala la Sahara," ubalozi ulimnukuu Ruto akisema wakati wa mkutano katika makao ya balozi jijini Nairobi.

Naibu rais wa wakati huo alisema msukumo wa kidiplomasia wa Kenya upo katika msimamo wake wa kutoegemea upande wowote kuhusu mizozo ya kikanda na suala la Sahara halipaswi kuwa tofauti na sheria.

Ruto aliendelea kusema kuwa Kenya na Morocco ndizo zinazoongoza katika kanda zao na akabainisha ushirikiano wao wa pande mbili utanufaisha bara zima.

yyy

Chanzo cha picha, Foreign Affairs Kenya

Maelezo ya picha, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Sahrawi Brahim Ghali alipokuwa Kenya

Hii ilikuwa ishara ya kwanza ya kubatilisha utambuzi wa Sahara ikiwa Naibu Rais wa wakati huo angepanda kiti cha urais. Ilikuwa ni suala la muda tu.

Utata wa kwanza ya kidiplomasia kati ya Kenya na Sahara Magharibi ulitokea mwaka wa 2005 wakati Rais wa zamani wa Kenya, marehemu Mwai Kibaki alipopokea hati za utambulisho kutoka katika ubalozi wake .

Mzozo wa pili ulijiri Februari 2014, wakati Nairobi ilipotoa kibali kwa Sahara Magharibi kuanzisha ujumbe wa kidiplomasia ikiashiria kuanza kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili. Hatahivyo Kenya haina ubalozi huko Sahara Magharibi.

Mgogoro mwengine wa kidiplomasia ulipozuka kuhusu suala hilo, Nairobi ililazimika kumpeleka aliyekuwa Spika wa bunge la Seneti Ekwe Ethuro kutuliza mvutano. Kenya ina uwakilishi wa kidiplomasia mjini Rabat kupitia kwa balozi wa heshima.

Sahara Magharibi ni nchi ya Afrika Kaskazini ambayo inadhibiti sehemu za eneo la Sahara Magharibi.

Nchi hiyo ya Kiislamu iko ndani kabisa ya eneo la Sahara na ilitawaliwa na Wahispania hadi 1976.

Baada ya hapo, chama cha kisiasa katika eneo la Sahara Magharibi kinachojulikana kama Polisario Front (Popular Front for the Liberation of Saguia el -Hamra and Rio de Oro) kimekuwa mstari wa mbele katika harakati za kujiondoa kutoka kwa Wamorocco.