Je, kwanini mitandao ya kijamii inaanzisha aina ya usajili wa kulipia?

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
- Author, Zoe Kleinman
- Nafasi, BBC
Kwanza nikiri – nimelipia kwenye mtandao wa kijamii wa Elon Musk X (zamani Twitter) ili kupata tiki ya buluu.
"Kwanini unampa pesa tajiri mkubwa zaidi duniani?" alifoka rafiki yangu.
Ni kweli, swali lake ni la msingi, lakini nilifanya hivyo kwa sababu mbili. Kwanza, kuna akaunti ghushi chache nizijuazo zinazojifananisha na mimi, na kulipia kunakupa uthibitisho wa akaunti yako.
Pili, kwa sababu nilitaka niweze kutumia huduma za X za AI chatbot na Grok, na kulipia ndio njia rahisi ya kupata huduma hizo. Na nililipia mimi mwenyewe na si BBC.
Lakini hata unapolipia ili upate tiki kwenye jina lako, bado kuna chaguo la kuficha tiki hiyo wakati unaendelea kupata huduma zote kama mlipiaji.
Kuna hisia za ukosoaji kwa baadhi ya watumiaji mashuhuri kuhusu kununua tiki – ili akaunti ionekane vizuri zaidi, badala ya kuipata kutokana na maudhui yako.
Manufaa ya kununua ni kuweza kuandika machapisho marefu na kuyahariri - na nimefurahia kupunguzwa kwa matangazo.
Aina mpya ya biashara

Chanzo cha picha, Azeem Azhar
Johnny Ryan, mtaalamu wa matangazo kutoka Irish Council for Civil Liberties, anasema kwa namna fulani watoa matangazo ni mabwana wa kufurahishwa kuliko watumiaji.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Mtoa matangazo kwa ujumla hajali kuhusu maudhui ya tangazo," anasema.
Kuna msemo wa zamani usemao "ikiwa hulipii bidhaa, wewe ndiye bidhaa" - maana yake, kama unatumia kitu bure, basi kampuni inayokimiliki inachukua taarifa uliyoweka na kuzipeleka kwa makampuni ili zitangaze kwako.
Ni mtindo wa biashara ulioanzishwa na wenye faida kubwa. "taarifa ni mafuta mapya!" Ni msemo niliousikia katika tasnia ya teknolojia, miaka michache iliyopita.
Lakini kuna mabadiliko sasa, makampuni ya teknolojia yanazidi kuangalia usajili wa kulipia kama njia mbadala ya kupata pesa.
Miezi sita iliyopita, Meta ilianzisha usajili wa kulipia bila matangazo kwa Facebook na Instagram barani Ulaya. Ni dola za kimarekani 14 kwa mwezi, kwa vifaa vya mkononi. Kampuni hiyo kubwa ya teknolojia imekataa kuniambia ni watu wangapi wamejisajili kufikia sasa.
Snapchat Plus, iliweka huduma ya kujisajili na usipokee matangazo, imepata watumiaji milioni moja ndani ya wiki chache baada ya kuzinduliwa mfumo huo Juni 2022. Na 2023 huduma ya malipo ya YouTube, ambayo huondoa matangazo, ilifikia watumiaji milioni 100.
Netflix, kwa upande mwingine, ilizindua mpango wa malipo nafuu ya usajili unaojumuisha matangazo, na Amazon Prime ilianzisha matangazo kwenye jukwaa lake la video, na sasa inatoza watumiaji (ambao tayari wamejisajili) ada ya ziada ili kuyaondoa matangazo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Usajili wa kulipia ni "sehemu ya soko ambalo ni jipya na linalokua," anasema Azeem Azhar, mwanzilishi wa jarida la teknolojia la Exponential View.
"Hakuna wateja wapya, kwa hivyo ni lazima ufikirie jinsi utakavyoongeza mapato kwenye biashara yako.”
"Kuna sehemu ya watumiaji wa mtandao ambao wako tayari kulipia, kama vile kuna sehemu ya watumiaji wa mashirika ya ndege ambao wako tayari kulipa ili kupanda ndege haraka zaidi."
Lakini, anaonya, mitandao ya kijamii inapaswa kuwa waangalifu.
Watumiaji ni bidhaa au wateja?

Chanzo cha picha, Getty Images
"Ikiwa kila mtu atalazimika kulipa, utakuwa na watu wachache sana wanaoitumia - kwa hivyo haitakuwa na shughuli nyingi na matokeo yake haitohitajika," anaongeza.
"Kuna tofauti kati ya kuhitaji watumiaji bila malipo ili kuweka taarifa na kuunda maudhui, na watu wanaotaka kulipa zaidi kwa matumizi bora zaidi."
Labda hili ni somo ambalo X tayari imejifunza - ndani ya siku chache baada ya kuzindua mpango wake wa usajili kwa malipo, ilitoa tiki ya buluu bure kwa akaunti zote zilizo na wafuasi zaidi ya milioni.
Haya yanajiri kwa vile majukwaa mengi ya habari yamefaulu kusajili ili upate taarifa. Mwaka jana kwa mfano, Taasisi ya Reuters iliripoti kuwa 33% ya Wasweden walilipia ili kupata habari mtandaoni.
Azhar ana takriban watu 100,000 waliojisajili kwenye Substack - jukwaa linalounganisha watayarishi wa maudhui na hadhira. Ni bure kuchapisha, na Substack inachukua 10% kwenye usajili wa kulipia, pamoja na ada ya ziada ya 3% ya malipo ya mfumo wa malipo wa Stripe.
Substack inasema zaidi ya watu milioni tatu wamejiandikisha ili kupokea maudhui ya watu na makampuni mbali mbali.
"Ni ulimwengu bora zaidi watazamaji wanapokuwa ni wateja badala ya kuwa bidhaa," anasema mwanzilishi wa Substack, Hamish McKenzie.














