Hadithi ya mwanamke aliyelazwa kwa miaka 12 katika hospitali ya magonjwa ya akili kwa sababu hawakuielewa lugha yake

Hadithi ya Rita Patiño Quintero ikawa mada ya hali halisi

Chanzo cha picha, PIANO PRODUCTIONS

Polisi walifika kanisani Juni 8, 1983. Mwanamke huyo, akiwa na nguo chafu, miguu iliyojeruhiwa na kuchanganyikiwa, alitamka baadhi ya maneno ambayo maafisa hawakuweza kuelewa.

Alihojiwa kwa Kiingereza, lakini mawasiliano hayakuwezekana. Na kwa kuwa hakuna aliyejua kile ambacho mgeni huyo alikuwa akisema, alipoteza uhuru wake kwa miaka 12 iliyofuata.

Jina lake lilikuwa Rita Patiño Quintero, mwanamke wa kiasili wa Rarámuri, asili ya Jimbo la Chihuahua, kaskazini mwa Mexico.

Siku hiyo, alikimbilia katika orofa ya chini ya hekalu la Methodist katika jiji la Dentro, magharibi mwa Kansas, Marekani.

Kabla ya mamlaka kufika, mchungaji alimgundua Rita alipokuwa akila mayai mabichi.

Unaweza kusoma

Inaaminika kwamba alifika huko moja kwa moja kutoka kwa ardhi ya Mexico. Hii ni kwa sababu rarámuri ina maana ya "wakimbiaji wepesi" na inatoka kwa lugha ya jamii ya Rará, ambayo ina maana ya mguu, na muri, mwanga.

Kwa kabila hili, kukimbia kuna umuhimu muhimu wa kijamii na kitamaduni.

Rarámuri hukaa kwenye miteremko ya Milima ya Tarahumara, ambayo topografia yake ngumu inawalazimisha kushinda vizuizi, kuvuka vijito na kupanda milima.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Huko Kansas, Rita anaweza kuwa alikabiliana na hali ya ukame na baridi zaidi kuliko milimani.

Alipelekwa kwenye kituo cha polisi, ambako alimpiga afisa wa polisi ambaye alikuwa akijaribu kumsafisha, anasema mtengenezaji wa filamu Santiago Esteinou, ambaye Aprili 2024 alitoa filamu ya hali halisi ya L a Mujer de Estrellas y Montañas " ("Mwanamke wa Nyota na Milima. ", kwa tafsiri), ambamo hadithi yake inasimuliwa kulingana na uchunguzi wa muda mrefu kwenye kumbukumbu na kupitia mahojiano.

Alihitimisha kwamba lazima awe mzaliwa wa asili na kwamba alikuwa ametoka katika nchi fulani ya Amerika Kusini. Lakini ingawa hakuelewa chochote alichokuwa akimwambia, alitoa maoni kwamba maneno ya Rita hayakuwa na maana.

Walimpeleka mahakamani na kuhitimisha kuwa hakuwa na utimamu wa kiakili, kwamba alikuwa hatari kwake mwenyewe, kwa hivyo walimpeleka hospitali ya magonjwa ya akili," Esteinou anaelezea BBC News Mundo.

Rita alikuwa hawezi kuzungumza Kihispania, lugha yake ya asili ilikuwa Rarámuri. Katika mfumo wa mahakama ya Kansas na taasisi ambako alipelekwa, hakukuwa na watafsiri ambao wangeweza kusaidia katika kesi yake.

Mwanamke huyo hakuelewa taratibu za kisheria dhidi yake, hakujua alikuwa wapi wala kwa nini alikamatwa.

Maisha yake yote yaliwekwa alama ya kutengwa, tiba, urasimu wa kitaasisi na upweke. Lakini pia alikuwa mwanamke aliyezungukwa na hekaya na mafumbo.

Rita Patiño Quintero alikuwa nani?

Mchungaji wa kondoo, mkunga, mtaalamu wa mitishamba, fundi, pia dobi (mfua nguo).

Rita alikwenda na kufanya mambo mengi, kulingana na maandishi ya Esteinou, ambayo wifi yake, mpwa wake na majirani kadhaa waliomjua katika ujana wake walishiriki.

Lakini kitu ambacho mkurugenzi anasisitiza kuhusu Rita, ambaye alizaliwa mwaka wa 1930, ni kwamba hakufuata vigezo vya jamii ambako aliishi.

Asili ya Piedras Verdes, baadaye aliishi karibu na eneo la Cerocahui, katika mji katika manispaa ya Urique, Mexico.

Alimiliki kundi kubwa la kondoo, alikuwa "mwanamke tajiri kwa maana hiyo", anasema mtayarishaji filamu huyo. Na pia alikuwa mfadhili: alizalisha jibini na kuichangia kwa jamii.

Lakini siku moja kila kitu kilibadilika na Rita hivi karibuni atakuwa "mtu asiyehitajika" kati ya watu wake.

Majirani wanasema mifugo yake iliibiwa na alishtakiwa kwa kumuua mumewe, jambo ambalo halijawahi kuthibitishwa.

"Mtu mzuri, mzuri sana. Na maisha yangu yote nilisema alikuwa hivyo. Kilichotokea ni kwamba walimtendea vibaya. Ilisemekana kwamba alipigana na mumewe na kumuua", anasema Procópio Mancinas, ambaye aliishi karibu na Rita huko Urique na ambaye anashiriki katika filamu.

"Rita Patiño hakumuua Jerónimo Renterías. Waliiba mbuzi wa Rita Patiño, wakaiba blanketi zake, wakaiba kondoo wake", anaongeza katika hati hiyo.

Imani pia ilienea katika jiji hilo kwamba "amelogwa".

 Majirani wa Rita, kama vile Procópio Mancinas, wanadai kwamba alikataliwa na majirani.

Chanzo cha picha, PICHA KUTOKA KWENYE MAKALA "LA MUJER DE ESTRELLAS Y MONTAÑAS"

Baada ya "hali hiyo ya kulogwa", Rita alipata shida kuwasiliana.

"Kisha nikamwambia mume wangu: 'Nafikiri Rita ni mjinga. Hazungumzi vizuri tena, kama alivyofanya tulipokuwa wadogo.' Alianza kujisemea mwenyewe. Hiyo haimponyi mtu yeyote, hivyo ndivyo anavyokufa kama kichaa", anatoa maoni Soledad Mancinas, mke wa binamu wa Procópio, katika filamu hiyo.

Ukweli ni kwamba Rita alianza kutangatanga na mtoto wake. Na jamii yake ilianza kuogopa. Majirani wanasema hakukaribishwa popote tena.

"Kuna watu walikuwa hawamtaki, alipofika walifunga mlango mara moja. Kisha wengine wakaanza kusema anataka kuwaua. Lakini haikuwa hivyo, alikuwa na njaa, anataka chakula", anasema. Procópio Mancinas.

Esteinou ana nadharia kwamba kwa kweli, Rita angeweza kuwa mtu mwenye ulemavu ambaye hakueleweka na wale walio karibu naye.

Kama matokeo ya kila kitu walichosema juu yake, mtengenezaji wa filamu anasema kwamba viongozi walimchukua mtoto wake, ambaye pia anaonekana kwenye makala.

Kwa nini aliondoka Mexico na jinsi alivyofika Kansas ni siri, Esteinou anasema.

Lakini hili sio jambo gumu kukisia, na kuongeza, haswa wakati wa kuchambua ukweli alioishi.

Ukombozi

Awali mahakama iliamuru mwanamke huyo ajitolee katika hospitali ya magonjwa ya akili ya Larned State, pia huko Kansas, kwa miezi mitatu.

Hali yake ya afya ilipimwa tena mwishoni mwa kipindi hiki, angekuwa Marekani.

Lakini mtetezi wa umma aliyehusika na kesi hiyo hakuwahi kufika mbele ya majaji. Pia hakuweza kuwasiliana naye kwa sababu ya ukosefu wa watafsiri.

Wakati huo huo, timu ya matibabu ilidai kutofahamu asili ya mgonjwa, ambayo iliwakilisha shida kubwa katika kuwasiliana na mtu yeyote wa familia.

Miezi ilipita na kugeuka kuwa miaka. Miaka ambayo Rita hakuweza kuzungumza, peke yake, mbali na utamaduni wake, nchi yake na kupewa dawa bila kutambuliwa kwa ugonjwa kutokana na vikwazo vya lugha.

"Ninaona aina nyingi za ubaguzi na unyanyasaji katika kesi ya Rita. Ni mwanamke wa kiasili ambaye anazungumza lugha isiyoeleweka kabisa, ambaye ni maskini, mhamiaji na pengine ana ulemavu fulani", anasema Mkurugenzi .

Alipoachiliwa, Rita alirudi kuishi katika Milima ya Tarahumara pamoja na mpwa wake na familia yake.

Chanzo cha picha, PIANO PRODUCTIONS

Ilikuwa miaka kumi tu baadaye ambapo hali yake ilibadilika na hali ya kushindwa kwa taasisi kuhusu kulazwa kwake hospitalini kuligunduliwa.

Shirika la Huduma za Ulinzi na Kinga la Kansas, ambalo sasa linajulikana kama Kituo cha Haki za Walemavu cha Kansas, liliamua mnamo 1994 kukagua kesi za wagonjwa ambao walikuwa wamelazwa hospitalini kwa zaidi ya miaka mitano.

Kwa Rita, chombo kilimteua wakili Toria Mroz.

"Moja ya mambo ya kwanza tuliyofanya ni kuangalia rekodi zake za matibabu. Mwanzoni kabisa mwa nyaraka, kulikuwa na kumbukumbu ya ukweli kwamba alikuwa ameonesha kuwa anatoka Chihuahua na kwamba alikuwa asili ya Tarahumara," Mroz. anasema katika makala.

"Ilikuwa katika rekodi yake ya matibabu muda wote alipokuwa huko. Lakini miaka 10 ilipita na bado alikuwa pale. Waliendelea kusema, 'Hatujui anatoka wapi au anazungumza lugha gani," anasema Mwanasheria.

Lakini si hivyo tu, pia kulikuwa na ushahidi kwamba maafisa wa ubalozi mdogo wa Mexico huko Salt Lake City, Utah na Kansas walijulishwa kuwepo kwa Rita hospitalini na mfanyakazi wa kijamii, lakini hawakuwahi kuchukua hatua yoyote ya kumuondoa hospitalini.

Timu ya wanasheria wa shirika hilo iliishtaki hospitali hiyo na zaidi ya watu 30 waliokuwa sehemu ya wafanyakazi wake. Waliomba fidia ya Dola za Marekani milioni 10.

Mchakato wa kisheria ukawa changamoto, hasa kwa sababu Rita hakuweza kutoa ushahidi mahakamani na kwa sababu nchini Marekani kulikuwa na daktari mmoja tu wa magonjwa ya akili mwenye uwezo wa kuelewa Tarahumara, anasema Esteinou.

Mwanamke huyo aliachiliwa na kurudi Mexico mnamo 1995.

Santiago Esteinou anasema kwamba katika hadithi ya Rita aina kadhaa za ubaguzi kama vile kabila na jinsia vimebainika

Chanzo cha picha, PIANO PRODUCTIONS

Lakini kesi hiyo ilianzia 1996 hadi 2001 na kuishia kutatuliwa kupitia makubaliano ya fidia ambayo yalikuwa chini sana kuliko kiasi cha awali kilichoombwa na mawakili.

Kwa kila kitu alichopitia katika miaka hii 12, mwanamke huyo alipokea dola za Marekani 90,000 (karibu R$476,000), lakini kati ya hizo alilazimika kutenga kiasi cha Dola za Marekani 32,641 (karibu R$170,000) kwa shirika lisilo la kiserikali (NGO) iliyomsaidia yeye na wanasheria wao.

Pesa zilizobaki, ambazo zilipaswa kumsaidia Rita kurudi katika nchi yake, zina hadithi yake.

Kuishi milimani na kupoteza pesa

Rita anatazama upeo wa macho ameketi kwenye kilima. Nywele zake zote ni nyeupe, ngozi yake imekunjamana. Mbele kuna milima tu na kila kitu karibu ni msitu.

Esteinou anaonesha tofauti na hospitali katika filamu yake. Mwanamke huyo, hatimaye yuko huru, kwa sauti yake mwenyewe na katika lugha ya Rarámuri, anasikika.

- Unajisikiaje, Rita?

- Najisikia vizuri, sikuwa mgonjwa.

- Je, una furaha kuishi katika milima?

- Nina furaha sana kuwa hapa.

- Huna huzuni?

- Ninahisi vizuri sana kuishi na asili.

Muongozaji alianza kurekodi mnamo 2016, lakini filamu hiyo ilikamilishwa mnamo 2022.

Katika kipindi hiki alikutana na Rita na mpwa wake, Juanita, ambao walimtunza.

Ingawa alijisikia vizuri katika nchi yake, Esteinou alishuhudia jinsi Rita alivyolazimika kuishi maisha duni, licha ya fidia iliyoamriwa na mahakama ya Marekani.

Kurudi kwenye Milima ya Tarahumara, Rita aliishi katika umaskini

Chanzo cha picha, PIANO PRODUCTIONS

"Mahakama iliunda akaunti na kumteua mtawa aitwaye Beatriz Zapata, aliyechaguliwa na shirika, kuwa msimamizi wa mali ya Rita.

Kwa takribani miaka miwili, walianza kutoa karibu dola 300 kwa mwezi na kisha dola elfu 6. Kisha mtawa huyo alitoweka na pesa hizo,” anasema msanii huyo wa filamu.

Baada ya miaka kadhaa, mahakama ilimwita mtawa huyo kwa sababu alikuwa ameacha kuripoti malipo kwa Rita. Iligundulika kuwa pesa nyingi tayari zilikuwa zimetumika.

Na ingawa hakimu alimwamuru alipe mara mbili ya ile aliyotumia, mtawa huyo alitoa dola 10,000 tu.

Wasimamizi wawili wapya waliteuliwa, wakipokea $1,000 kila mwaka kwa ajili ya kusimamia akaunti ya Rita. Wote wawili walidai kuwa hawakuweza kugundua aliko mwanamke huyo na baada ya miaka kumi, pesa hizo ziliisha.

Aliaga dunia mnamo 2018 na akafanyiwa karamu ya kuagwa katika jamii yake.

Rarámuri wanaamini kwamba kusherehekea kifo husaidia marehemu kwenda kwenye safari nyingine ya maisha, ambayo ni asili yao: nyota zinazoangaza milima ya Tarahumara.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga