Mwanasayansi wa mishipa ya fahamu asiyeamini uwepo wa hiari

Chanzo cha picha, DIVULGAÇÃO
- Author, Margarita Rodriguez
- Nafasi, BBC
Daktari wa mishipa ya fahamu (neva), Robert Sapolsky, ambaye ni profesa wa biolojia na elimu ya neva katika Chuo Kikuu cha Stanford, nchini Marekani, anaamini hakuna hiari.
Ni mmoja wa wanasayansi wanaoheshimika na jarida la New Scientist, Sapolsky alitumia miongo mitatu kuwasoma nyani wa mwituni nchini Kenya.
Katika kitabu chake kipya, Sapolsky anadai "nyuma ya kila wazo na tendo kuna mlolongo wa sababu za kibayolojia na kimazingira. Hakuna mahali popote katika mlolongo huu ambapo hiari inahusika."
Hiari ni nini?
Kwa mujibu wa profesa huyo, njia bora ya kuelezea hiari ni kuelezea kile ambacho sio hiari.
"Mazingira ya kufanya maamuzi yapo kila siku, kwa mfano, kuchagua nini cha kula. Lakini hilo halihusiani na hiari," anafafanua.
"Nchini Marekani, mfumo mzima wa sheria unatokana na wazo kwamba watu wana chaguo na hufanya wakijua wangeweza kufanya uamuzi tofauti."
"Ili kufanya uamuzi, tunakuwa na nia. Tunajua matokeo yatakuwaje, pia tunajua tunapaswa kufanya nini na kipi hatupaswi kufanya, tunajua njia mbadala. Kwahiyo kwa baadhi ya watu, hiyo huitafsiri kuwa ndio hiari."
Lakini, kulingana na Sapolsky, mtazamo wake juu ya hiari unakwenda mbali zaidi ya hapo.
Hoja ya kisayansi

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Sapolsky anasema ubongo unapoamuru jambo fulani, huamuru kutokana na kitu fulani kilichotokea muda mfupi kabla.
"Kwangu mimi, kila kitu ni matokeo ya yale yaliyotangulia," anasema. "Huu ni ulimwengu ambao hakuna kinachotokea bila maelezo. Kinachotokea hutokea kwa sababu ya kile kilichotokea hapo awali."
Sapolsky aliacha kuamini katika uhuru wa kuchagua alipokuwa kijana. Katika majadiliano kuhusu hiari, kuna swali ambalo kwa Sapolsky ni la msingi: nia zetu zinatoka wapi?
Sapolsky anaeleza kwamba neuroni yoyote (seli ya mfumo wa neva) hufanya kazi kama matokeo ya kile ambacho maelfu mengine ya niuroni zinazoizunguka zinafanya.
Kama hoja ya kutetea nadharia yake, anaomba kuonyeshwa "mishipa ya ubongo ambayo tabia zake hazitegemea matendo mengine au matendo ya kibaolojia yaliyopita".
Anasema tufikirie ujana wetu, utoto wetu, tulipokuwa tumboni. Neuroni zako zimeundwa na jeni ulizoanza. Na kabla ya hapo. Babu zako walikuwa wafugaji au wakulima? Je, waliishi katika msitu au jangwa?
Kile ambacho mababu zako walifanya kitapitishwa karne baada ya karne katika kila kizazi na kuchonga ubongo wa watoto wao ili awe na maadili sawa ya kitamaduni. Na tabi hizo zitakwenda kwenye mifumo mingine ya utendaji ya mwili.
Mfano mwingine ni homoni. Ikiwa tuna kiwango cha juu cha homoni fulani, hii inaweza kuathiri tabia zetu, kwa mfano, tabia ya kukasirika sana au kufanya vitu vya hatari au ubongo unavyojibu jambo fulani.
Sapolsky anatukumbusha kwamba homoni hudhibiti jeni na jeni zinahusiana sana na ufanyaji wa maamuzi.
Kwa kuzingatia haya yote, analeta changamoto: “nendeni mkabadilishe mambo hayo yote. Nionyeshe ubongo wako ulizalisha tabia isiyotegemea homoni, na ukiweza kufanya hivyo, nitakubali kuna hiari," anasema.
Kwa mwanabiolojia wa neva, katika karne ya 21 tuna maarifa mengi ya kisayansi ambayo yameonyesha jinsi jeni, homoni na mazingira ni mambo ambayo kwa pamoja, hutufanya sisi ni nani.
"Si juu yangu kuthibitisha kwamba hiari haipo. Nadhani mzigo wa uthibitisho ni kwa watu wanaosisitiza kuwa hiari ipo,” anasema.
"Nionyeshe homoni zinazofanya kinyume na kile ambacho homoni inatakiwa kufanya kikawaida. Nionyeshe jinsi ulivyobadilisha mlolongo wako wa DNA. Fanya hivyo kisha tutazungumza kuhusu hiari."
Hoja kinzani

Lakini kuna maana gani ya kujitahidi kufanya maamuzi bora ikiwa mwishowe, kama asemavyo katika kitabu chake, hatuna hiari kutokana na biolojia yetu, mazingira yetu na mwingiliano kati ya hayo mawili.
Ingawa katika historia kumekuwa na watu wenye kutilia shaka uhuru wa kuchagua, wapo wengi pia ambao wanatetea kuwepo kwake.
Adam Piovarchy, mtafiti katika Chuo Kikuu cha Notre Dame, anasema, Sapolsky anafanya makosa kudhani kwamba maswali kuhusu uhuru wa kuchagua hujibiwa tu kwa kuangalia sayansi inasema nini.
Anaongeza kuwa hiari pia ni swali la kiroho na maadili, jambo ambalo wanafalsafa wamekuwa wakijifunza kwa muda mrefu.
John Martin Fischer, mwanafalsafa na profesa katika Chuo Kikuu cha California, mtaalamu wa hiari, pia anatilia shaka mbinu ya mwanasayansi wa neva.
“Sayansi ni jambo zuri, lakini hilo halilifanyi swali kuhusu hiari kuwa swali la kisayansi.”
Mwandishi Oliver Burkeman, katika makala yake iliyochapishwa The Guardian, anasema, kusema kuwa hatuna uhuru kunaweza kutugeuza kuwa viumbe wa ajabu.”
Keiran Southern aliandika katika gazeti la The Times "ikiwa mawazo ya Sapolsky yangekubaliwa, yangesababisha mabadiliko makubwa ya kijamii, hasa katika mfumo wa haki na jinai."
Sapolsky anataka kutushawishi kwamba hiari haipo, ikiwa atashindwa, angalau anatualika kuwa na mawazo kuwa hiari ipo kidogo kuliko vile inavyopaswa kuwepo.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi












