"Nililazwa hospitalini kwa miaka 50 licha ya kutokuwa na ugonjwa wowote"- Charles Esler

Na Lucy Adams
Mwandishi wa Masuala ya Kijamii, BBC News
Charles Esler aliishi zaidi ya miaka 50 ndani ya milango iliyofungwa ya hospitali licha ya kutokuwa na ugonjwa wowote mbaya.
Charles, ambaye ana matatizo kidogo ya kujifunza na kifafa, alilazwa hospitalini kwa mara ya kwanza alipokuwa na umri wa miaka 10.
Aliiambia BBC kuwa aliadhimisha sherehe nyingi za "siku ya kuzaliwa" hospitalini na hakupenda alivyokuwa amefungiwa bila kuwa na uhuru.
Dada yake Margo anasema alipigania Charles kuhamishwa hadi mahali ambapo angeweza kujitegemea na mwaka jana, akiwa na umri wa miaka 62, hatimaye alipewa funguo za nyumba yake mpya kwa mara ya kwanza.

Chanzo cha picha, MARGO MCKEEVER
Uchunguzi wa BBC Scotland umegundua kuwa mamia ya watu wenye ulemavu wa kujifunza bado wamekwama katika hospitali au wanaishi umbali wa mamia ya maili kutoka zilipo familia zao.
Hii ni licha ya miongo kadhaa ya sera ya serikali ambayo imethibitisha wazi kwamba lazima wote waondoke kwenye taasisi za kuwatunza wa muda mrefu na kurejea makwao.
Miaka miwili na nusu iliyopita, Serikali ya Uskoti iliahidi kwamba watu "wengi" wangehamishwa katika nyumba zao kufikia mwezi Machi mwaka 2024.
Hata hivyo, takwimu mpya ambazo BBC ilizipata zinaonyesha kuwa idadi ya watu hospitalini imeongezeka.
Ombi la taarifa kutoka kwa mamlaka chini ya Sheria ya Uhuru wa Habari lilifichua kuwa idadi ya watu wenye ulemavu wa kujifunza hospitalini imeongezeka kutoka watu 173 hadi 191 tangu mwaka jana.
Takwimu za jumla katika sajiri mpya ya kitaifa, inayojumuisha watu walio mbali na nyumbani, ziliongezeka kwa 12%, kutoka 1,243 hadi 1,398.

Chanzo cha picha, MARGO MCKEEVER
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Walezi wa Charles wanasema kisa chake kinaonyesha kwamba kila mtu anaweza kusaidiwa kuishi katika jamii.
Bi Fleming alisema: "Aliishi vyema katika kipindi cha kurejea katika maisha yake huru na sasa anafanikiwa na anajitegemea sana.
Charles, aliyelelewa Glasgow, alisema: “Sasa ninaweza kutoka na kwenda mahali fulani, kwenda kwenye baa ndogo iliyo chini ya barabara na kula chakula cha mchana huko.”
"Ninapenda samaki na vibanzi(chips). Ninajisikia vizuri sana. Sijawahi kujua uhuru hapo awali."
Anasema anapenda kukaa sebuleni kwake na kutazama filamu za James Bond. Alijifunza kupika, kutunza bustani na kufanya kazi zake za nyumbani.
Dada yake Margo McKeever anasema alipigana kwa miaka mingi ili kaka yake apate nafasi yake.
"Haikutokea mara moja watu wengi walihusika na ilichukua karibu miaka 14 kupata eneo lake linalofaa la kuishi.
"Kila mtu anapaswa kuwa na mtu ambaye anaweza kuhakikisha kuwa unachukuliwa kama binadamu wengine na sio namba tu."

Chanzo cha picha, MARGO MCKEEVER
Fraser Malcolm ameishi katika hospitali hiyo kwa zaidi ya miaka mitatu, ingawa ilikubaliwa kuwa alikuwa tayari kuondoka.
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 20, kutoka Ayrshire Kaskazini, Uskochi, ana matatizo ya kuzungumza na mahitaji tata, lakini kabla ya kulazwa hospitalini wazazi wake wanasema aliishi maisha kamili.
Alihudhuria shule ya wataalamu, alisafiri kwa meli mara kwa mara, akaenda likizo na familia yake na akamsaidia baba yake kukarabati mashua.
Wazazi wake walisema kosa lake kubwa lilikuwa "kuomba msaada."
Mama yake Fraser, Karen, anasema mwanawe amekuwa na hali mbaya zaidi tangu alazwe hospitalini na hofu ya kufungwa hospitalini "inamuathiri mtu kuliko alivyokuwa zamani."
Anaongeza kuwa "anasikitishwa sana " kwamba idadi ya watu wenye ulemavu wa kusoma imeongezeka tangu mawaziri waahidi kuwarudisha watu nyumbani.
"Hili limekuwa pigo kubwa kwa familia yetu na kwa familia nyingine nyingi ambazo sasa ninawasiliana nazo," alisema. "Tunahisi kudharauliwa."

Familia ya Fraser imemwandalia chumba maalum na wanataka arudi nyumbani, lakini wanasema hali yake imekuwa mbaya sana hospitalini hadi anaogopa kuondoka chumbani kwake.
Kama familia nyingi, walikuwa na shida kupata pesa zinazofaa za utunzaji na hivyo kukubali kupata usaidizi katika kipindi cha mabadiliko ya kuhama kutoka hospitalini.
Msemaji wa Mamlaka ya Afya na Huduma ya Kijamii ya North Ayrshire amesema mamlaka hiyo itaendelea kufanya kazi na Fraser na familia yake ili kuhakikisha anaachiliwa na hospitalini.
"Kuna changamoto zinazoendelea ndani ya nchi na kote Uskochi katika suala la uwezo, upatikanaji na wa huduma za jamii kwa watu wenye mahitaji magumu ya msaada," alisema.
Duru mbali mbali za afya zilizozungumza na BBC Scotland kote nchini humo zilifichua kuwa zaidi ya watu 120 waliokuwa na matatizo ya kujifunza walikuwa wamelazwa hospitalini kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Kati yao, 28 wamelazwa hospitalini kwa miaka 10 na wanne kwa zaidi ya miaka 20.
Miaka miwili iliyopita, BBC iligundua kuwa watu wenye ulemavu wa kujifunza walikuwa wamekwama hospitalini.
Kati ya vijana waliopatikana, akiwemo Fraser Malcolm, wote bado wamenaswa, wakiishi ndani ya vyumba vya hospitali vyenye milango iliyofungwa.
Kyle Gibbon sasa ana umri wa miaka 37 na ameishi Carstairs, hospitali ya umma, kwa miaka 15.
Jamie ana umri wa miaka 26 na bado anaishi katika Hospitali ya Woodlands View huko Ayrshire na Arran. Amekuwa huko tangu akiwa na umri wa miaka 19
Louis Sainsbury sasa anaishi vyema nyumbani huko Perthshire baada ya kulazwa hospitalini kwa miaka mingi.
Maelfu ya watu wenye ulemavu wa akili waliishi katika hospitali za muda mrefu kabla ya miaka ya 1990, wakati ilitambuliwa kuwa maisha hayo hayakuwa ya kibinadamu.
Mnamo mwaka wa 2000, Serikali ya Uskoti ilichapisha ripoti inayoonyesha haki ya watu wote wenye ulemavu wa kujifunza kuishi katika nyumba zao na jumuiya.
Wataalamu wanasema inawezekana kabisa kwa kila mtu kuishi katika nyumba yake mwenyewe kwa usaidizi ufaao.

Chanzo cha picha, MALCILM FAMILY
Dk Sam Smith, mkurugenzi wa C-Change Scotland, shirika linalosaidia watu wenye ulemavu kuishi nyumbani, alisema: "Tulimaliza kukaa kwa muda mrefu hospitalini zaidi ya miaka 20 iliyopita kwa sababu tulijua kuwa watu wanaweza kuishi ndani ya jamii.
Serikali ya Uskochi inasema imefanya kazi na mamlaka za mitaa kuunda sajili ya kitaifa ya watu wenye ulemavu wa kujifunza ambao wako hospitalini au mamia ya maili kutoka nyumbani, na imetoa pauni milioni 20 (dola milioni 25) kusaidia watu hawa kurejea nyumbani.
Waziri wa Masuala ya Kijamii Maree Todd aliiambia BBC Scotland: "Tumejitolea kabisa kuendeleza suala hili. Lakini kama ripoti hizi zinavyoonyesha, ni vigumu kutatua tatizo hili.
"Jukumu la kisheria liko kwa mamlaka za mitaa na ninafanya kazi nao kwa karibu ili kujaribu kuboresha hali hiyo.
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Yusuf Jumah












