Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Walimpiga risasi baba yangu na mjomba wangu nikishuhudia'
- Author, Michelle Katami
- Nafasi, Sports writer, Kenya
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Alama ya kovu katika upande wa kulia wa kichwa cha James Lokidichi ni kumbukumbu ya kudumu ya mzozo alioukimbia alipokuwa mtoto, akiwa amembeba mdogo wake.
Hata hivyo, maumivu bado yanamuandama, huku akijizuoa kulia, alielezea siku ambayo hatoisahau mwaka 2011 ambapo familia yake iliuawa na watu waliokuwa na silaha na alilazimika kukimbia kutoka nyumbani kwao katika eneo linalojulikana sasa kama Sudan Kusini.
''Walimpiga risasi babangu na mjombangu nikiwaona,'' kijana huyo wa miaka 23 aiambia BBC.
"Waliiteketeza nyumba yetu na mimi pia niliungua, nilikuwa nikiwawalilia baba yangu na mjomba. Walimpiga risasi mama yangu pia. Alikimbia na kutuacha."
"Nilimchukua mdogo wangu wakati mama alipokimbia. Wale [wapiganaji] walisema 'Waacheni hawa vijana'."
Wawili hao hawajawahi kumuona mama yao tangu tukio hilo lilipotokea.
Kuwika na kusaka nafasi kwenye michezo
Ndugu hao wawili hatimaye walifanikiwa kufika nchini Kenya, Lokidichi akiwa ni mmoja wa wakazi 300,000 katika Kambi ya Wakimbizi ya Kakuma.
Baada ya kilichomkuta utotoni, anaamini michezo inaweza kuwa hatua ya kuelekea maisha bora na anatafuta nafasi katika timu ya Olimpiki ya wakimbizi (ROT).
Akiwa mwanariadha wa mbio za kati alikuwa miongoni mwa washiriki zaidi ya 100 katika mashindano yaliyofanyika katika Shule ya Michezo ya Lornah Kiplagat, iliyoko viungani Iten, wiki iliyopita, ambapo Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) ilikuwa ikitafuta wanariadha walio na vipaji, wanajudo na wanataekwondo kuwasaidia kupitia ufadhili wa masomo.
Lokidichi, anahevutiwa na bingwa wa mbio ndefu wa Kenya, Eliud Kipchoge, anatumai kuwapa motisha wakazi wenzake katika kambi ya wakimbizi iliyoko kaskazini-magharibi mwa nchi.
"Tutakapofanikiwa, tutakwenda kuwasaidia wale waliobakia. Tutawashauri wengine katika kambi," alisema.
"Tutawaonyesha kuwa kuna msaada na matumaini kwa ajili ya siku za baadaye. Tukiendelea kujifua pamoja kama timu."
Ndoto ya kuelekea Dakar 2026
Timu ya Olimpiki ya wakimbizi ROT ilishiriki kwa mara ya kwanza katika Michezo ya Olimpiki ya Rio de Janeiro mwaka 2016.
Cindy Ngamba aliyezaliwa Cameroon alikuwa mshindi wa kwanza wa medali katika timu hiyo alipochukua medali ya shaba katika masumbwi, uzito wa kati kwa wanawake katika Olimpiki za Paris 2024.
Timu ya wakimbizi sasa inatarajiwa kuundwa kwa ajili Michezo ya Vijana ya Dakar 2026 - tukio la kwanza kubwa la IOC linalofanyika Afrika.
Laurence Namukiza, kijana mwenye umri wa miaka 15, anatumai kupata nafasi katika kikosi hicho, na ushindi wake wa mara tatu wa Taekwondo katika mashindano ya majaribio unaweza kumsaidia kufikia lengo lake.
Namukiza ni mwanafunzi katika shule moja iliyoko Kakuma, ambayo ilianzishwa na kutambulika kwa jina la mwigizaji wa Hollywood, Angelina Jolie, balozi mwema wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR).
Ugumu wa maisha katika kambi - ambapo misaada ya kila mwezi kwa wakazi ilipunguzwa kutoka shilingi 1,500 za Kenya ($11.60, £9.20) hadi shilingi 950 ($7.40, £5.80) kwa mwezi - ulimlazimisha Namukiza kujiunga na mchezo huo ulipoanzishwa shuleni kwake mwaka jana.
"Nilijiapiza nitajitahidi ili niweze kuwasaidia familia yangu," alisema.
"Utapata familia ya watu 16 lakini chakula kinachotolewa kama msaada ni cha watu watano."
"Kupata kazi ni vigumu ikiwa huna elimu rasmi na vyeti. Mama yangu anateseka kutulea."
"Matokeo na ushindi nitakaopata utaniwezesha kuwaondoa katika kambi ya Kakuma na kuwapeleka sehemu bora."
Namukiza alikuwa bado mdogo wakati familia yake ililazimika kuondoka nyumbani kwao huko Uvira, DR Congo, mwaka 2010.
Akiwa mtoto wa nne katika familia ya watoto tisa, taekwondo imemfundisha maadili ya nidhamu na uvumilivu.
Pia imemsaidia kupambana na mitazamo ya kijinsia na kumwezesha kupata ujuzi wa kujilinda.
"Nakumbuka watu wakiniuliza 'Kwa nini umeingia katika mchezo huu? Ni wa wanaume'," alisema.
"Kwa mafunzo ya taekwondo, sasa najua jinsi ya kupigana. Ninajiamini na naweza kujilinda dhidi ya mtu yeyote anayejaribu kunidhuru, na pia naweza kusaidia wasichana wengine katika kambi ya Kakuma."
"Lakini niko hapa kuonyesha kuwa michezo ni kwa wote na hakuna ubaguzi wa kijinsia."
Matumaini ya siku za baadaye
Mashindano ya ROT yalifanyika kwa kushirikiana na Kamati ya Olimpiki ya Kitaifa ya Kenya (NOC), Athletics Kenya, UNHCR, pamoja na Shirikisho la Michezo la Dunia na Shirikisho zinazohusiana na judo na taekwondo.
Hisia mbalimbali zilionekana katika mazingira ya mashindano, huku kukiwa na matarajio, wasiwasi na uvumilivu ulioonyeshwa kwa nyuso za washiriki.
Kulikuwa pia na hisia kubwa ya uhuru.
"Unapowatoa kwa siku moja au mbili kutoka kambi ya Kakuma, wanajihisi kuthaminiwa na kuenziwa," alisema Paul Tergat, Rais wa Kamati ya Olimpiki ya Kitaifa ya Kenya (NOC), alipozungumza na BBC Sport Africa.
"Hiyo ndiyo maana ni muhimu sana kuwapa nafasi na ufahamu."
Mshindi wa zamani wa mbio za mita 800, Janeth Jepkosgei, ambaye sasa ni kocha wa timu ya ROT pamoja na Shirikisho la Michezo la Dunia, anafahamu michezo huunganisha.
"Ningependa kuwapeleka wanariadha hawa kwenye Olimpiki zijazo na ningependa kuwaona wakifika fainali," alisema mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 41.
"Tungependa kubadilisha kipindi hicho cha huzuni kuwa furaha wanaposhiriki mashindano na kuwa washindi."
Kuhusu hali ya Wakimbizi Nchini Kenya, takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na UNHCR zinaonyesha kuwa Kenya ni nyumbani kwa zaidi ya wakimbizi 820,000 waliosajiliwa na waombaji hifadhi.
Na vita vya kiraia vikiendelea nchini Sudan na mapigano yakiongezeka mashariki mwa DRC, idadi hiyo inaweza kuongezeka.
"Hakuna anayependa kuwa mkimbizi," alisema Tergat.
"Tunataka kutumia michezo kuwapa heshima na hadhi. Wao ni ndugu zetu, kwa hiyo tunahitaji kuwapa hii fursa ya kukuza vipaji vyao na kuwahamasisha."
Mwisho wa mashindano, washindi walitambuliwa lakini jambo moja lilikuwa wazi - ushindi haukuwa na maana ya uteuzi wa moja kwa moja kwa ufadhili wa IOC.
Wanariadha walirudi Kakuma na wanasubiri kuona kama watafanikiwa na kuchaguliwa kuwa katika kikosi hicho.
Wana matumaini wakati huu wakisubiri hatma ya ushiriki wao.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid