Sexting: Jinsi ya kuwazuia vijana athari za kutuma jumbe za ngono kwenye simu za mikononi

Mojawapo ya hatari ya kutuma ujumbe wa ngono ni kwamba picha za faragha zinaweza kuangukia kwenye mikono isiyofaa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mojawapo ya hatari ya kutuma ujumbe wa ngono ni kwamba picha za faragha zinaweza kuangukia kwenye mikono isiyofaa.
    • Author, Santiago Vanegas
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Teknolojia imebadilisha kwa kiasi kikubwa mahusiano ya kijamii.

Kwa vijana, mabadiliko haya yameleta hali ambapo uamsho wao wa kihisia na kingono huanzia kupitia jumbe za mitandaoni.

Hali hii imezua dhana ya ''sexting'' yaani kutuma au kupokea jumbe, picha au video zenye maudhui ya kingono kupitia simu ya mkononi.

Ingawa tabia hii imeenea sana miongoni mwa watu wazima, pia imeanza kuonekana kwa vijana.

Kwa mujibu wa utafiti uliochapishwa kwenye jarida la JAMA Pediatrics, mtoto mmoja kati ya watatu mwenye umri wa miaka 12 hadi 17 amewahi kupokea ujumbe wa faragha wenye maudhui ya kingono kupitia simu ya mkononi.

Wataalamu, akiwemo Dkt. Corinne Cross, msemaji wa Chama cha Madaktari wa Watoto wa Marekani (AAP), wanatahadharisha kuwa tabia hii inaweza kuwa na madhara makubwa, hasa pale ujumbe wa faragha unapofika mikononi mwa watu wasiostahili.

Hii ndiyo sababu jukumu la mzazi au mlezi linakuwa la msingi mno.

Pia unaweza kusoma:

"Ni jukumu letu kuwasaidia watoto wetu kuepuka makosa yanayoweza kuwasababishia madhara makubwa," anasema Dkt. Carol Spekho, mwanasaikolojia kutoka taasisi ya Child Mind Institute.

"Sexting ni moja ya mambo ambayo, yakifanywa bila tahadhari, yanaweza kuwa na madhara ya kina na ya muda mrefu."

Dkt. Corinne Cross anaongeza kuwa vijana mara nyingi hawana uwezo kamili wa kutathmini madhara ya matendo yao kwa sababu sehemu ya ubongo inayohusika na maamuzi (frontal lobe) huwa bado haijakomaa.

"Tunachopaswa kufanya ni kuwasaidia kuona athari zinazoweza kujitokeza, ili wakijikuta katika mazingira hayo, wakumbuke mazungumzo tuliyowahi kuwa nao," anasema.

Hata hivyo, kwa wazazi wengi, si rahisi kuzungumzia mada hii kwa sababu mara nyingine huonekana kuwa ya faragha au ya aibu.

Kwa hiyo, wataalamu wanashauri yafuatayo kama mbinu madhubuti za kuanzisha mazungumzo haya.

1. Zungumza naye kabla hajaingia kwenye mazingira hatarishi

Kulingana na Corrine Cross moja ya makosa makubwa ambayo wazazi hufanya ni kusubiri hadi tatizo litokee ndipo waanze kulizungumzia.

Kwa mujibu wa Dkt. Cross, sexting huweza kuanza mapema kuanzia umri wa miaka 12, wakati watoto wanaanza kuwa na hisia za kuvutiwa na wengine.

"Huu ndio wakati ambapo mtoto anaweza kukusikiliza," anasema. "Watoto mara chache sana huwataarifu wazazi pale mtu anapowaomba picha ya faragha."

Cross anasema kosa la kawaida ambalo wazazi hufanya ni kusubiri kwa muda mrefu sana ili kuzungumza na watoto wao kuhusu kutuma ujumbe wa ngono.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Cross anasema kosa la kawaida ambalo wazazi hufanya ni kusubiri kwa muda mrefu sana ili kuzungumza na watoto wao kuhusu kutuma ujumbe wa ngono.

Dkt. Yolanda Reed wa Chuo Kikuu cha California, Los Angeles, anaeleza kuwa ni muhimu mtoto awe na maarifa kuhusu sexting kabla hajakutana nalo moja kwa moja.

"Mazungumzo haya yanapaswa kuanza mara tu mtoto anapopewa simu ya mkononi," anashauri.

Njia bora ya kuanzisha mazungumzo ni kumuuliza mtoto anajua nini au amesikia nini kuhusu mada hiyo.

Kisha, mzazi anapaswa kumpatia maelezo sahihi kulingana na umri wake.

Kwa watoto wadogo, eleza kwamba ujumbe wa aina yoyote haupaswi kuwa na picha au video za watu waliovua nguo, wakibusiana au wakigusa sehemu za siri.

Kwa vijana, zungumza kwa uwazi kuhusu maana ya sexting na waulize moja kwa moja kama wamewahi kuona picha za utupu au nusu utupu mitandaoni.

"Mazungumzo haya hayatakiwi kuwa ya mara moja tu, bali yawe endelevu," anasisitiza Dkt. Cross.

2. Jiweke kwenye nafasi ya mtoto wako

Kosa jingine linalofanywa na wazazi ni kutoa marufuku ya moja kwa moja bila kuelewa hali halisi ya kihisia ya kijana.

"Tunawaambia watoto wetu, 'Kama mtu anakutaka utume picha ya faragha, huyo ni mtu mbaya. Usimjibu.' Lakini hawafuati ushauri huo kwa sababu hatujaelewa wanavyohisi," anasema Cross.

Inawezekana mtu anayemwomba picha ni mtu anayemvutia kijana kimapenzi.

Katika hali kama hiyo, ni vigumu kwake kusema hapana.

Dkt. Spekho anashauri kwamba mazungumzo yaanze kwa kukiri kuwa kutuma picha au jumbe za kingono kunaweza kuonekana kama jambo la kuvutia au la kukubalika.

"Hakuna ubaya kwa kijana kutamani kujisikia anavutia au anatamanika," anasema.

Kushirikiana maelezo ya faragha mara nyingine huwa njia ya vijana kujenga mahusiano ya karibu, jambo ambalo ni sehemu ya ukuaji wao.

Espekho anasema kushiriki maelezo ya faragha ni sehemu ya kuwa kijana

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Espekho anasema kushiriki maelezo ya faragha ni sehemu ya kuwa kijana

"Kupenda mtu haimaanishi kufanya kila wanachotaka," anashauri Cross. "Katika uhusiano wenye afya, lazima kuwe na mipaka. Ni muhimu kijana ajue mapema mipaka yake ni ipi."

Wafundishe kwamba mtu anayewaheshimu atakubali maamuzi yao, hata kama ni ya kukataa kushiriki katika tabia hiyo.

Kulingana na yeye, ushauri huo una athari kubwa kwa watoto na vijana kuliko kusema, "Usifanye hivi."

3. Lenga matokeo ya kitendo, si kuhukumu

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Badala ya kuzungumzia kama sexting ni sahihi au si sahihi, elekeza mazungumzo katika kuelewa athari za muda mfupi na mrefu.

"Usiwe mkosoaji wala mkaripiaji katika mazungumzo haya," anashauri Dkt. Spekho ambaye ni mwanasaikolojia. "Mtoto wako anapaswa kujisikia huru kukuamini."

Waeleze kwamba mara tu picha inaposhirikishwa, haiwezi kufutwa kabisa. Inaweza kusambaa bila mipaka na kumletea madhara ya kijamii, kihisia au hata kisheria.

"Ukifikiria kuwa picha hiyo itakua ya kuaibisha ikionwa na bibi, mwalimu au mtoto wako wa baadaye basi usiitume," anashauri Cross.

Kwa mujibu wa JAMA Pediatrics, asilimia 14.5 ya vijana hutuma ujumbe wa faragha bila idhini ya mhusika.

Mara nyingi, picha hizo husambazwa si kwa nia mbaya bali kwa kudhaniwa kuwa ni salama kushiriki kwa watu wa karibu.

"Lakini kila tendo kina matokeo," anasema Spekho.

Cross anaongeza kuwa mara nyingine kijana anapotumiwa picha ya faragha, huona fahari na hutamani kuwaonyesha marafiki zake kama uthibitisho wa kupendwa.

Huwa nawaambia kuwa mahusiano huweza kufa na mnaweza kuachana kwa hasira. Je, itakuwaje mtu huyo akiwa na picha zako za siri?" anauliza.

Jambo la vijana kutuma ujumbe wenye mada ya ngono limekuwa la kawaida miongoni mwa vijana Uingereza.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Jambo la vijana kutuma ujumbe wenye mada ya ngono limekuwa la kawaida miongoni mwa vijana Uingereza.

Dkt. Yolanda Reed anashauri wazazi kutumia taarifa za vyombo vya habari kuhusu athari za sexting kwamtumiwa na anayetumiwa picha hizo kama njia ya kuanzisha mazungumzo ya kielekezo.

"Hiki kinaweza kuwa kisingizio cha kufanya mazoezi na mtoto wako jinsi ya kujibu ikiwa mtu atamwomba kutuma au kupokea ujumbe au picha za faragha," Reed anasema.

Zaidi ya hayo, katika nchi nyingi kutuma ujumbe wa ngono huonekana kuwa ponografia ya watoto na kunaweza kuwa na matokeo ya kisheria.

"Wakumbushe watoto wako kwamba kuna sheria maalum zinazoongoza matendo yao na kwamba ikiwa watakamatwa, wanaweza kukabiliana na madhara makubwa. Imetokea kwa watu wengine," anasema Carol Spekho.

4. Wafundishe kupinga shinikizo

Vijana wengi wamesema waliombwa picha za faragha mara kadhaa kabla ya kuamua kuzituma.

Kwa hivyo, sehemu ya malezi ya mzazi ni kuwasaidia watoto wao kujifunza namna ya kusema hapana bila kujisikia vibaya au kushinikizwa.

"Tunapaswa kuwafundisha watoto kuwa kwenye uhusiano wa heshima, hapana ni hapana iwe kimwili au kidijitali," anasema Cross.

Dkt. Reed anasisitiza umuhimu wa kuwafundisha vijana misingi ya uraia wa kidijitali yaani kuwa na maadili ya matumizi ya mitandao, kutokushinikiza au kushinikizwa kutuma picha za faragha.

Hata hivyo, licha ya jitihada za wazazi, uamuzi wa mwisho uko mikononi mwa kijana.

Hii ina maana kuwa matatizo bado yanaweza kutokea, ikiwemo ujumbe wa faragha kuvuja.

Katika hali kama hizo, Dkt. Spekho anasisitiza umuhimu wa kumkumbusha kijana kuwa:

"Ingawa unaweza kujisikia aibu au kuchanganyikiwa, hilo halipunguzi thamani yake wala hadhi yake kama binadamu."

Mada zinazohusiana:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid