Vita vya Sudan: Walionusurika mauaji ya Wad al-Nourah watoa ushuhuda

Chanzo cha picha, X
- Author, Mohammed Mohammed Osman
- Nafasi, BBC News Arabic
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Kwa mkulima Ali Ibrahim mwenye umri wa miaka 40, jinamizi la mauaji lilianza alasiri ya tarehe 5 Juni kwa sauti ya silaha nzito: "Hatujawahi kuona makombora kama haya tangu tukiwa wadogo. Milipuko hiyo ya mabomu ilidumu kwa saa nne huku nyumba zikiwa zimeharibiwa, watoto wakipiga kelele, na wanawake na wazee wasioweza kutoroka.”
Ni shambulio ambalo liliuwa takribani watu 100 siku hiyo, katika kijiji cha Wad al-Nourah, kwa mujibu wa watu waliojitolea wa kamati ya upinzani ya eneo hilo.
Ali anasema hawakuwa na silaha: “Sisi ni wakulima wa kawaida. Hatujawahi kubeba silaha. Hatuna maadui. Ni raia tu tunajaribu kulinda maisha yetu.”

Chanzo cha picha, X
BBC imesikia ushuhuda kutoka kwa manusura kadhaa wanaowatuhumu wapiganaji wa RSF, kundi la wanamgambo wanaopambana na jeshi, kwa kufyatua mabomu na kuvamia kijiji hicho katika mashambulizi mawili, wakitumia silaha nzito, na kuua na kujeruhi makumi ya wakaazi ndani ya saa chache tu.
Idadi ya vifo katika tukio hilo ni idadi kubwa zaidi ya vifo vya raia ndani ya saa chache tangu vita kati ya Jeshi la Sudan na RSF kuanza Aprili 2023.

BBC ilifanikiwa kuzungumza na waathiriwa kadhaa na manusura wa shambulio la Wad al-Nourah ambao sasa wanapata matibabu katika hospitali ya serikali ya Al Managil, na pia kuchambua video zilizosambazwa.
Hospitali hiyo iko umbali wa kilomita 80 kutoka Wad al-Nourah, na manusura wengi na waathiriwa walifika hapo saa chache baada ya shambulio hilo. Kulingana nao, vikosi vya RSF vilijaribu kuwazuia kuondoka kijijini na kupora magari yao mengi.
Uvamizi wa asubuhi

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Baada ya kupitia masaa ya hofu kutokana na mashambulizi ya mabomu na majaribio ya kutafuta njia ya kuwasafirisha waliojeruhiwa na kuwazika wale waliouawa, wakazi walishtushwa na shambulio kubwa la pili la RSF katika kijiji chao mapema asubuhi iliyofuata, Nisreen mama wa nyumbani na mmoja wa walionusurika sasa akiwa hospitalini aliambia BBC.
"Waliingia nyumbani kwetu, wakanipiga mimi na ndugu zangu, na kuuliza, 'dhahabu iko wapi?' Dada yangu mdogo aliogopa na kumwambia mama awape dhahabu, ilikuwa na thamani ya mabilioni ya pauni za Sudan."
Maelezo ya Nisreen yanalingana na yale ya manusura wengine, ambao wote walithibitisha kwamba vikosi vya RSF, vilivamia kijiji kutoka pande tatu, viliingia ndani ya nyumba, kuwaua raia, na kupora vitu vya thamani, ikiwa ni pamoja na dhahabu, magari, na mazao ya kilimo yaliyohifadhiwa."
Hamad Suleiman, mfanyabiashara wa rejareja mwenye umri wa miaka 42, alisema wapiganaji wenye silaha wa RSF waliingia kwenye nyumba ya kaka yake na kuanza kufyatua risasi ovyo.
"Nilikwenda nyumbani kwa kaka yangu na kukuta wamewapiga risasi na kuwauwa, kaka na mpwa wangu, na mpwa mwingine alijeruhiwa na yuko nami hapa hospitalini."
Alijaribu kujadiliana na wapiganaji wa RSF na kuuliza kwa nini wameua familia yake. Akasema, "wakaniambia nisome Shahada. (Tamko la Kiislamu wakati mtu anapohisi kifo kinakaribia).
“Walinipiga risasi mkononi na wakaondoka. Wakapora magari yote. Na nilijeruhiwa na sikuweza kupata njia ya kutoka kwa masaa mengi."
Majibu wa RSF

Tuliwasiliana na RSF ili kutoa majibu kwa kauli za walionusurika na shutuma za mashambulizi, mauaji, uporaji na vitisho. Hata hivyo, hatukupokea jibu kufikia wakati wa kuchapishwa kwa ripoti hii.
Lakini msemaji wa RSF, Al-Fateh Qurashi, alitoa taarifa ya video kwenye X (zamani Twitter), siku moja baada ya tukio hilo, akikana kwamba walikuwa wakiwalenga raia.
Alisema vikosi vyao vilikabiliana na vikosi vya jeshi la Sudan (SAF) na vikosi vya ujasusi, vijuulikanavyo kama Al Mustanfaron, wanamgambo wanaobeba silaha ndogo na wanaoshirikiana na SAF, ambao walikuwa kijijini wakati wa shambulio hilo.
Uchambuzi wa picha
Timu ya BBC ya kutafuta ukweli ilichambua video zilizotolewa na RSF, ambazo walidai zinaonyesha maeneo na mitaro inayotumiwa na "Al Mustanfaron" huko Wad al-Nourah. Uchambuzi ulibaini maeneo haya yote yalikuwa nje ya kijiji, sio ndani.
Uchambuzi huo pia ulionyesha wanachama wa RSF walifyatua makombora kuelekea ndani ya kijiji, kwa kutumia silaha nzito kutoka umbali wa maili moja.
Wad al-Nourah ni mamia ya vijiji vilivyotawanyika katika Jimbo la Gezira. Wakazi wake wengi wanafanya kazi za kilimo na biashara, na kuna soko dogo la kila wiki ambapo wafanyabiashara kutoka vijiji jirani huja kununua na kuuza mifugo na mazao.
RSF ilichukua udhibiti wa jimbo la Gezira, kusini mwa mji mkuu, Khartoum, mwezi Desemba na imekuwa ikishutumiwa kutekeleza mateso mengi dhidi ya raia – tuhuma ambazo inakanusha mara kwa mara.
Jimbo la Gezira limekuwa mojawapo ya majimbo yaliyoathiriwa zaidi na vita hivyo, kwani mapigano yalifika huko mapema, na pia likawa kimbilio la maelfu ya watu waliokimbia makazi yao huko Khartoum na Darfur.
Tangu RSF ilipochukua udhibiti wa eneo hilo mwishoni mwa mwaka jana, kijiji kimoja baada ya kingine kimekumbwa na vitendo vya ukatili.
RSF inaendelea kukanusha tuhuma za kufanya uhalifu wa kivita kama vile kuua, uporaji, ubakaji na kuchoma vijiji na badala yake inawanyooshea kidole wale wanaowaita "watu wasio watiifu."
Wito wa uchunguzi

Kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa (UN), vita vya Sudan vimesababisha vifo vya watu 14,000 na kuwalazimu watu milioni mbili kuyakimbia makazi yao tangu Aprili mwaka jana, wakati Sudan ilipotumbukia katika machafuko baada ya jeshi lake na wanamgambo wenye nguvu kuanza mapambano makali ya kuwania madaraka.
Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa wa Misaada ya Kibinadamu nchini Sudan, Clementine Nkweta-Salami, ametaka uchunguzi wa kina na wa uwazi ufanyike ili kubaini mazingira ya shambulio hilo.
Wanakijiji waliopoteza makumi ya wapendwa wao wanatumai, kamati ya uchunguzi itaundwa na wahusika watawajibishwa, badala ya kukwepa adhabu kama ilivyotokea huko nyuma nchini Sudan.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah








