Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je Afrika inahitaji nini kushinda Kombe la Dunia?
Na Nishat Lada
BBC Sport
Mkufunzi wa timu ya Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Sebastien Desabre anaamini nchi za Afrika zinahitaji kuboresha viwango vya viwanja vyao iwapo zinataka moja ya timu zao kushinda Kombe la Dunia.
Kauli ya Desabre ilikwenda sambamba na uamuzi wa Shirikisho la Soka Afrika kuiongeza Ghana katika nchi zilizopigwa marufuku kuandaa mechi za kimataifa.
Mkufunzi huyo Mfaransa aliyeiongoza Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kutinga nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2023 mwaka huu, anaamini kiwango cha uchezaji barani Afrika kinaimarika, ukosefu wa viwanja hauwasaidii makocha kufanya kazi zao.
Aliiambia BBC: "Kwa bahati mbaya, baadhi ya viwanja na baadhi ya vifaa havifikii kiwango cha malengo ya Rais wa CAF, wala kufikia kiwango cha malengo ya mashirikisho." "Hii ndio sababu Afrika inaona kuwa vigumu kupata matokeo mazuri," aliongeza.
Benin, Kenya, Madagascar na nchi nyingine zililazimika kuwa mwenyeji wa wapinzani wao katika mechi za kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika 2025 katika viwanja visivyoegemea upande wowote wa timu kwa sababu viwanja vyao havikukidhi mahitaji ya Umoja wa Afrika ya kuandaa mechi za kimataifa.
Ghana inatarajia kujiunga na kundi hilo mwezi ujao, kutokana na hitilafu za kiufundi katika uwanja wa Baba Yara, ikiwa ni pamoja na kutoridhishwa na ubora wa uwanja, huko Kumasi.
Wizara ya vijana na michezo ya Ghana imeitaka CAF kukagua viwanja vingine nchini. Iwapo hawataidhinishwa, Black Stars italazimika kucheza mechi yao dhidi ya Sudan mwezi ujao nje ya nchi.
Morocco ilitinga nusu fainali ya Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar na kuwa timu ya kwanza ya Afrika kutinga hatua ya nne bora. Lakini Desabre anaamini kuwa kuboresha vifaa ni muhimu kwa timu za Afrika kupata matokeo bora.
"Kiwango cha uchezaji wa kulipwa kinaimarika," alisema mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 48. "Baada ya zaidi ya miaka 10 barani Afrika, nimeona mabadiliko katika CAF, katika mashirikisho ya ndani, katika shule za mpira wa miguu. Nina uhakika kwamba kuna wakati timu ya Afrika itashinda Kombe la Dunia."
"Lakini tunapaswa kuendelea kujenga viwanja na kuboresha viwanja vya mazoezi, kusaidia wakufunzi na wachezaji, kufurahia na kupata matokeo mazuri," aliongeza.
Desabre alikuwa mmoja wa wakufunzi wa kitaifa waliohudhuria kongamano la makocha nchini Ivory Coast, lililoandaliwa na Umoja wa Afrika.
Lengo la jukwaa hili ni kutathmini matokeo ya mwisho ya Kombe la Mataifa ya Afrika, ambalo lilifanyika nchini, na kufikiria njia za kuboresha kiwango cha mashindano ya baadaye.
Desabre anasema jukwaa hilo ni fursa nzuri ya kuzungumza na makocha wenzake walioshiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2023, hasa wakati ambapo mechi za kufuzu michuano ya mwaka 2025 nchini Morocco zimeanza.
"Kuna uhusiano na kuheshimiana kati yetu," anaongeza. "Kazi ya kila mkufunzi wa soka inaweza kuwa tofauti, lakini ni muhimu kila mmoja wetu afaidike na wengine, kuendeleza maarifa yake kila wakati, na kujifunza masomo kutoka kwa mafunzo yaliyopita."
Timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imepata matokeo mazuri katika mechi za kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika 2025, kwani ilishinda mechi mbili za kwanza katika kundi hilo, dhidi ya Ethiopia na Guinea.
"Kushinda mechi mbili za kwanza ni muhimu kwa ajili ya kujiamini," alisema Desabre. "Lakini kuna mechi sita zaidi, na huu sio mwisho, kwa sababu hatujafuzu bado."
"Tunapaswa kuweka malengo yetu kwa ajili ya mechi ijayo mwezi Oktoba," aliongeza.
Mechi za kufuzu kwa ajili ya michuano ijayo ya Kombe la Mataifa ya Afrika, itakayoandaliwa na Morocco, zitamalizika mwezi Novemba, ikimaanisha timu zitalazimika kusubiri zaidi ya mwaka mmoja kabla ya michuano hiyo kuanza.
Fainali hizo zitafanyika kuanzia tarehe 21 Desemba 2025 hadi tarehe 18 Januari 2026.
"Nadhani ingekuwa bora kama mashindano yataanza baada ya kufuzu," Desabre anasema. "Lakini hilo ndilo linalofanyika katika mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia pia."
"Sisi ni wataalamu na tunatakiwa kukabiliana na hali ya sasa," aliongeza.
Aliendelea kusema kuwa: "Tunashughulikia mechi moja baada ya nyingine. Ni muhimu kwa timu yetu, mashabiki wetu, na nchi yetu kushinda mechi inayofuata, iwe ni katika mechi za kufuzu, mechi ya kirafiki, au katika Kombe la Dunia."
Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi