"Nimempenda mwanamke huyu maisha yangu yote!": wanandoa ambao walilazimika kungojea miaka 45 kuwa pamoja

Alipokuwa na umri wa miaka 9, Irene alipelekwa kwenye makazi mapya ya vijana (hostel) katika eneo la Sunderland, nchini Uingereza, ambayo yalikuwa ni makazi ya tatu kuhamia tangu azaliwe.

“Walinipeleka huko kwa sababu mama yangu alifariki nikiwa mdogo sana,” anaeleza Irene.

Alan, ambaye alikuwa na umri wa miaka 7 wakati huo, alimuona akiwasili kupitia kwenye dirisha la nyumba. “Irene alishuka kwenye gari na, alipomwona, na hisia fulani zilianza kunipata ,” asema.

"Nilienda kwenye mlango wa mbele na wanawake ambao walikuwa wakisimamia na mara moja nilijitolea kumuonyesha eno la makazi."

Irene anakumbuka jambo hilo wazi: “Kulikuwa na mvulana aliyekuwa akingoja mlangoni - nitamkumbuka daima - na, kwa urahisi, mara tu nilipomwona, urafiki wetu ulianza. Baada ya hapo tulikuwa pamoja kila wakati.”

Waliunganishwa kwa kuwapoteza mama zao na kutengwa na ndugu zao.

"Tulikuwa na uhusiano mzuri,"anasema Irene. Na hiyo, wakati huo, ilimaanisha “kila kitu, kila kitu tu”.

Wavulana na wasichana katika makao hayo hawakuruhusiwa kuzungumza wao kwa wao au kucheza pamoja, lakini Irene na Alan hawakuwahi kutengana.

"Tulizungumza jinsi tunavyotamani mama zetu wangekuwa hai, na tukajiuliza familia zetu zingine walikuwa wapi," anasema Irene.

"Tulikuwa tukienda kwenye kilima cha Bunny, kilima kilichokuwa karibu, kucheza; "Tulikuwa na wakati mzuri."

"Tungeenda kisiri na kurudi nyumbani peke yetu, bila kutazamana," anakumbuka.

"Ilikuwa vigumu sana, kufanya hilo , lakini ilibidi."

Kuwa katika makao ya watoto ilikuwa kama kuwa mfungwa, anasema Alan.

Nyakati zangu za kuwa na Irene zilileta tofauti : "Kuwa pamoja kulikuwa kitu cha bure na wazi. "Tuliweza kuzungumza juu ya jambo lolote."

Siku moja, huko Bunny Hill, Alan aliomba kumuoa Irene.

“Nakumbuka nilimpa ua la msituni nikamwambia: 'Tukikua nataka kukuoa, utakubali kuolewa nami ?' Naye akanitazama na kusema, ‘Ndiyo, lakini itabidi usubiri kidogo.’.”

"Nilijua tulikuwa kwenye matatizo makubwa."

Kila kiangazi, makazi hayo ya watoto yaliwachukua watoto hao kwa safari ya kwenda Whitby, mji wa kando ya bahari huko North Yorkshire, Uingereza.

Katika matembezi hayo, Alan na Irene waliamua kuepuka tahadhari walizokuwa wamewekewa na kukimbia "kama washenzi" pamoja.

Lakini mmoja wa wasimamizi wa makazi aliwashangaza katikati mchezo wao wa kufurahisha.

Siri yake ilikuwa imefichuka. Na wasimamizi walikasirika.

"Nilijua tulikuwa katika matatizo makubwa,"Alan anakiri, "lakini hatukujua matokeo yangekuwaje."

Walikuwa wakali kuliko walivyoweza kuwazia.

Miongo kadhaa baadaye, Alan na Irene walirudi mahali ambapo walikamatwa pamoja.

Asubuhi iliyofuata, Irene alipoenda shule, "Alan alichukuliwa."

Alipowauliza alikokwenda, walimwambia kuwa amechukuliwa.

Lakini ulikuwa uoongo.

"Waliniingiza kwenye gari na kunipeleka kwa mwendo wa kasi hadi upande ule mwingine wa jiji hadi kwenye makazi mengine ya watoto," Alan asema.

"Lilikuwa tukio la kuhuzunisha sana... ghafla nilijipata mahali pa ajabu tena, nikiwa na watu wapya na hakuna wa kuungana naye."

Nakumbuka nikijihisi mwenye hatia. Irene angejisikiaje? Je, unaweza kuwa na wasiwasi kwamba ulifanya kitu kibaya?

Alianza kukimbia kutoka kwa nyumba mpya na kujaribu kutafuta njia ya kurudi alipokuwa rafiki yake.

Hakuwa na wazo la kufika huko, lakini kwa namna fulani, hatimaye, alifanikiwa.

Katikati ya msimu wa baridi, alingoja usiku kucha katika makazi hayo. Lakini kesho yake asubuhi alipoenda kumchukua Irene kwenye kituo cha basi, polisi walimzuia na kuondoka naye.

Alihisi “haja kamili ya kumuona Irene”, lakini kila alipotoroka, walimburuta hadi nyumbani.

"Ulikuwa wakati mzuri na mbaya zaidi"

Miaka mingi baadaye, rafiki wa kike wa Alan wakati huo alimtaja mtu fulani kwenye gym yake aitwaye Irene, ambaye alisema alikuwa katika makao ya watoto.

"Nilitetemeka,"Alan anakumbuka, "na nikafikiria, hii inawezekana?"

Alimpeleka rafiki yake kwenye mazoezi, alipotazama nje alimuona Irene.

"Ulikuwa wakati mzuri na mbaya zaidi ,"anasema Alan.

Wote wawili walikuwa kwenye uhusiano, hawakuweza kueleza jinsi walivyohisi kweli walipokutana.

Lakini wakati huo huo walihisi "tamaa" ya kuwa pamoja.

“Nilitaka kutoroka naye na kuacha kazi yangu, kuacha kila kitu na kukimbia, lakini sikuweza”, anasema Irene.

"Ilikuwa vigumu sana," anasema Alan, lakini walijua kuwa wakati haukuwa sawa.

"Ilitubidi tuwe pamoja kwa asilimia mia moja na hatukutaka kitu chochote kituzuie."

Na hivyo wakatengana, kwa mara ya pili.

Alan alikwenda Uskochi kufanya kazi. Irene alifikiri hatamuona tena.

Lakini miaka michache baada ya kukutana kwenye ukumbi wa mazoezi, alimuona.

"Nilikuwa nikiendesha gari langu nikitembea katika jiji na nikamuona Alan," anasema Irene.

"Nilihisi hisia ya kusisimua, kwa sababu nilijua alikuwa amerudi. Na nilikuwa naenda kumtafuta.”

Kwa muda wa miezi mitatu walitafutana.

Alan alikwenda madukani kila siku na alitumia saa moja au mbili kuzunguka huku na huko, akijaribu kumtafuta Irene.

"Kila mwaka walitoweka."

Saa 1 asubuhi mnamo Mei 10, 2004 - karibu miaka 45 tangu walipotengana mara ya kwanza - Irene alimwona Alan barabarani.

"Nilipiga kelele nikiita jina lake. Naye, mara tu aliponiona, alinikimbilia, akaninyanyua hewani na kuanza kupiga kelele: 'Nimempenda mwanamke huyu maisha yangu yote!' "Ilikuwa kama sitamuacha tena."

"Wakati huo ulikuwa ni msukumo wa hisia tu,", Alan anasema.

"Miaka yote ambayo ilikuwa imepita ilitoweka na tulikuwa wavulana wawili kwenye kilima tena."

Akipiga kelele kwa hisia alimwambia: “Niko huru! "Siko na mtu yeyote, tunaweza kuwa pamoja!"

Wakiwa wamekumbatiana, walizunguka huku na huku, wakipiga kelele za furaha mbele ya umati ulioshangaa.

"Ilikuwa kama ulimwengu wote ulikuwa umebadilika wakati huo.

"Kila kitu tulichokuwa tumepitia kilififia tu na kuacha kuleta maana. Tulikuwa pamoja tena,” anasema Alan.

“Milele,” Irene anaingilia kati. "Wakati huu sasa ni milele".

Walikula chakula cha jioni pamoja na “tulikesha tukizungumza kuhusu maisha yetu na kile kilichotokea tangu tutengane,” anasema Irene.

"Na tangu wakati huo hatujawahi kuacha kuzungumza," anaongeza Alan.

Urafiki wa utotoni hivi karibuni uligeuka kuwa uhusiano wa kimapenzi.

"Tulitengana kwa njia fulani kama marafiki na familia, lakini tulipokutana, ulikuwa upendo," Alan anasema.

"Mara nilipomwona, nilimpenda mara moja."

Mnamo 2007 hatimaye walifunga ndoa, karibu miongo mitano baada ya ombi la awali la Alan katika mlima wa Bunny Hill.

Katika fungate yao walikwenda Whitby, mahali ambapo walikuwa wanacheza kwa upendo na kisha kulazimishwa kutengana.

“Kwa kweli, ilikuwa ni kulipiza kisasi kwa taasisi iliyo,” anasema Irene. "Kusema hivyo, licha ya yote, tulijikuta na kurudi pamoja".

Maisha ni “mazuri” sasa, asema Irene.

"Familia yangu inampenda Alan kabisa."

Na hisia ni sawa: "Nimepata familia mpya," anasema mumewe.

“Siku hiyo tulipokutana tena, nilihisi kuwa tuko nyumbani,” asema.

"Na ndivyo hivyo," mke wake anasisitiza tena.

“Bado tuna furaha nyingi; tunachekeshana. “Huo ndio wakati mzuri zaidi maishani mwetu,” asema Alan.

"Inapendeza kabisa... Maisha yangu yalianza tena siku tulipokutana tena".

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi